Wakati Rais John Pombe Magufuli ameingilia kati mgogoro wa umiliki wa ardhi kwa mjane kutoka Tanga, Swabaha Mohamed Shosi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa jijini Dar es Salaam watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wamepandikiza hati juu ya hati ya kiwanja na kuzua mgogoro mkubwa na upotevu wa kodi.
JAMHURI kwa muda sasa limekuwa likifuatilia habari hii ya kiuchunguzi, ambapo Serikali inapoteza zaidi ya Sh bilioni 3 hadi 4 kwa mwezi kama kodi, kutokana na kampuni iliyopangishwa kwenye jengo kihalali kuondolewa na madalali na kuharibu vitu vyake.
“Mgogoro huu unasikitisha. Polisi kwa bahati mbaya waliingia katika mgogoro huu bila kufahamu. Wameingizwa mkenge nao wakaamini ndiyo ukweli, hadi wakatuma FFU kufanya kazi haramu ya kuwaondoa wapangaji kwenye jengo ambalo anayedai kulimiliki sasa dalali alimuuzia kimakosa.
“Nimeamua kujitokeza kuwaambia ukweli, ila naomba msinitaje maana hawa jamaa wana nguvu kubwa huko mahakamani na sehemu nyingine wanaweza kunipoteza au wakanifungulia kesi isiyoisha milele nikahangaika. Nimekuwa nasoma mnavyoandika suala hili nimeona heri niwasaidie na kuisaidia jamii kwa kuieleza ukweli,” amesema mtoa habari wetu.
Mtu huyo aliyesema yeye alikuwa mmoja wa wafanyakazi waliochangia mgogoro huu mwaka 1998, amefungua kabrasha la ukweli kwa kusema: “Uhalisia, uko hivi. Kuna mfanyabiashara anaitwa Hasham Kassam. Huyu aliipangisha Kampuni moja inayoitwa H. K. Foam kwenye jengo lake. Kampuni hii ilishindwa kulipa mishahara na stahili za wafanyakazi tukaipeleka mahakamani Kisutu.
“Shauri letu lilikuwa la madai Na 298 la mwaka 1998. Tuliongozwa na ndugu Sililly Lushinga na wafanyakazi wenzake 23. Kesi hiyo iliendelea hadi mwaka 2007 tuliposhinda. Mwezi Machi mwaka huo, Mahakama ilitupatia Warrant of Attachment (hati ya kukamata na kuuza mali). Hapo ndipo shida ilipoanzia.
“Mahakama iliagiza zikamatwe mali zinazohamishika kutoka katika hiyo ofisi kwa kuwa H. K. Foam alikuwa mpangaji na hakuwa mmiliki wa hicho kiwanja ni mali ya Hasham Kassam aliyekuwa amempangisha. Deni letu kwa wakati huo lilikuwa Sh 1,189,757,343.
“Aprili 25, 2007, Hakimu Mkazi Mwandamizi, jina lake limenitoka kidogo, ila saini yake ipo kwenye hii hati aliyotupa, alituruhusu kwenda kuuza mali zinazohamishika za H. K. Foam. Tulipoipeleka kwa dalali, dalali akabadili mchezo. Akatangaza kuuza jengo na kiwanja kama unavyoona hili tangazo lake.
“Tena mwenye kiwanja na jengo, hakuwa na taarifa hadi watu wa benki alikokuwa amechukua mkopo walipompigia simu na kumhoji inakuwaje anauza kiwanja na jengo alilochukulia mkopo, ndipo akashtuka na kukimbia mahakamani kuweka zuio.
“Huko mahakamani alikuta watu wameishajipanga, wala hakufanikiwa. Amefungua kesi nyingi hazina idadi tangu mwaka 2007, hadi leo zinatupwa kutokana na zuio la awali (preliminary objection) au anaambiwa amekosea kuorodhesha namba na mambo mengi ya hivyo.
“Mtu aliyenunua kiwanja na jengo lililokuwamo namfahamu kwa jina la Osama (Mohamed Suleiman Mohamed) ambaye ni mfanyabiashara mkubwa hapa Dar es Salaam, na alilinunua kwa jina la Educational Book Publishers. Hapo ndipo mchezo umeendelea huko mahakamani hadi leo Kassam sidhani kama atapata kitu.
“Kilichofuata, nadhani Juni mwaka jana, Osama alituma mabaunsa wakaenda kumwondoa mpangaji wa Kassam kwa nguvu ofisini. Mpangaji huyu – Kampuni ya Petrofuel – ndiye unayekuwa ukiandika kuwa wakati anafanya biashara alikuwa analipa kati ya Sh bilioni 3 hadi 4 kwa mwezi kama kodi serikalini,” amesema mtoa habari wetu.
JAMHURI limewasiliana na mmoja wa watu walioko karibu na Osama kujiridhisha iwapo habari hiyo ni ya kweli, na mtu huyo akasema: “Osama hana makosa hata kidogo. Mchezo ulichezwa na Dalali wa Mahakama, ambaye ni Mamba Auction Mart.
“Dalali aliambiwa auze mali zinazohamishika, yeye akauza hadi jengo na kiwanja. Bahati mbaya sheria inasema mtu akinunua mnadani mali kihalali, na akalipa kiasi chote anachodaiwa, basi huwezi kumnyang’anya tena mali hiyo hata kama kulikuwapo na dosari. Kosa alilifanya dalali, na Osama alinunua kihalali kwa mujibu wa tangazo la dalali.
“Ninachofahamu baada ya kubaini kuwa kiwanja kina makandokando, Osama anajua alifanyaje, lakini alikimbia akabadilisha hati haraka sana. Wizara ilimpatia hati kupitia Halmashauri ya Manispaa Temeke, na sasa anaendelea kukilipia kodi zote.
“Ndiyo maana ilipofika Juni 24, 2016 akaona kwa miaka 9 tangu amenunua kiwanja na jengo kwenye mnada, bado Kassam ameendelea kupokea kodi kutoka kwa wapangaji kama Petrofuel naye hafaidiki kitu. Ndipo akatafuta madalali wakaondoa huyo mpangaji. Hata hayo mafuta lita zaidi ya 280,000 hajamzuia Petrofuel kuyatoa, hata akitaka kesho anayatoa,” amesema mtoa taarifa wa upande wa Osama.
JAMHURI limefanya juhudi za kumtafuta Kassam ambaye alisema: “Mpaka sasa nipo kwenye mshangao. Najiuliza inawezekanaje mpangaji wako akatenda makosa ukauziwa nyumba yako.
“Ni sawa na kusema ninyi mlipopanga hapo JAMHURI katika Jengo la Matasalamat Mansion, mkishindwa kulipa wafanyakazi wenu, wakienda mahakamani na Mahakama ikaruhusu mali zenu ziuzwe, basi jengo la National Housing Corporation (NHC) mnakopanga linauzwa eti kwa sababu JAMHURI wafanyakazi wanaidai.
“H. K. Foam alikuwa mpangaji wangu, hakuwa mmiliki wa kiwanja na jengo. Haikubaliki hii. Nimeomba msaada mahakamani sifanikiwi, ila bado naendelea kupambana. Nimeomba msaada Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu ameingilia suala hili, ila Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sirro, anaonesha kuwa na upande maana ametamka kuwa kiwanja hiki ni mali ya Educational Book Publishers, wakati akijua si kweli.
“Nazidi kuomba msaada Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, anisaidie. Kamishna wa Ardhi anisaidie, na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais John Pombe Magufuli, naomba anisaidie. Nimefanyiwa uhuni wa hali ya juu. Hadi leo bado ninayo hati halisi, na hiyo hati waliyonayo ni feki. Naendelea kuilipia kodi zote, sijui wao hiyo waliyonayo wanailipia wapi kodi na kwa namba ipi ya kiwanja. Naomba jamii inisaidie naumizwa kwa kosa ambalo si langu jamani,”amesema Kassam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Educational Book Publishers, maarufu kama Osama, JAMHURI lilipowasiliana naye amesema kwa ufupi: “Mtafute wakili wangu ndiye azungumze.”
Wakili wa Educational Book Publishers, Wilson Ogunde, alipoulizwa, amesema mteja wake ni mmiliki halali wa kiwanja hicho Na 12B, E. Plot 20 kilichopo Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam na alifuata taratibu zote kukipata, ila aliyekuwa mpangaji katika kiwanja hicho, Kampuni ya Petrofuel, ndiye amegoma kuondoa mafuta aliyoyaacha baada ya kuondolewa kihalali.
JAMHURI limemtafuta Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, aliyesema suala hilo limekwisha siku nyigi na analishangaa gazeti hili kuliamsha.