Na Nizar K Visram
Mahakama ya Marekani imeamuru kuwa jengo lenye thamani ya dola milioni 3.5 lililo karibu na Washington lichukuliwe kutoka kwa Yahya Jammeh, aliyekuwa Rais wa Gambia.
Uamuzi huu wa Mei 24, mwaka huu ni baada ya kudhihirika kuwa fedha zilizotumika kununulia jengo hilo la anasa zimetokana na rushwa na wizi wa mali ya umma.
Hivyo mahakama imeamuru liuzwe na fedha zitumike kufidia wananchi wa Gambia walioathirika kwa utawala wa Jammeh.
Jengo limesajiliwa kwa jina la Zainab Jammeh, mke wa Yahya Jammeh. Lina vyumba vya kulala saba, kila kimoja na bafu lake, ukumbi wa sinema, bwawa la kuogelea, chumba cha mazoezi na nyumba ya wageni. Jammeh alikuwa akitembelea Marekani na kukaa hapo na mkewe.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Kenneth Polite, Jr amesema serikali yake imeamua kudhibiti mali zilizopatikana kwa njia zisizo halali katika nchi za kigeni.
“Kesi hii inaonyesha jinsi tunavyoweza kufichua mali haramu zilizopo Marekani,” amesema na kuongeza kuwa wakuu wa nchi za kigeni hawataweza kuficha mali zao haramu Marekani: “Tutatumia kila mbinu kufichua mali hizo na kuzirudisha zilikotoka.”
Hata hivyo, Polite hakueleza ilikuwaje wasubiri mpaka Jammeh apokonywe urais na wananchi wa Gambia ndipo wapitishe hukumu hiyo. Kwani alipokuwa madarakani hawakujua kuwa jengo hilo lilipatikana kwa njia zisizo halali?
Na wakati wote huo walikuwa wakimkaribisha Jammeh White House na kumkirimu ilhali wakijua fika alivyokuwa akitawala Gambia.
Walijua kwa sababu tangu mwaka 2010 wananchi wa Gambia waishio Marekani walitangaza kuwa Jammeh amenunua jengo eneo la Potomac karibu na Washington na kuunda umoja wao (Democratic Union of Gambian Activists – DUGA).
Utafiti wao uligundua kuwa jengo la kifahari lilinunuliwa na mtu aliyejitambulisha kama MYJ; ufupisho wa jina Yahya Jammeh.
DUGA wakaanza kuandamana nje ya jengo husika. Wakapandisha bendera ya Gambia mlangoni na wakasambaza vipeperushi. Polisi wakaja na kuwafukuza.
Wakati mmoja Jemmeh alipokuwa Marekani, DUGA waliandamana nje ya hoteli alipofikia. Walinzi na wapambe wake wakawashambulia na mmoja ikalazimika kupelekwa hospitali.
Marekani wakampa Jammeh ‘msaada’ wa dola milioni 1.2 wakati wanaharakati wakitaka Marekani izuie misaada na imzuie yeye na mkewe kutembelea Marekani.
Walitaka pia Marekani itaifishe mali zake. Hata hivyo, Marekani haikuchukua hatua mpaka Jammeh alipotimuliwa na wananchi.
Kabla ya hapo, Marekani walikuwa na uhusiano mzuri na Jammeh. Mwaka 2014 Jammeh na mkewe walikaribishwa White House na Rais Barrack Obama. Aliporudi Gambia akapokewa na wafuasi wake wakiwa wamevalia fulana zenye picha ya Obama akisalimiana na Jammeh.
Na haikuwa Jammeh peke yake! Madikteta wengine waliowahi kukaribishwa Marekani ni Rafael Trujillo wa Dominican Republic, Ferdinand Marcos wa Philippines, Muhammad Zia-ul-Haq wa Pakistan, na Augusto Pinochet wa Chile.
Karibu na jengo la Jammeh jijini Washington kulikuwa na jengo jingine lililomilikiwa na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Equatorial Guinea, tangu mwaka 1979. Yeye pia anatuhumiwa kuwa amekusanya mali kwa njia sisizo halali.
Haikuwa ajabu kwa Jammeh kukimbilia Equitorial Guinea kama mgeni wa Obiang baada ya kutimuliwa Gambia.
Jammeh alitumia mbinu mbalimbali kujikusanyia mali. Moja ni kuchukua hisa katika kila kampuni; kuanzia bekari za mikate hadi uchimbaji wa mchanga.
Kila aliyetaka leseni alipaswa kumpatia hisa au gawio. Njia nyingine ni kutoza kamisheni katika kila kibali cha biashara alichotoa. Pia alijichotea fedha kutoka mfuko wa serikali na kuzihamishia kwenye akaunti zake.
Kwa mfano, Julai 2010, kampuni ya kuagiza petroli iliambiwa kuwa mwishoni mwa mwaka leseni yake ingemalizika. Mmiliki akaonana na Jammeh.
Mara moja dola milioni moja zilihamishwa kutoka akaunti ya kampuni na kuingia akaunti ya MYJ nchini Marekani. Siku hiyo hiyo Jammeh akahuisha leseni na baada ya siku chache dola milioni 2.5 zikaingizwa tena katika akaunti ya MYJ. Hapo ndipo jengo la Potomac (Maryland) likanunulkiwa na MYJ kwa dola milioni 3.5.
Shirika la Kimataifa la Kupambana na Rushwa (OCCRP) lilifichua jinsi Jammeh na wenzake walivyopora takriban dola bilioni moja kutoka mfuko wa serikali. Shirika hilo lilifanikiwa kupata maelfu ya nyaraka, zikiwamo barua za serikali, mikataba, akaunti za benki na hati miliki. Zote hizi zinaonyesha jinsi Jammeh alivyokuwa akipora mali za umma.
Jammeh hakusamehe hata akiba ya wafanyakazi. Alichukua dola milioni 60 kutoka mfuko wa pensheni. Katika uwanja wa diplomasia alitumia uhasimu baina ya China na Taiwan na akajipatia zaidi ya dola milioni 100.
Huyu ndiye aliyekuwa Rais wa Gambia ambaye alipenda kuitwa Mheshimiwa Sheikh Profesa Alhaji Dk. Yahya Abdul-Aziz Awal Jemus Junkung Jammeh Naasiru Deen Babili Mansa.
Alijiita profesa kwa sababu alidai amevumbua dawa ya kuponya ukimwi ambayo alisema inafanya kazi siku ya Jumatatu na Alhamisi tu.
Mwaka 1999 Jammeh alitunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Saint Mary, Canada. Ni kwa sababu aliwapa raia wa Gambia; ‘uhuru wa kuishi maisha bora yenye amani na maelewano’.
Shahada nyingine za udaktari alizipata kutoka Chuo cha Saint Mary (Marekani), Chuo Kikuu cha Costa Rica na cha Taipei.
Alidai kuwa alitunukiwa shadada za PhD pia kutoka Urusi na Ujerumani. Akadai kuwa alipokea barua kutoka kwa Rais Obama; ikagunduliwa kuwa ni feki.
Jammeh alianza kutawala Gambia mwaka 1994 baada ya kumpindua kijeshi Rais Sir Dawda Jawara aliyechaguliwa na wananchi. Wakati huo Jammeh alikuwa luteni mwenye umri wa miaka 29, akiwa amepata mafunzo ya miezi minne katika chuo cha polisi Marekani.
Kwa mujibu wa asasi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu (HRW), Jammeh aliunda kikosi cha wafuasi wake (junglers). Kazi yao ilikuwa kuwakamata wapinzani wake, kuwaua na kuwatupa kisimani.
Mmojawapo ni Deyda Hydara, mhariri wa gazeti huru (The Point) ambaye aliuawa kwa risasi mwaka 2004 alipokuwa akielekea nyumbani kutoka ofisini.
Mwaka 2016 ulifanyika uchaguzi na Adama Barrow akatangazwa kuwa mshindi. Jammeh akakataa kumuachia kiti. Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ilituma ujumbe kumshauri, lakini aling’ang’ania.
Ndipo ECOWAS ikatuma majeshi kumuondoa kama ilivyofanyika Zimbabwe. Jammeh akaona maji yamemfika shingoni, akachukua ndege na kukimbilia Equatorial Guinea anakoishi uhamishoni.
Hata wakati wa kukimbia, aliamua asiondoke mikono mitupu. Akaondoka na magari 13 ya kifahari kama Rolls-Royce, Benz na Bentley.
Hakuweza kuyapakia yote katika ndege, hivyo akapakia mawili na yaliyobaki akaagiza yamfuate. Inasemekana aliondoka na dola milioni 11, hivyo kuacha mfuko wa serikali ukiwa mtupu.
Baada ya Jammeh kutoroka, serikali ya Barrow ikaunda tume ya ukweli, maridhiano na fidia. Ripoti iliyotoka mwaka 2019 imeshauri kuwa Jammeh afikishwe mahakamani akajibu ‘shutuma za jinai’ na ubakaji, mauaji na utesaji. Tume ilitoa mapendekezo 265 na serikali ikayakubali yoye isipokuwa mawili tu.
Tume imedhihirisha kuwa Jammeh alikusanya majengo 281 nchini Gambia, Marekani na Morocco. Pia alikuwa na akaunti zaidi ya 100 katika benki tofauti duniani. Nyumbani kwake ilikutwa bastola ya dhahabu. Kwa ujumla tume imegundua kuwa alipora zaidi ya dola milioni 300 zilizokusudiwa kuwasaidia watoto yatima, wanafunzi na wananchi wasiojiweza.
Tume pia iliorodhesha fedha alizopata kwa njia ya rushwa kutoka kwa wawekezaji na wafanyabiashara ambao aliwapatia vibali na leseni. Miamala takriban 10,000 ilichunguzwa kuona jinsi fedha za umma kutoka Gambia zilivyotoroshwa nje ya nchi.
Habari za hivi karibuni zinasema Serikali ya Gambia imeamua kumfungulia mashtaka Jammeh pamoja na wasaidizi wake 70 waliotajwa katika ripoti ya tume.
Ni pamoja na aliyekuwa makamu wake, Isatou Njie-Saidy na ‘Junglers’ waliotumika katika mauaji.
Hata hivyo, tatizo ni jinsi ya kumrudisha kutoka Equatorial Guinea. Nchi hiyo haina mkataba na Gambia utakaowezesha Jammeh kukamatwa na kurudishwa Gambia.
+1 343 204 8996