*Wakabidhiwa Takukuru kwa mahojiano 

*JAMHURI yadhihirisha umahiri wake

licha ya Mkurugenzi wa Jiji kutishia 

kulishitaki kwa kuandika habari hiyo 

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Hatimaye yametimia. Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwasimamisha kazi vigogo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa Sh bilioni 10 za serikali zilizokusanywa pasipo kuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.

Waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri na wenzake tisa.

Majaliwa ametoa maagizo hayo Julai 11, 2022 alipozungumza na viongozi wa Dar es Salaam, wabunge, madiwani na watumishi wa Wilaya ya Ilala wakati wa ziara yake ya kikazi jijini humo.

Maagizo hayo yanatokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa mapato ya ndani katika halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika hatua nyingine, watumishi hao wamekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dar es Salaam kwa mahojiano kuhusu tuhuma zinazowakabili.

Mbali na Shauri, watumishi wengine ni Tulusubya Kamalamo (Mweka Hazina), James Bangu (Mhasibu Mapato), Abdallah Mlwale (Mtunza Fedha Mkuu) na Mohammed Kaisi (Mhasibu wa Masoko).

Watumishi wengine wanaotajwa kutakiwa kuchukuliwa hatua ni Jesca Lugonzigwa (Ofisa Hesabu), Josephine Sandewa (Ofisa Hesabu), Tatu Mkangwa (Kibarua) na Felician Maro (Mhasibu Msaidizi) ambao wameisababishia halmashauri hasara ya Sh 1,214,907,637.

“Watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hivyo kuisababishia halmashauri hasara ya jumla ya kiasi cha Sh 10,137,577,401 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki,” amesema.

Amewataja mawakala wanaodaiwa kufanya udanganyifu wa makusanyo ya mapato kwa kuchezea tarehe za mashine za PoS kwa kuzirudisha nyuma hivyo makusanyo ya kiasi cha Sh 131,356,400 kutoonekana katika taarifa za makusanyo kuwa ni Kampuni ya Pick Trading Ltd na Workers General Supply.

“Ripoti ya CAG imebaini kuwa wataalamu wa halmashauri waliohusika na upotevu wa mapato walikuwa wakiingilia moja kwa moja kati ya mfumo wa LGRCIS na benki na kuandika katika mfumo malipo yasiyofika benki.

“Kwa lengo la kuficha ukweli wa kasoro na matumizi ya fedha kinyume cha sheria za fedha za umma. Pia wahasibu waliingiza katika mfumo kiasi ambacho hakikupelekwa benki kwa lengo la kupotosha taarifa halisi za makusanyo. Licha ya Ilala kupata hati safi lakini ndani yake kuna mambo hayana tija,” amesema.

Pia ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo ufuatilie vyanzo vyote vya mapato na waweke makadirio yatakayowawezesha kukusanya zaidi na kila mhusika atekeleze majukumu yake ipasavyo.

JAMHURI la kwanza kuripoti 

Katika toleo namba 530 la Novemba 23 hadi 29, 2021, Gazeti la JAMHURI lilikuwa la kwanza kuripoti tuhuma za ubadhirifu huo.

Katika habari hiyo, liliripoti idadi ya vigogo watano wa halmashauri hiyo kusimamishwa kazi kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa ufisadi wa mabilioni ya shilingi. Huku CAG akiwa ameanza kufanya ukaguzi huo maalumu kubaini upotevu wa fedha hizo za mapato yanayokusanywa kupitia PoS.

Wakati huo alipozungumza na JAMHURI ofisini kwake, Shauri, akathibitisha kuwapo kwa ukaguzi huo.

Akawataja waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni Kamalamo, Bangu, Rutataza, Mlwale na Kaisi.

Uchunguzi huo umekuja baada ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, kutilia shaka ukusanyaji wa mapato wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 ambayo ni asilimia 26 ya lengo.

“Ni kweli kuna ukaguzi ila wanaochunguza si TAMISEMI, ni CAG na hadi sasa hivi hakuna kiasi cha fedha kilichotajwa kupotea,” amesema Shauri.

Amesema tuhuma zilizopo si za wizi, bali ni kutaka kujua kwa nini makusanyo yamegota asilimia 26? Shauri hakutaka taarifa hizo za ukaguzi zichapishwe katika JAMHURI.

“Ni kweli kuna ukaguzi ila wanaochunguza si TAMISEMI bali ni CAG na hadi sasa hivi hakuna kiasi cha fedha kilichotajwa kupotea,” amesema na kuongeza:

“Pia si kwamba kuna tuhuma za wizi ndiyo maana kuna ukaguzi, hapana. Nakushauri acha kuandika hiyo habari tunaweza kukushitaki halafu ukatulipa mabilioni. Hata kama watakutwa na hatia haina haja ya kuiandika.

“Kwa kuwa kuna ukaguzi ndiyo maana hao watumishi wa jiji ikabidi wasimamishwe ili uchunguzi ufanyike, kwa sababu isingewezekana wao wabaki ofisini wakati uchunguzi unaendelea.

“Ukaguzi ukishamalizika watarudi ofisini kuendelea na majukumu yao. Tumwache CAG afanye kazi yake na hata akimaliza ukaguzi huo ataandika ripoti yake ambayo itapatikana kuanzia mwakani, hebu tusubiri kwanza.”

Taarifa zilizopatikana wakati huo kutoka kwa vyanzo tofauti vya habari ndani ya Idara ya Fedha na Biashara ya halmashauri hiyo zimesema vigogo hao walipewa barua za kusimamishwa kazi Novemba 4, 2021.

“Hizo barua za kuwasimamisha zimetoka TAMISEMI, kwa sababu kuna special audit. Barua zimetoka masjala ya siri na wakakabidhiwa Alhamisi jioni (Novemba 4, 2021) kisha wote wakajifungia ofisini kuzijadili,” kimesema chanzo kimoja na kuongeza:

“Mashine za PoS zilianza kutumika mwaka 2004, kwa maana ya kukusanya mapato kwa mfumo au kwa kutumia njia ya kielektroniki tofauti na ule wa zamani wa kutumia ma-cashier.

“Jiji ni kama kuna mtandao wa hao watu ndiyo maana TAMISEMI ikaunda timu ya kuchunguza. Hizo PoS ziko zaidi ya 50 na tuhuma za upotevu wa mapato zimeibuka kwa sababu kuna ushirikiano kati ya vijana wanaokusanya hizo fedha na watu wa IT.

“Kwa mfano, inawezekana zikakusanywa Sh laki tano kwa siku, lakini katika mfumo wa hesabu za makusanyo kule ofisini ikaonekana kwamba kilichokusanywa ni Sh elfu hamsini tu.”

Pia chanzo kingine kimesema vijana wanaokusanya mapato hayo kwa kutumia mashine hizo wanapewa mikataba mifupi ya ajira, sababu inayoweza kuwashawishi kufanya vitendo vya hujuma ya mapato.

“Ni sahihi kabisa kufanya ukaguzi huo kwa sababu vijana wanaokusanya mapato wanapewa mikataba ya ajira ya mwaka mmoja au miwili, ndiyo maana watu wa IT ni rahisi kuwamudu,” kinasema chanzo chetu.

Vijana wanaotumia mashine hizo kukusanya mapato nao walihojiwa wakati huo katika jengo la DMDP lililopo Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, chanzo kingine kimesema tuhuma hizo zimeibuka kwa sababu mtandao idarani hapo umeota mizizi, kwa kuwa kuna baadhi ya watumishi wamedumu muda mrefu katika nafasi zao.

“Kwa kawaida idara yoyote ile inayohusu fedha lazima kuwe na rotation (mzunguko) ya watumishi katika nafasi zao,” kimesema chanzo hicho.

Dosari nyingine inayotajwa ni kwa baadhi ya watumishi wa idara, hasa zinazohusu fedha na mipango, kukaa sehemu moja kwa kipindi kirefu sana.

Kunatolewa mfano kuwa wapo baadhi ya watumishi waliodumu katika nafasi hizo tangu Charles Keenja akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji la Dar es Salaam miaka ya 2000 hadi leo.

Hii ni mara ya kwanza kwa CAG mwenyewe kufanya ukaguzi katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kwa kawaida kuna wakaguzi wa nje wanaotoka ofisi ya CAG na wanakuja mara mbili, ikiwamo katikati na kabla ya mwaka wa fedha wa serikali haujafungwa na kuna wakaguzi wa ndani wanaokagua kila siku. Lakini ukaguzi huu maalumu ni mara ya kwanza,” kimesema chanzo hicho.