Kama ilivyo ada, sina budi kuanza na salamu za kiungwana kama Mtanzania mwenye kuheshimu mila na desturi zetu. Sisi Watanzania tulipandiwa mbegu hiyo na hatuna budi kuiheshimu na kuiendeleza, ndiyo maana ni rahisi zaidi kumjua Mtanzania halisi kwa kupitia salamu na jinsi anavyowaheshimu watu wengine.
Katika hili kunaweza kukawa na baadhi ya wenzetu ambao wanaharibu taswira ya Utanzania, kwa kudhani kwamba kudharau utamaduni wako ni maendeleo. Katika hili pia wapo wenzetu wachache, nadhani ni wale wanaokwenda na wakati zaidi wa Kimagharibi na kupuuza uhalisia wa utamaduni wetu.
Nianze kwa kuwapa pole ya uchovu, sikuwahi kufikiria hata siku moja kwamba dunia ya Tanzania inaweza kwenda kasi ya namna hii, kila siku mwaka mmoja naona ni kama siku moja, kichwa kinajaa mno na mambo ni mengi kwa wakati mmoja wa maisha ya leo, zamani kila kitu kilikuwa rahisi labda kutokana na mfumo tulioishi, leo tunapata uchovu zaidi wa akili, si nguvu.
Dunia inakwenda kasi kiasi kwamba ukikosea kidogo unaweza kuona uko nje ya mfumo wa maisha, unaweza kupambana na maisha ambayo hukuzoea kutokana na teknolojia iliyopo, nawapa pole wazee wenzangu ambao mnalazimisha kukimbia na dunia inayokwenda kasi kuliko mlivyozoea, kasi katika teknolojia, siasa, utamaduni, michezo na maisha kwa ujumla.
Pamoja na yote hayo, bado nimeamua kushika kalamu kuwapa pole kwa matukio makali yanayotukuta kama vifo, ajali, uhasama, uhalifu, unafiki, upweke, wivu, majanga na maradhi. Najua zamani kulikuwa na baadhi ya hayo na hasa yale ambayo ni ya asili kama vifo. Lakini leo kuna hata vifo ambavyo ni feki na vifo ambavyo vinatengenezwa na binadamu wenzetu.
Tuna matatizo mengi yanayotusibu kama wananchi lakini leo nimeamua kulisema moja ambalo kwa kweli linakera sana iwapo limekutokea, nalo ni urasimu wa Kitanzania, iwapo halijawahi kukutokea, basi nina hakika nitakachozungumza hutaweza kukielewa mpaka pale kitakapokutokea.
Labda wengi hawajui urasimu ni nini. Kiufupi urasimu ni jambo ambalo linafanyika kwa kufuata taratibu zinazostahili, jambo rasmi la kufanyika ili uweze kuvuka kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. Tunauona huo urasimu katika mazingira mengi, ukienda hospitalini hauwezi kuonana na daktari moja kwa moja mpaka uandikishe jina, ufanye malipo ya awali na upange foleni ya kumuona daktari, huo ndio urasimishaji wa mambo ulivyo.
Katika kufanya hivyo, tunafuata sheria na kupunguza msongamano na malalamiko mengi ambayo hayana maana. Sasa hapa kwetu kuna wa dunia nyingine kabisa, na maana nyingine kabisa, kuna urasimu unaofanya mambo mengi kukwama na hata kuleta malalmiko ambayo si ya maana kabisa kiasi cha kuona dunia inakwenda kasi ya upande wa pili. Hili ndilo ambalo leo limenishikisha kalamu kuandika waraka huu.
Swali rahisi linaweza kuwa, tuanzie wapi kufuta urasimu wetu wenye maana tofauti na dhana halisi? Tumeona siku kadhaa za nyuma baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali wakipigia kelele jambo hili akiwemo mkuu wa nchi juu ya urasimu wetu wa kutafuta mipango ya kando na kuleta dhana ya rushwa, tumeona jinsi ambavyo watu wanatumia urasimu kukwamisha mambo kwa manufaa yao.
Mtu akiniuliza leo nia hasa ya urasimu wetu ni ipi? Jibu ni rahisi sana kwamba suala la rushwa bado ni tatizo kwa waajiriwa wengi, lakini jibu la pili ni kwamba wengi wetu hatujui tunafanya nini au tunafanya kazi kama mazoea ya kufuata reli bila kujali mabadiliko yaliyopo sasa hivi kwenye dunia inayokwenda kasi sana.
Kuna madhara mengi ya urasimu wetu kwenye mambo ya msingi ambayo kimsingi kama ningekuwa na mamlaka basi kuna watu ambao nadhani ningewapunguza ili kutoa ile dhana ya kutaka rushwa au kutaka kujithibitisha uwepo wao kwa kusumbua watu katika nafasi zao, lakini kubwa zaidi ni kupoteza fursa ya kutumikiwa na watu ambao labda wangeweza kuleta manufaa na tija kwa taifa.
Swali jingine rahisi, hivi ni kweli tunashindwa kubadililika? Tuna sababu ya kutumia teknolojia ya zamani katika ulimwengu na Tanzania inayokimbia mwendo wa kasi?
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.