Kuna wakati huwa najiuliza kama kweli kuna watu wengine wanafikiria kama ninavyofikiria mimi kizuzu, hasa katika kipindi hiki cha biashara huria na mfumo wa vyama vingi na mbwembwe za kuomba kura kwa kunadi mahitaji ya wapigakura, bila kujali athari ambazo zitajitokeza baada ya kuruhusu mahitaji yao.

Kuna wakati niliwahi kuandika juu ya hili, tena nikimwomba Mkuu wa Usalama Barabarani, aliangalie kwa jicho la tatu na kutoa mapendekezo yake, lakini naona ni kama vile barua ilipokewa na kutupwa katika kapu la takataka. 

Naamini tangu wakati ule barua yangu ikitupwa katika ‘dust bin’ ilianza kuondoka na roho za wananchi wengi wasio na hatia na viungo vyao pia kupunguzwa mwilini, huyu naye anaweza kuwa jipu kama hili halioni na hawezi kutumia madaraka yake kwa weledi wa taaluma yake.

Siku za hivi karibuni kumetokea kuimarisha kwa huduma za afya hasa katika hospitali zetu za rufaa. Tumeona jinsi wagonjwa wengi walivyokosa huduma bora za kiafya kutokana na kuzorota kwa uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wao.

Baadhi ya huduma ambazo zilipewa kipaumbele ni pamoja na huduma za akina mama na mtoto, vifaa tiba, dawa na uboreshaji wa utumishi katika hospitali zetu. Naamini hili limefanyika hata katika hospitali nyingine za wilaya na mikoa kwa lengo la kuhakikisha huduma bora inapatikana kwa wakati na vizuri.

Mtu anayefikiria kizuzu kama mimi angeanza kufikiria jinsi ya kudhibiti madhara yanayotokana na mazingira wezeshi ili kuweza kusaidia jamii kuepukana na madhila hayo, suala la kusafisha mazingira ni bora zaidi kuliko kutibu kipindupindu kwa gharama kubwa au kupoteza maisha ya watu.

Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine duniani zina sheria ambazo zinapaswa kufuatwa, kwa mujibu wa utawala bora wowote duniani. Nchi yetu siyo kisiwa cha kuwa na ustaarabu wetu pekee bali ni nchi miongoni mwa nchi nyingine ambazo tunaingiliana kielimu, kiustaarabu, kiutamaduni, kiuchumi na kadhalika.

Nchi yetu inapaswa kuangalia vipaumbele katika sekta zote ili iweze kwenda mbele kiuchumi, na maendeleo siyo umiliki wa mali bali inaweza ikawa na umiliki wa elimu bora ambayo inatusaidia kuchanganua mambo ya msingi yanayotupa taabu. Kwa ufupi, kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto ni bora zaidi kuliko kumiliki mali nyingi.

Hivi sasa katika nchi yetu tunakabiliwa na tatizo la ajira kwa ngazi zote, na viongozi wetu wanalijua hilo kwa mapana na marefu na wanajua athari kubwa zitokanazo na upoteaji wa nguvu kazi hasa za vijana ambazo ni muhimu zaidi katika kukuza uchumi wa nchi.

 Viongozi hawa hawa wanajua athari za ajira mbalimbali zitokanazo na ajira mbaya na huzitumia wakati wakiomba kura za wananchi ili ziweze kuwapa uongozi. baada ya uongozi husahau kuwa ajira zile zinawapunguza wapiga kura wake kwa vifo na afya zao.

Leo nakumbusha tena, kwa uzuzu wangu siamini kabisa kama pikipiki ni ajira kwa vijana  bali ni uchunguliaji wa mtutu wa bunduki ulioshikwa na mwendawazimu kwa abiria, vijana wengi wamejikita katika biashara hii kwa kukurupuka kutokana na kutotayarishiwa mazingira mazuri ya kuwa na kazi ambazo siyo hatarishi.

Vijana wengi wanamiliki pikipiki bila kujua kuendesha na sheria za barabarani, hawavai kofia, hawafuati sheria, wanapakia abiria wengi kwa wakati mmoja na wanapita mbele ya askari bila kujali kama kuna sheria za barabarani ama la.

Kuna ajali kila uchao, ajali ambazo zinapoteza maisha ya watu wengi wakiwamo akina mama, watoto wachanga, wanafunzi na hata wao wenyewe, wameendelea kwa kutumia pikipiki kufanya uhalifu, uhalifu ambao sasa unazidi kushika kasi.

Kwa kuacha biashara hii ‘haramu’ iendelee mambo yafuatayo tunapaswa kuyafanya; kuimarisha huduma za afya kwa kununua dawa nyingi kwa ajili ya wanaopata ajali, kuongeza na kusomesha madaktari wengi zaidi, kuongeza vitanda, wodi, kupanua na kujenga mochari nyingi zaidi.

Kuongeza benki ya damu kwa kuwakamua wasio na hatia, kuongeza Jeshi la Polisi kushughulikia ajali za barabarani, kuongeza Jeshi la Polisi kuwalinda watu na mali zao, kutumia fedha nyingi za kigeni kununua vipuri mbalimbali vya pikipiki badala ya mbolea.

Nina mengi ninayoweza kuzungumzia juu ya athari za ajira za pikipiki, lakini naamini wasio mazuzu kama mimi wanaweza kuchambua vizuri zaidi tatizo hili, haiwezekani nchi yenye wasomi tuaminishwe kuwa pikipiki ni ajira na siyo usafiri wa kawaida unaofuata sheria.

Tanzania bila vilema, vifo, ajali za pikipiki inawezekana lakini Tanzania hiyo hiyo kwa siasa za kupewa kula na siyo kura vyote hivyo vinawezekana.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.