Wiki jana, niliandika makala niliyojaribu kupendekeza kiongozi tunayemhitaji, na niliahidi kuwa mmoja wa wagombea katika nafasi ya ubunge kama nitajiridhisha kuwa suala la kuchafuana kwa maneno halipo tena.

Makala yale yalilenga nafasi zote za uongozi kuanzia serikali za mitaa hadi ngazi ya urais. Nilisema vile kwa kuwa najua unafiki wa viongozi wabovu, kwamba wao huanza kujitakasa mbele ya watu na kuwa wanyenyekevu kwa muda, ili wapate madaraka na hapo ndipo tutakapogundua kuwa huyo ni nyoka kuliko huyo mjusi aliyetajwa kuwa nyoka.


Watanzania wenzangu, sasa tunaelekea katika mchakato wa kubadilisha awamu nyingine kama ambavyo wenzetu wengine wa Afrika Mashariki, yaani Kenya walivyoweza kufanya mabadiliko ya watawala, ambao wana muda wa kuweza kuthibitisha kama wao ni mijusi na si nyoka kwa Wakenya.


Nimewiwa kuandika barua hii kwa kuwa naona wingu zito la ‘uongo mtakatifu’ unaozidi kuzagaa miongoni mwa jamii katika kujisafisha kundi fulani dhidi ya kundi jingine, ambalo lipo kimya juu ya uongozi – uwe wa serikali ya mtaa au ubunge au hata urais – kama imefikia katika kiwango hicho kwa sasa, sina hakika.


Ningependa Watanzania wote tuwe kama mimi ama wazee  wenzangu wa miaka ile ya uchaguzi wa jembe na nyumba. Uchaguzi ule haukulenga majungu ama makundi ndani ya chama kimoja, na ni ukweli usiopingika ndipo tulipowapata viongozi wa umma na si viongozi wa kundi fulani.

 

Ningependa nishauri turudi kule ambako tulitoka sisi na viongozi wetu, na kisha tujiulize maswali machache yafuatayo ambayo kimsingi siku zote nayaita ya kipumbavu kwa wenye akili; ni kiongozi gani wa jembe na nyumba ambaye alijilimbikizia mali? Ni kiongozi gani aliyetangulia mbele ya haki kama Julius ambaye kaacha utajiri uliotukuka wakiwamo akina Edward, Rashidi, Mzee Mgeni, Makwetta, Elinawinga, Jamal na wengineo?


Hawa ndiyo wanaoweza kuonekana walikunywa maji ya bendera ya TANU kwa maana ya kuwatumikia wananchi, wanachama, umma, chama na kisha Taifa kwa ujumla, hawa ndiyo ambao leo wameweza kuchora ramani halisi ya Taifa hili ambalo tunajivunia kwa sera ambazo ziko wazi tangu awali, sera ambazo tulikubaliana katika maazimio mengi ya wakati ule kwamba chama ni cha wakulima na wafanyakazi, na si wafanyakazi na wafanyabiashara.


Hotuba ya mwisho ambayo niliisikia katika redio yangu ya kizamani iliyosemwa na Julius mjini Dodoma wakati wa uchaguzi wa rais mwaka 1995, alisisitiza mambo makubwa manne lakini katika hotuba yake alionekana bado kupinga sana wafanyabiashara kuingia katika mfumo wa siasa na uongozi, kwa hofu ya mazingira ya utata wa kimaslahi kwa watawaliwa.

 

Hotuba ile ina mashiko hadi leo, alizungumza kwa dhati ya moyo wake na kama vile mtoa usia anayejua kuwa hii ndiyo kauli yangu ya mwisho kwenu, hana njia mbadala ya kuwafundisha nini cha kufanya kumpata kiongozi bora.


Naandika barua hii kwa nia ya kuwashauri mnaojiingiza katika sera ya mgawanyo kuwa huko ni kubaya na pengine tusiombe tufike kwa faida ya kizazi kijacho, tuanze kupinga kubaguana kwa makabila, vyama, ukanda, na ushirika wa kimadaraka, hakuna mmiliki wa Taifa hili zaidi ya Watanzania wote, tulikabidhiwa na mkoloni.


Taifa hili ni letu na wamiliki ni sisi, na  viongozi wote wenye kuheshimu misingi ya uongozi na hata wale wenye mbwembwe na kulewa madaraka tumewaajiri sisi kwa kura zetu, tusikubali mambo yao ya kutunyanyasa baada ya kuwapa ajira ambazo ni za muda mfupi, ajira ambazo wanazitumia kwa manufaa yao na si yetu ambao ni waajiri.


Tusigeuzwe mazuzu ndani ya vyama vyetu kwa maneno ya kizushi na kujitakasa wakati ni wachafu, muda wa uchaguzi bado wangojee wakati wa kampeni lakini pia watueleze walichukua hatua gani kwa hao wanaowachafua wakati wakiwa madarakani.


Siku chache zilizopita nilimsikia mkuu wa nchi akitoa onyo kwao hao wachaguliwa yaani tuliowaajiri, alisema makundi yote yaishe, aliowateua wafanye kazi, atakayeshindwa atawajibika yeye na wenzake wote, tunategemea wafanye kazi wasifanye majungu lakini pia vyama vingine navyo vifanye kazi ya kuielekeza serikali na siyo kungojea tatizo litokee ndipo waanze kutoa lawama na kuanzisha majungu.


Sina chama chochote mpaka leo, mimi ni muumini wa chama cha TANU na bado sioni mahali pabaya ambapo sera zetu za kizamani zimepitwa na wakati, bado naamini chama cha wakulima na wafanyakazi, bado naamini katika ujamaa na kujitegemea, bado naamini katika Azimio la Arusha, bado naamini katika maadui wakuu watatu, bado ni wa zamani lakini wa leo kifikra.

Mzee Zuzu,

Kipatimo.