Kuna wakati nakumbuka miaka yetu ya giza totoro la habari, kwamba habari ilikuwa ni kitu nyeti ambacho mwananchi alipaswa kujua kwa gharama ya muda au kwenda safari kuitafuta, leo habari unaipata mahala ulipo na unachagua unataka habari gani.

Napenda upatikanaji wa habari mchanyato kwa wakati muafaka na pia napenda wingi wa vyombo vya habari ambavyo vinatoa habari kwa wakati kwa kuwa sihitaji kutumia gharama zile za zamani  za muda wala kusafiri ili kupata habari.

 

Nimeamua kuandika waraka huu mahususi kutokana na ukweli uliopo katika habari zetu ambazo tunazipata katika vyombo vyetu ambavyo tunaviamini na Serikali  ikaamua kuvisajili rasmi  ili vitoe habari kwa wananchi, lakini sielewi lengo la habari hizo ni lipi.

 

Zamani tukiwa wadogo na ninadhani tukiwa katika mfumo wa kizamani yaani mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea tulikuwa na vyombo vya habari, wengi, hasa wale wa leo wataona vyombo vile vilikuwa vya kishinikizo na vilikuwa havitoi habari kwa wakati.


Naweza nikakubaliana nao kimsingi hasa ukizingatia mabadiliko makubwa ya kimaisha na kiuchumi ambayo leo yapo, lakini kama taifa  tunazidi kupotea kwa sababu kubwa mbili mosi tunapoteza Utanzania kiutamaduni na pili tunauza uhuru wetu kwa kupata habari ambazo zinatufanya tusiwe sisi kama tulivyo.


Kwa hoja yangu ya kwanza ya kupoteza utamaduni wetu wa Utanzania  katika habari, inatokana na habari ambazo tunalishwa na hao ambao wanadhani kuwa habari ambazo wanatupatia ndizo tunazohitaji kutokana na mahitaji ya wakati huu.


Zamani, tulikuwa tukipata habari ambazo zilikuwa zinatufundisha jambo muhimu kwa wakati huo, mathalani kama ni kilimo cha mpunga basi tulikuwa tukielekezwa kilimo hicho cha mpunga katika mazingira yetu na mafanikio ambayo yalikuwa yakifikika katika mahadhi yetu.


Nimetoa mfano wa kilimo cha mpunga lakini mifano ni mingi sana, zilikuwapo habari kama za maradhi, michezo, uchumi, utamaduni nakadhalika na zote zilibeba mandhari ya kwetu na zilikuwa zinakusudia kuongeza mapambano na ufanisi katika mazingira yetu.


Leo ni tofauti sana, hatuna tena uwezo wa kupata habari za kilimo chetu, maradhi yetu yanayotusibu kutokana na mazingira yetu, hatuna tena michezo yetu tunayoifahamu kutokana na mazingira na makuzi yetu, hatupati tena habari za ngoma zetu ambazo zilikuwa zikiimbwa katika mazingira na utamaduni tunaoufahamu.


Hivi ndivyo vyombo vyetu vya habari ambavyovimeamua kutulisha taarifa ambazo siyo zetu, dhima kubwa ya chombo chochote cha habari ni kutoa habari yenyewe, kuiburudisha jamii, na mwisho kuelimisha jamii yake inayopokea hiyo habari.


Kwa waraka huu nataka kuiuliza jamii yetu, hivi ndivyo ambavyo tunavipata kutoka katika vyombo titiri vilivyopo na kuweza kutupa habari muhimu kwa mazingira yetu? Je habari hizo zinatuburudisha ipasavyo kimaadili? Na mwisho ni elimu gani tunayopata kutokana na mazingira tunayoishi sisi tunaopata habari.


Pili nataka kujua uhuru wetu uko wapi? Maana kubwa ya uhuru ni kujitawala na kuwa na utamaduni wetu, swali tunalopaswa kujiuliza ni kweli kwamba wingi wa vyombo vya habari tulivyonavyo vinakidhi matakwa ya walio huru ama tunatafutiwa mkoloni?


Haya ni mawazo yangu kama Mzee Zuzu lakini nilidhani tunapaswa pia kujua hatima yetu ya kuwa na mlolongo wa vyombo vya habari ambavyo vingi kati ya hivyo havikidhi haja ya kutupatia habari na kuendeleza utamaduni wetu, japokuwa katika burudani nadhani tayari wanamakoloni yao ambayo yanaridhika na kile ambacho wanapata.


Kuna wakati ilisemwa kuwa ipendekezwe vyombo vya habari kuwa muhimili mmojawapo wa dola, mimi nilikubali kwa kuwa bila vyombo vya habari mambo yanaweza yakasimama lakini swali la kujiuliza tunatoa habari gani kwa hiyo jamii ambayo tunaiomba ituunge mkono kuwa muhimili wa dola?


Sisi kama wanahabari tuna nafasi gani kuieleza jamii kuwa tunanguvu katika kuleta taarifa za msingi kwa wakati na maadili yenye ukomavu na kuifanya tasnia ya habari iweze kuheshimika na kuogopwa kama tungekuwa muhimili wa dola kiukweli?


Haya ni maswali machache tunayotakiwa kujiuliza halafu turejee kule ambako kulikuwa na uhaba wa habari na vyombo vya habari na tuone jinsi ambavyo vyombo vile vya kikoloni vilifanya nini na sisi wa kileo tunafanya nini ili tuheshimike zaidi.

Wakatabahu

Mzee Zuzu

Kipatimo.