Miongoni mwa mambo niliyoshindwa kuyaamini wakati wa vikao vya Kamati za Bunge vilivyofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita, ni matumizi ya fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuhusu bei ya mayai.
Katika taarifa yake iliyokataliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), halmashauri hiyo inaonyesha kwamba imekuwa ikinunua yai moja la kuku kwa Sh 900 kutoka kwa wazabuni, jambo ambalo hata kwa akili za kiwendawazimu haliwezi kukubalika.
Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Idd Azan, pamoja na wajumbe wake walishangaa. Akawataka viongozi wa halmashauri hiyo angalau kuitaja kwa mdomo bei ya yai moja huko Tunduru ambapo walisema kwa pamoja ni Sh 500.
“Bei ya yai kwenye hesabu hizi mnaonyesha ni Sh 900, lakini hapa mnasema ni Sh 500. Huu ni uzembe au ufisadi?” Alihoji Azan, ambaye ni Mbunge wa Kinondoni, Dar es Salaam.
Mbali na bei ya yai, kamati hiyo pia ilikataa kupokea ripoti ya matumizi ya fedha za miradi mbalimbali zilizoonyeshwa kwenye vitabu vilivyowasilishwa kwao na halmashauri hiyo.
Zikiwa zimetumika bila mchanganuo kuonyeshwa kama inavyotakiwa, Azan alisema mbali na uzembe huo, inawezekana kuwa matumizi ya fedha hizo pia yameongezwa kama ilivyo kwenye bajeti ya ununuzi wa mayai na kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI) kumuonya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ephraim Ole.
Hicho ndicho nilichoshindwa kukiamini endapo kinaweza kikafanywa na watendaji wa serikali waliopewa mamlaka ya kukusanya, kupokea, kugawa na kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kila senti inayotolewa au kupatikana ifike na kutumika vizuri.
Nimezuru Tanzania kuanzia mijini hadi vijijini. Baadhi ya mikoa nimekwenda mara nyingi. Nimekula nyumbani, hotelini hadi kwenye vibanda vya kina mama ntilie na hata kwa wakaanga chips mitaani, lakini hakuna popote nilipoikuta bei ya yai moja likiuzwa kwa Sh 900!
Mbali na hivyo, mimi mwenyewe ni mjasiriamali ambaye pamoja na biashara nyingine za kunisukumia maisha yangu ya kila siku, nafuga kuku wa mayai.
Najua, kwa mfano, kwamba Dar es Salaam ambako bei ya vitu vingi yakiwamo mayai iko juu. Uongo uliowasilishwa na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa LAAC unaonyesha wizi unaofanyika kijinga na bila aibu.
Trei moja inayobeba mayai 32 Dar es Salaam ambako ndiko kwenye bei kubwa inauzwa Sh 6,500 ambayo ni sawa na wastani wa Sh 203.125 kwa kila yai moja. Rejareja madukani ni kati ya Sh 250-300.
Ni ujasiri wa kishetani kukosa hadi woga kwa Kamati ya Bunge kuwa yai moja linauzwa kwa Sh 900 na kibaya kupindukia, bei hiyo inaletwa kutoka kwenye mji mdogo kabisa wa Tunduru.
Pamoja na hayo, idadi ya wakazi wote wa mji huo pia ni ndogo ikilinganishwa na wale wanaoishi katika vitongoji vyha majiji kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na kadhalika. Kutokana na ukweli huo, bei ya vyakula nayo ambayo ni pamoja na yai kamwe haiwezi kuwa Sh 900.
Tofauti na ilivyokuwa hapo zamani, watendaji wa serikali hivi leo wanaiba wanavyoweza kwa sababu hawachukuliwi hatua kali za kisheria zinazoweza kuwatisha.
Wanapata taarifa kutoka kila kona ya nchi kupitia vyombo vya habari kwa mfano kuwa Halmashauri ya Wilaya, Mji au Manispaa fulani imepoteza mamilioni na hata mabilioni ya fedha za umma kupitia miradi ya serikali, posho za watumishi au kwa kuwalipa mishahara wafanyakazi hewa, lakini hakuna adhabu ya maana wanayopewa.
Inatangazwa kuwa pamoja na kuiba fedha hizo zote, watendaji hao wa umma wanaadhibiwa kwa kuhamishiwa vituo vingine vya kazi na kuendelea na nyadhifa zilezile, mishahara ileile, marupurupu yaleyale na pia haki zote zikibaki palepale kama zilivyo; huku serikali ikifidia hasara yote iliyopatikana!
Mathalani, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini anayekabiliwa na kesi mbili za jinai – moja ya kuhujumu uchumi na nyingine ikiwa ya kuitia hasara ya fedha nyingi serikali – amehamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe huku akiwa na wadhifa ule ule!
Kinachochefua zaidi ni kuona mkurugenzi huyo huyo anakwenda Ujerumani ili kuiwakilisha halmashauri katika shughuli za kikazi, licha ya kuitia hasara kubwa na kuhamishiwa kituo kingine; jambo ambalo limemkera hata Mwenyekiti wa LAAC, Augustine Mrema.
Wanajua namna mamilioni ya fedha za serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo yalivyotafunwa na watendaji wake, kisha wakasimamishwa na kufunguliwa mashitaka ya jinai mahakamani, lakini wanaendelea kutamba kwa mishahara.
Kama mfanyakazi anasimamishwa kazi na kuendelea kulipwa mshahara wake wote, akabaki kwenye nyumba inayomilikiwa au kulipiwa na mwajiri wake hata kama itakuwa hivyo kwa miaka 20 hawezi kulalamika au kunung’unika kwa namna yoyote.
Atafurahia kwa sababu atakuwa amepata muda kwa kutosha wa kufanya kazi zake ikiwamo kufungua miradi ya biashara na kuisimamia yeye mwenyewe, ikamwingizia fedha nyingi kwa mtaji wa mamilioni aliyojichotea, lakini akaendelea kulipwa mshahara, akabaki kwenye nyumba inayomilikiwa au kulipiwa kodi ya pango na mwajiri.ama alivyosema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipohutubia maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, wiki iliyopita, serikali sasa ingeanzisha utaratibu maalumu kwa ajili ya kesi za watumishi na watendaji wanaotuhumiwa kutumia vibaya ofisi zote za umma iwe kwa kuiba au vinginevyo.
Ushauri huo ni muhimu zaidi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa vile ndiyo inayosimamia utendaji wa shughuli zote za kila siku za serikali, halafu inabidi utekelezaji wake nao uanze hima.
Mbali na uozo mwingine, matumizi mabaya ya madaraka, ukiwamo wizi wa fedha za umma kama unaofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ubadhirifu unaoitafuna miradi ya serikali ni mkubwa zaidi kwa Tamisemi. Katika hali hiyo na hata vinginevyo, kama wezi hao bado hawatafungwa jela, tena kwa kesi ambazo zitaendeshwa kwa muda usiozidi angalau miezi 12 hivi, kisha wakafilisiwa mali zao zote zilizopatikana kinyume cha sheria, hakika wizi hautakoma.
Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0762 633 244