Mkutano wa tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulihitimishwa Novemba 9, mwaka huu, mjini Dodoma, ukiwa umetikiswa zaidi na hoja binafsi za wabunge; Kabwe Zitto, Halima Mdee na hukumu ya Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), aliwasilisha hoja yake binafsi ya kuitaka serikali ichukue hatua za kisheria dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Tanzania. Hoja hiyo iliridhiwa na Bunge.
Naye Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema), aliwasilisha hoja yake binafsi ya kuitaka serikali isitishe ugawaji wa ardhi hadi tathmini ya kina itakapofanyika kujua kiasi cha ardhi kinachomilikiwa na wawekezaji.
Sambamba na hilo, Mdee anataka tathmini ya kina ifanyike kubaini wageni na wazawa waliojipatia ardhi kinyemela kupitia serikali za vijiji kinyume cha Sheria ya Ardhi Namba 5 ya mwaka 1999.
Kwa upande wake, Spika Makinda, ambaye ni Mbunge wa Njombe Kusini (CCM), aliwasilisha taarifa ya uamuzi wake kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za kibunge.
Hoja ya Zitto
Katika hoja yake binafsi ambayo nusura ipunguzwe makali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Zitto ameendelea kuwatuhumu baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali na kutaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya Tanzania.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, anadai kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wamo walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu kati ya mwaka 2003 na 2010, uwaziri na makatibu wakuu wa Nishati na Madini katika kipindi hicho.
Anasema wengine ni waliowahi kuwa mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa serikali, makamishna wa Nishati, wakurugenzi wakuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wenyeviti na wajumbe wa Bodi wa TPDC. Anataka serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kuwezesha mabilioni ya fedha na mali nyingine zilizotoroshwa kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na kwingineko zirejeshwe zitumike kuwapunguzia Watanzania ugumu wa maisha.
Lakini pia, anataka watuhumiwa hao wabanwe waeleze walipataje mabilioni hayo ya fedha na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini iwachunguze na kuwashughulikia kisheria waliojilimbikizia kwa njia haramu.
Zitto anasema Benki Kuu ya Uswisi imetangaza kuwa dola za Marekani milioni 196 zilikuwa zimehifadhiwa katika benki za nchi hiyo. Hata hivyo, mbunge huyo anadai kuwa fedha zinazomilikiwa na Watanzania nchini humo ni zaidi ya mara 20 ya kiasi hicho.
Baada ya mjadala mkubwa uliowahusisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wabunge kadhaa, Spika wa Bunge alisema hoja hiyo ya Zitto inaingia kwenye utaratibu wa kutekeleza maazimio yaliyofikiwa bungeni na kwamba serikali itapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa hoja hiyo katika Bunge la 11 la Aprili 2013 na kama ikishindwa, Bunge litaunda kamati ya uchunguzi.
Zitto ameeleza kuridhishwa na uamuzi huo wa Bunge, akisema hiyo ni mara yake ya kwanza kwa hoja yake binafsi kupitishwa na Bunge tangu awe mbunge.
Hoja ya Mdee
“Kwa mujibu wa Kanuni Namba 54 (1), (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, naomba kutoa hoja binafsi ya kuitaka serikali kusitisha ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje mpaka hapo tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiwango gani cha ardhi kiko mikononi mwa wawekezaji,” alisema Mdee.
Mbunge huyo anaonesha hofu kwamba ardhi ya Tanzania inaweza kuishia mikononi mwa wawekezaji wachache matajiri na wananchi kuachwa wakiwa masikini, ikiwa serikali haitaikubali na kuifanyia kazi hoja yake hiyo.
Anahofia kuwapo kwa wimbi la wageni wanaokaribishwa kuwekeza kwenye kilimo kwa maelezo kwamba watasaidia kuinua uzalishaji katika sekta hiyo, ingawa mara kadhaa uwekezaji huo umegeuka kuwa shubiri kwa wananchi, hususan wakulima wadogo.
Anasema ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji usiofuata taratibu, umeendelea kusababisha migogoro ya ardhi katika maeneo mengi na kuongeza umaskini usiyo wa lazima miongoni mwa wazawa.
Hoja hiyo ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa mawaziri na wabunge. Mawaziri waliochangia ni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alikazia msimamo wa mawaziri na wabunge waliopinga kipengele cha kusitisha ugawaji ardhi kupisha thathmini ya kubaini kiasi cha ardhi kinachomilikiwa na wawekezaji.
Hatimaye hoja hiyo ya Mdee iliungwa mkono na wengi, hivyo kupitishwa na Bunge chini ya Spika Makinda, ambapo utekelezaji wake utafanyika bila kusitisha ugawaji wa ardhi.
Uamuzi wa Spika
Spika Makinda, alisoma bungeni taarifa ya uamuzi wake kutokana na ripoti ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliyochunguza na kumshauri Spika kuhusu wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini waliotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi (CCM), iliwasafisha wabunge waliotuhumiwa ikisema tuhuma zilizotolewa dhidi yao ni za uongo.
Katika uamuzi wake, Spika ametoa onyo kali kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na wabunge waliotoa tuhuma hizo, akiwataka kutorudia uongo.
Mbali ya Profesa Muhongo na Maswi, Spika Makinda ametoa onyo kali kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na wabunge wengine waliounga mkono tuhuma hizo akiwataka kutorudia kosa la kuzungumzia bungeni jambo wasilokuwa na uhakika nalo.
Spika amesema viongozi hao wamelifedhehesha na kulidhalilisha Bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo na kuuaminisha umma wa Watanzania kwamba baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
Miongoni mwa tuhuma zilizotolewa ni pamoja na iliyotolewa na Maswi kwamba baadhi ya wabunge wa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walikwenda ofisini kwake kuomba rushwa watetee taarifa mbalimbali za wizara hiyo.
Waliotuhumiwa na Maswi ni Mbunge wa Viti Maalumu, Sarah Msafiri (CCM), aliyedaiwa kumwomba rushwa ya Sh milioni 50 azigawe kwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Zedi, alituhumiwa kuomba rushwa ya kuwagawia wajumbe wa kamati yake Sh milioni mbili kwa kila mmoja wasiendelee kulalamikia utendaji wa Maswi.
Inaelezwa Maswi aliwatuhumu pia wabunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe na Sarah Msafiri na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), kwamba walimtishia lazima aachie madaraka kutokana na utendaji wake usioridhisha katika wizara hiyo.
Baada ya uamuzi wake huo, Spika Makinda amesema ameivunja moja kwa moja Kamati ya Nishati na Madini bila kujali imesafishwa na kuahidi kuunda mpya katika Bunge lijalo.
Hata hivyo, kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ameelezea kutoridhishwa na uamuzi huo wa Spika Makinda, hivyo ameahidi kukata rufaa.
“Sijakubaliana na uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge na hatima ya Kamati ya Nishati na Madini. Nitakata rufaa. Ripoti yote ya Ngwilizi inapaswa iwekwe hadharani,” alisema.