Mwaka 1973 hadi 1974 tuliamrishwa tuishi pamoja katika Vijiji vya Ujamaa, lengo likiwa ni kusogeza huduma za jamii kama zahanati, shule, maji na maendeleo kwa ujumla wake, karibu kwa wananchi wote.
Lilikuwa jambo gumu kukubaliana hasa ukizingatia kuwa uwezo wetu wa kuelewa ulikuwa mdogo baada ya miaka michacha ya uhuru, na hatukujua sheria za nchi kwa maana ya Katiba, na elimu ya ngumbaru ilikuwa bado kuenea nchi nzima.
Baada ya miaka yote ya kuishi Tanzania na kupitia taratibu zote za sheria, nimegundua kuwa maisha yangu ni bora yanapokuwa chini ya utawala wa kisheria badala ya kuishi kama mnyama katika mbuga ya wanyama. Nimethubutu kuishi kwa amani kwa sababu nafuata sheria za nchi na hili kila Mtanzania anapaswa kulifahamu na kulitenda.
Hivi sasa kwa kizazi chetu cha leo, kila siku watu wanalalamika kutotendewa haki kutokana na jinsi Serikali inavyowafanyia. Ni kipindi ambacho elimu imetolewa kwa kiwango cha juu sana kuliko wakati wetu, ni kipindi hiki inakopatikana katika kila taasisi, ni kipindi ambacho vyombo vya sheria vimetapakaa karibu kila kona ya nchi yetu.
Utii wa sheria bila shuruti ni kaulimbiu ya Jeshi la Polisi, lakini kwangu mimi naona ni kauli ya serikali yoyote makini kama hii iliyopo madarakani.
Uzuri wa sheria huwa inauma pande zote, uzuri wa sheria unatufanya tuishi kwa amani tukiwa na matumaini ya amani ya kesho yetu. Siku za hivi karibuni hapa nchini kumejitokeza katiba nyingine ya watu wachache ambayo wao kwayo waliamua kuitumia pasi na Katiba kuu ya Taifa, walitumia katiba yao kutuaminisha kuwa huo ndiyo mwongozo mkuu wa Taifa hili na kwamba tunapaswa kuwafuata wao waliosoma katiba hiyo ili tuishi watakavyo wao.
Katika katiba hiyo yao, walituaminisha kuwa anayetumia Katiba kuu ya nchi ni mnafiki, mzandiki na mpenda sifa. lakini walifika mbali zaidi na kumwona mpenda Katiba kuu ni mtu wa zamani asiyetaka kwenda na wakati na kwamba maendeleo yasingeweza kufika mapema. Hawa wote walitenguliwa madaraka na kutolewa kafara.
Kundi hili la watu wachache waliotumia katiba yao kwa manufaa yao tulipoamua kutumia Katiba ya wote, wameanza kuona kama wanaonewa, wanatafuta usaidizi wa kutetewa na waliokuwa hawatumii katiba yao, baadhi yao ndiyo waliotuuzia viwanja mabondeni, sehemu za wazi na hata maeneo hatarishi.
Baadhi yao ndiyo waliogeuza miradi ya kitaifa kuwa miradi yao binafsi na familia zao, waligeuza ofisi za Serikali kuwa mali zao binafsi, waligeuza mali ya umma kuwa mali zao binafsi na walitumia kifungu chao cha sheria kuwa madaraka siyo dhamana ya wananchi bali ni dhamana ya kifamilia.
Leo yanapotumbuliwa majipu ya katiba ile ndogo ya watu wachache, kuna watu hawataki kukubaliana kama ilivyokuwa kwetu miaka ile ya 1970, hawataki kusikia mtu akichukuliwa hatua kwa kukiuka Katiba yetu kuu ambayo ilisahauliwa na sisi wengi baada ya kupumbazwa na malikauli zao.
Leo tupo nyuma kuwatetea na kuwaona wanaowatumbua majipu ya Katiba kuu wana makosa kwa sababu hawakupaswa kufanya hivyo baada ya kuaminishwa kijinga, leo wanaotumbuliwa wanajua wazi kuwa walitumia katiba yao na siyo Katiba yetu wote katika kujinufaisha na kujijengea himaya ya kutufilisi Watanzania wote.
Utii bila shuruti ulipaswa kutumika kwa mtu yeyote anayelitakia mema Taifa hili na pengine tungetumia Katiba kuu tangu enzi zile basi tungekuwa tupo mbali kimaendeleo, naheshimu Katiba ya nchi na ninajua kuwa iwapo kila mtu atafuata sheria, basi tutakuwa na amani na maendeleo yatapatikana.
wasaalam
mzee zuzu
kipatimo.