Aliyosema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko
Kama ilivyobainishwa katika Ajenda ya Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), leo Dar es Salaam inayo heshima ya kuwa mwenyeji wa wajumbe kutoka Afrika na kwingineko, wakihudhuria Mkutano huu muhimu unaolenga kuimarisha azma ya Afrika ya kuipatia bara hili nishati.
Baada ya kupata Uhuru mwaka 1960, nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao. Tanzania ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 21 pekee wakati wa Uhuru, kwa sasa nchi ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,160.
Pamoja na mafanikio makubwa ya kuzalisha umeme barani Afrika, takriban Waafrika milioni 571 bado hawana huduma ya umeme. Mkutano huu umeitishwa rasmi kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Natoa shukrani za dhati kwa waandaaji wenza wa Mkutano huu ikiwemo: Benki ya Dunia; Benki ya Maendeleo ya Afrika; Rockefeller Foundation; Sustainable Energy for All (SEforALL), na The Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP) kwa ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa Mkutano huu.
Uwepo wenu, mawazo na utaalamu wenu ndiyo vitakavyofanikisha Mkutano huu. Natarajia majadiliano yenye tija na tushirikiane katika kuunda mustakabali wa nishati barani Afrika.
Natarajia mkutano huu utakuwa ni hatua muhimu katika kufanikisha lengo letu la upatikanaji wa umeme kwa wote.
Katika mkutano huu, Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia, watapata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza Mpango wa Mission 300.
Maazimio ya Nishati ya Kitaifa yaliyotayarishwa na nchi 14 zitakazokuwa za majaribio yatatoa mfumo wa utekelezaji wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji zaidi kutoka kwa serikali, wabia wa maendeleo, mashirika ya misaada na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya upatikanaji wa nishati.
Kupitia uhamasishaji wa rasilimali na utaalamu katika kuharakisha juhudi za kupeleka umeme barani Afrika, Mission 300 itaonyesha dhamira yetu ya pamoja katika kufanikisha upatikanaji wa nishati safi kwa wote, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuboresha maisha ya watu.
Tanzania inachukulia mkutano huu kama kichocheo cha utekelezaji wa Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu, uhifadhi na ufanisi. Sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika mchanganyiko wa uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa nishati.
Ifikapo mwisho wa mwaka 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000. Nishati yetu inatoka kwenye vyanzo safi na mbadala vinavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, huku miundombinu ya umeme ikifikia vijiji vyote 12,318 nchini.
Vile vile, Tanzania inamarisha muunganiko wa Afrika kwani ina miundombinu ya umeme inayounganisha nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, na Uganda, huku miundombinu ya kuunganisha Zambia ikiwa inaendelea.
Pamoja na maendeleo ya nishati tunayojivunia, bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati. Tuna matarajio ya kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda, madini, na huduma za ukarimu jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati.
Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika. Jitihada hizi zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na yamejumuishwa katika Azimio litakalotiwa saini, huku tukitoa wito wa ahadi na ushirikiano zaidi katika kuboresha upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani mwetu.
Miongoni mwa mambo mengine yatakayofanyika katika mkutano huu, tutashirikiana uzoefu; kupata ahadi muhimu za kisiasa; kutumia ushirikiano ili kufungua uwekezaji wa sekta binafsi; kuanzisha ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati; na kukubaliana mfumo wa ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kiashiria cha Ufuatiliaji wa Maazimio ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano huu.
Ni matarajio yangu kwamba, mamlaka zinazohusika za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati mbadala na mchango wa mtaji wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji wa nishati.
Sasa ni wakati wa kufungua uwezo wa nishati wa bara la Afrika na kukabiliana na pengo la nishati. Tuitumie fursa ya Mkutano huu kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio yetu ya nishati na kuimarisha ushirikiano unaohitajika kuyatekeleza.
Aliyosema Rais wa Benki ya Dunia (WB), Bw. Ajay Banga
Tunaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030
*Aliyosema Rais wa Benki ya Maendele ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina .
Tanzania imekua mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
Nawahakikishia kuwa lengo la kuwafikishia umeme watu milioni 300 Afrika linakwenda kufanikiwa, tunahitaji uwazi na uwajibikaji katika kufikisha lengo hili.
Mkutano huu unalengo la kuifungua Afrika kwenye eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika za Afrika wanaunganishwa na umeme.
Aliyosema Waziri wa Fedha na Mipango, Zambia, Mhe. Dkt. Situmbeko Musokotwane.
Nawashukuru ndugu zetu Watanzania kwa kuiuzia umeme Zambia kwa sababu tunakabiliwa na upungufu wa nishati ya umeme.
IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI – MAELEZO