Hatimaye waandishi wa habari, Christopher Gamaina na wenzake wawili wa jijini Mwanza wameachiwa huru kwa dhamana ya mahakama.
Wanakabiliwa na tuhuma ya unyang’anyi wa kutumia nguvu wa Sh milioni tatu, katika kesi namba 11 ya mwaka 2018.

Kila mmoja amedhaminiwa na watu wawili kwa kusaini hundi ya maneno ya shilingi milioni tatu, kila mmoja.

Kesi hiyo inatokana na kinachodaiwa kuwa ni ufuatiliaji wao wa habari dhidi ya mtu mmoja wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza.

Gamaina, Zephania Mandia na Manga Misalaba wameachiwa Agosti 5, mwaka huu katika Mahakama ya Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza, baada ya kukaa gerezani tangu Aprili 18, mwaka huu.

Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza iliwafutia hukumu ya miaka 30 jela ya Aprili 18, mwaka huu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Magu.
Waliondolewa Gereza la Magu na kusafirishwa hadi Gereza Kuu la Butimba Julai 19, mwaka huu, kuanza kutumikia adhabu ya miaka 30 jela, kabla ya uamuzi mwingine wowote kufanyika.

Baada ya kufutiwa kifungo hicho, Mahakama Kuu iliamuru kesi yao inayowakabili ya unyang’anyi wa kutumia nguvu ianze kusikilizwa upya.

Pia, katika uamuzi huo Mahakama Kuu kupitia Jaji Mustapha Mohamed Siyani, imeelekeza kesi hiyo isikilizwe na hakimu mwingine na si yule aliyewahukumu kifungo cha miaka 30.

Pamoja na mambo mengine, ilifutilia mbali ushahidi wa serikali dhidi ya waandishi hao wa habari wa vyombo tofauti.

“Kusikilizwa upya kwa kesi hii ni kulinda haki ya pande zote mbili (interest of justice) kwa serikali na watuhumiwa,” Jaji Siyani amenukuliwa wakati akiwafutia kifungo wanahabari hao.
Katika kesi hiyo, waandishi wa habari Gamaina, Zephania na Manga, wanatetewa na mawakili wawili, Constantine Mutalemwa na Linus Amri.

Mmoja wa waandishi wa habari hao, Gamaina, amesema kuwa wanaamii haki itatendeka katika kesi hiyo inayoendelea. Kwa sasa wapo nje kwa dhamana.

Gamaina ameushukuru uongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) kwa ushiriki wao wa karibu katika kesi hiyo.

Katika mahojiano na gazeti hili, wanahabari hao wamesema tangu waanze maisha yao Gereza Kuu la Butimba, Mwanza, walijitolea kuwa walimu ndani ya gereza hilo kubwa.

Pamoja na mambo mengine, walikuwa wakiwafundisha masomo mbalimbali mahabusu na wafungwa wengine gerezani humo.

Madarasa yao yaliwalenga waliokuwa wanafunzi kabla ya kufikishwa gerezani humo, pamoja na watu wazima wanaojua au kutojua kusoma na kuandika. Kila mmoja alikuwa na darasa lake.

Gamaina alikuwa anafundisha somo la Jiografia na Uraia (Civics) kwa waliokuwa wanafunzi wa sekondari, kidato cha pili.

Pia alijitolea kufundisha masuala ya uhifadhi na utalii, makosa ya ujangili na vigezo muhimu vya mambo ya habari.

Gamaina amesema kuwa walikuwa na faraja kuwafundisha maarifa mema wenzao gerezani, huku akisema masuala ya uhifadhi, utalii, makosa ya ujangili na mambo ya habari anayajua vema.

Manga Misalaba, alikuwa akifundisha somo la Hesabu, Kiswahili na Civics kwa wanafunzi wa sekondari, kidato cha pili na cha tatu kabla hawajapatikana na hatia au tuhuma wakiwa uraiani.

Zephania Mandia, yeye alijitolea gerezani Butimba kufundisha Chekechea kupitia somo la Kuandika. Wanafunzi wa Chekechea walikuwa ni watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Gamaina amesema waliamua kujitolea kufundisha wenzao ili kuwapa maarifa  endelevu yatakayowasaidia pindi watakapoachiwa huru.

“Wapo baadhi waliokuwa wanafunzi wakakumbwa na tuhuma huku uraiani. Wengine hawajui kabisa kusoma wala kuandika. Sisi tukaona tujitolee kuwafundisha waelewe vitu muhimu.

“Mfano, Zephania yeye alikuwa anafundisha Chekechea kusoma na kuandika A, E, I, O, U. Wapo waliokuwa wanahudhuria masomo ili wajue kusoma na kupata maarifa mema ya kiraia.

“Mbao za kufundishia zimo mle gerezani. Chaki, kalamu na madaftari vilikuwa vinatolewa na Gereza Kuu la Butimba Mwanza,” amesema Gamaina aliyewahi kuandikia magazeti ya Mtanzania, Rai na mengineyo ya Kampuni ya New Habari.

“Mara nyingi waliokuwa wanahudhuria masomo ni wa kuanzia miaka 17, 18 na 19. Walikuwapo pia wa miaka 30, lakini wachache.
“Wengine walikuwa wanakuja pale darasani wanakaa kusikiliza tu masomo. Hawaulizi hata maswali,” amefafanua katika mahojiano yake na JAMHURI.

Gamaina amesema walikuwa wanatunga na kuwapa mitihani ya kujipima wanafunzi wao, kisha kuwasahihisha na kuona uelewa wao.
Alipoulizwa kuhusu muda wa masomo, Gamaina ambaye ni mwakilishi wa Gazeti la Raia Mwema jijini Mwanza, amesema: “Ratiba ya masomo ilikuwa kama kawaida, kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa. Tulikuwa tunatunga na kuwagawia mitihani.”

“Wengi walikuwa wanapata asilimia 80 hadi 100. Hii ilikuwa inatupa picha kwamba kumbe hata mtu aliyepo gerezani hashindwi kitu.
“Ukweli tuliamua kwa dhati kusaidia wenzetu kuwafundisha yaliyo mema,” Gamaina ameeleza.

Akitolea mfano somo lake la uhifadhi, utalii, makosa ya ujangili, nyara na masuala ya kihabari, Gamaina amesema anauelewa mzuri wa mambo hayo, kwani ana cheti cha uhifadhi.

Baada ya hukumu hiyo ya awali kutolewa, Gamaina na wenzake Mei, mwaka huu walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.
Rufani yao hiyo chini ya mawakili wanaowatetea, Constantine Mutalemwa na Linus Amri, walikuwa wakipinga uamuzi wa kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani.
Mara ya kwanza rufaa yao iliitwa Juni 17, 2019, Julai 3 na baadaye Julai 17, kabla ya uamuzi wa kufutiwa hatia uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, jijini hapa Julai 24.
Kufutiwa kifungo kwa waandishi hao wa habari kuliibua shangwe nje ya mahakama dhidi ya wanahabari na raia waliokuwapo.

Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Edwin Soko, walikuwapo mahakamani hapo.

Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) nao walikuwapo mahakamani.

Wakili Mutalemwa na Linus wanaowatetea waandishi hao, baada ya uamuzi huo walimshukuru Jaji Siyani kwa kufuta kifungo hicho.

“Ni hatua nzuri sana kwetu tunaotafuta haki. Mahakama imetoa uamuzi mzuri dhidi ya wateja wetu.

“Kwa sasa waandishi wetu wameondoka kwenye hadhi ya wafungwa,” Wakili Mutalemwa amewaambia wanahabari muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kufutilia mbali adhabu kwa waandishi hao.

Wakili huyo aliwaambia wanahabari nje ya mahakama kuwa, kwa sasa wanaelekea Magu kutafuta haki dhidi ya wateja wao.

Gamaina, Zephania na Manga, walisalia Gereza Kuu la Butimba kabla ya amri ya mahakama ya kutolewa nje.

Baada ya kutolewa kwa Removal Oder walisafirishwa hadi Gereza la Magu, kwa taratibu za kuanza kusikilizwa kesi yao upya na mambo ya dhamana kufanyika kwa mujibu wa sheria.

Katibu Mkuu Mtendaji wa MCT, Mukajanga, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC na uongozi wa MPC, ulieleza kufurahishwa na kufutiwa kifungo kwa wanahabari hao.

Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) kimeeleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa kuachiliwa kwa wanataaluma hao.

Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko, amesema kuachiliwa kwa Gamaina, Zephania na Manga kumefungua ukurasa mpya katika milango ya utetezi wa haki za binadamu.

“Naishukuru sana mahakama kwa hatua hii nzuri. MPC inawashukuru pia waandishi wote wa habari kwa kuonyesha umoja kwenye jambo hili.

“Pia MPC inatoa shukurani za dhati kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa msaada wao kwenye kesi hii,” Soko ameliambia gazeti hili.

Kulingana na Soko, MPC, MCT, THRDC na wadau wengine wa masuala ya haki za binadamu, wanahitaji kuona haki ikitendeka dhidi ya shauri linaloendelea.

Ametoa wito kwa jumuiya za waandishi wa habari, kiraia na vyombo vya dola nchini kuimarisha upendo na mshikamano unaoigwa ulimwenguni kote.

“Tupendaneni,” Mwenyekiti huyo wa Mwanza Press Club ambaye pia ni mtetezi wa haki za kiraia amesisitiza, akiwa anapeleka ujumbe kwa dunia.

Soko ameeleza: “MPC na wadau wengine wa haki za binadamu, wanaamini mahakama itatenda haki dhidi ya kesi hii inayowakabili Gamaina, Zephania na Manga. Ustaarabu ni muhimu zaidi.”

Kesi hiyo ya wanahabari imepangwa tena kuitwa mahakamani Magu, Agosti 19, mwaka huu kwa ajili ya mwenendo wake.