Siamini kama mtu ambaye anayemwamini Mwenyezi Mungu anaweza kuamua, kwa mkono wake, kukatisha maisha ya mtumishi wa bwana kwa moyo safi na wa kijasiri. Haya naona ni maendeleo mengine ambayo enzi zetu hayakuwako, sielewi kama napaswa kuwapongeza au kuwalaumu kwa maendeleo hayo.
Mmefanya maendeleo mengi, mmegeuza kilimo kuwa udalali kila mwenye nguvu haendi shamba anangoja mazao yafike sokoni aweke cha juu ili maisha yaendelee, mkulima ameendelea kuwa yuleyule ambaye sasa nguvu zinamwishia na anapunguza mazao anayoleta sokoni.
Haya ndiyo maendeleo yenu, mmewauzia viwanda na mashamba hao wanaoitwa wawekezaji nanyi mmegeuka kuwa vibarua ndani ya viwanda vyenu na sasa mnalalamika kuwa mnanyanyaswa na hao wawekezaji, mnapiga kelele ambazo hazisikiki kwa watwana mliowachagua kuwa viongozi wenu. Hayo ndiyo maendeleo.
Ni kweli ni maendeleo kwa sababu sasa kila kitu ni digitali, hata elimu mnataka iwe digitali kwa sababu kama huna king’amuzi hayo ‘material’ utayapataje? Mtoto wa Ole, Kitope, Zuzu, Balile, Manyerere wanaosoma shule zile za kule kusiko na dishi watayatoa wapi hayo material?
Maendeleo kwa vile sasa hata ufaulu ni ujinga, bora kuwa bwege kwa kuwa hata usome vipi ni kazi bure utafanya nini katika Taifa hili ambalo kila siku ni bora ya jana kulikucha na makucha yake ya nafuu ya jana yake.
Ni maendeleo kwa kuwa tunafuga vijana wajinga wasio na kazi, watoto wasiopata elimu kwa maendeleo ya kesho, majambazi ambayo hayatosheki kila siku, makundi ya kisiasa ambayo yanasigana, makundi ya dini yasiyo na mwelekeo wa upendo katika jamii, watetezi wa haki za raia wanaokinzana na sheria zilizomo katika Katiba yetu ya nchi.
Ndiyo maendeleo ambayo nayaona kwa sasa, kwamba kile tulichokubaliana kuwa ni kweli leo tunakiita ni uongo kwa kauli moja ya wote huku tukiamini kuwa si kweli, tunapingana na sera zetu nzuri ambazo tulijiwekea tangu tunaasisi Taifa hili kwamba tutafuta ujinga, maradhi na umaskini.
Tulisema viongozi bora ndiyo misingi yetu na si bora viongozi, leo tunapinga hilo bora viongozi hawataki kutoka madarakani kwa sababu hawautaki umaskini kwa kutumia ujinga wetu, tunavishwa magwanda ya kutusitiri ujinga wetu nasi tunafurahia.
Haya ndiyo maendeleo kwa Taifa lililochagua njia ya kupita kuelekea karne ya sayansi na teknolojia, ulimwengu wa digitali, maisha ya harakaharaka, maisha ya njia mkato iwe kwa kuvunja sheria za kawaida au kukatisha maisha ya mwanadamu mwingine, maendeleo hayo.
Najua kuwa Mzee Zuzu sina ubavu wa kubadilisha maisha hayo, lakini najua kuwa kuna viongozi bora wanaopingana na bora viongozi ambao hao kwao wanakubalika zaidi na waliowavisha magwanda yao, wale wajinga wao wanaopelekwa na umaskini wao na kuwafanya wachache wanaojua ukweli wakiumia kwa jasho lao, na wakanyang’anywa na wavalishwa magwanda kiimani bila sheria kufuata mkondo wake, hayo ndiyo maendeleo ya kweli.
Kwamba, kula kwa jasho lako si jambo la hekima bali kula kwa jasho la mwingine ndiyo mambo ya kidigitali kwa maisha ya leo, na ndiyo maana tunaishi kwa nguvu za wazee badala ya nguvu za vijana, tunategemea mawazo ya wazee na kuyachakachua badala ya fikra tunduizi mpya za vijana wasomi wa leo kidigitali ya kweli.
Najua tutafika mahala ambapo tutajiuliza maswali mengi kama mgonjwa ambaye yu mahututi, lakini vipimo vyote vya kisasa havioneshi anaumwa nini. Tutaingia imani za kishirikina na kuamua tena kwa kauli moja kama Taifa kwamba tujipeleke kwa sangoma tukapigiwe ramli kumjua mchawi wetu.
Digitali itakuwa si yetu tena na itabidi tuzime na tuwashe analogi ili tujipange upya kwa ajili ya digitali ya elimu, afya, kilimo, imani za dini, heshima, utii wa sheria bila shuruti, kuheshimu Katiba na kadhalika.
Mkitaka kwenda kwa sangoma kitaifa, mnifuate niwaelekeze alipo kama si Butiama maeneo ya Mwitongo basi itakuwa Monduli. Huko kote nilikuwa nawafahamu waganga wa ukweli zamani, sina hakika kama bado wazima hawajatangulia mbele ya haki, lakini kama wametangulia tujue tunapaswa kujiganga maana hakuna mganga mwingine labda azaliwe leo.
Mzee Zuzu
Kipatimo.