Nianze na salamu kama kawaida na kuwapa pongezi tena ya kuendelea kuwa nasi katika gazeti letu ambalo nina hakika tunawafikia vizuri na tunawafikia pale ambapo wenzetu wengi wamekoma.
Lengo letu hasa ni kuwapa taarifa na si kuwapa uzushi, tunaahidi mwaka huu utakwisha tukiwa tumefika mbali zaidi ya pale wenzetu walipoishia.
Sisi huwa tunakumbuka miaka 23 ya Julius, ni miaka ambayo aliishi Ikulu na kuitumikia Tanzania, halina ubishi na ndiyo maana wengi wetu tumediriki kumuita Baba wa Taifa.
Kuna sababu inayotusukuma katika mioyo yetu kukubaliana kuwa Julius alikuwa na maono ya taifa hili na alikuwa na upendo kwa taifa hili, kwa ufupi unaweza kusema alikuwa mzalendo wa dhati kabisa tena namba moja.
Baada ya kuwepo Ikulu kama rais aliwashitua viongozi wengine wa Afrika pale aliposema ameongoza nchi hii kwa miaka yote tangu tupate uhuru na kwa wakati huo aliona ni busara kuondoka na kumwachia madaraka mtu mwingine ili aweze kuongoza kwa maono mapya, dunia ilitahayari na viongozi wengi waliolewa madaraka na hasa Afrika hawakumuelewa, sisi wenye kumjua tulimuelewa.
Waraka huu unasomwa na watu wengi lakini wengi wao hawajui uwajibikaji katika awamu ya kwanza ulikuwaje, tunaojua na kukumbuka tunaona kama hakuna tofauti sana na Awamu ya Tano, tofauti zipo kadhaa ambazo zinatokana na maendeleo ya leo na umaskini wa wakati huo.
Tofauti zipo kutokana na mabadiliko mengi yaliyotokea katika awamu za katikati na sasa, na yote haya ni matokeo chanya ambayo yamesababishwa na awamu zingine ili kuweza kupiga hatua katika awamu hii.
Ili kuifungua dunia hapa kwetu ilibidi awamu ya pili ya miaka kumi uwepo uhuru wa biashara na hiyo ilitokana na ukweli kwamba miaka yote ya nyuma tulikuwa tukiamini katika ushirika na tulifanya mambo mengi kwa ushirika.
Dunia inabadilika na inakuja na sera mpya kila wakati, kwa utaratibu wetu wa kukabidhiana vijiti tunaweza kuhimili kubadilisha sera ambazo kiongozi alikuwa muumini nazo na kumwachia mwenzie pasipo kugeuka jiwe la chumvi.
Uhuru huu wa biashara ulikuja na makandokando yake ya kuharibu hata pale ambapo tuliweka misingi imara, kiongozi wa awamu hiyo akapewa lawama nyingi bila kujua ni kwa sababu gani lakini tulipita na nchi ikawa imara na salama.
Miaka kumi ya utandawazi iligeuzwa na baadhi ya wananchi kama kipindi ambacho kilikuwa cha kila mtu kuchukua kilicho chake, ni kipindi ambacho sera za dunia zilibadilika na kuifanya dunia kuwa kijiji, suala la uwekezaji likawa jambo gumu kwa wananchi kulielewa lakini nalo lilipita na masika yake na nchi iliendelea kuwa palepale.
Miaka kumi ya Awamu ya Nne ya kasi ya maendeleo ikiwa imegubikwa na makandokando ya awamu ya ruksa kufanya chochote na dunia kuwa kijiji na kuelemewa na dhana ya uwekezaji wa mitaji katika nchi maskini ilikuja na kasi yake ya kukabiliana na maendeleo hayo, hata hivyo awamu hiyo iliweza kuiweka nchi katika mstari na kuweza kuikabidhi salama kwa viongozi wa Awamu ya Tano.
Hatimaye awamu ya miaka hii kumi ya kufanya kazi ikaingia madarakani, inapokea makandokando mengi ya awamu zote zilizotangulia, ni awamu ambayo imefikia katika sera ya kidunia kuifanya Afrika kuwa mtaji wa nchi za Ulaya.
Ni awamu ambayo imepokea nchi kukiwa na kukata tamaa kwa wananchi na baadhi ya wananchi kuupoteza taratibu uzalendo wao, ni awamu ambayo viongozi wengi wenye maadili wamezeeka na hawawezi kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni awamu ambayo wachache waliamua kujilimbikizia mali ya umma bila kuwa na haya.
Kutokana na athari hizo, watendaji wengi wameshindwa kujitoa katika mfumo mbaya ambao ulitengenezwa na wajanja wachache ili waweze kuishi, madhara makubwa yanawakumba wenye dhamana ya uongozi na wanaweza kushindwa kukabiliana nao kutokana na namna walivyojipanga.
Leo nimeanza na unabii katika uongozi wetu, kuna mambo ambayo yanaendelea na wengi hawayajui, lakini ili tufike huko ni lazima jasho la damu litoke na wajanja walimie meno, nitatabiri kwa maono yangu nini kitatokea wakati wa awamu hii na ijayo.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.