Leo nimeamua kuanza na kauli hii kutokana na jinsi ambavyo uamuzi wa suala la makinikia lilivyovaliwa njuga na mkuu wa kaya na kuonesha wazi kuwa hakuna linaloweza kushindikana iwapo dhamira ya mtu binafsi inaweza kuamua kufanya jambo.
Nimewaza mambo mengi sana ambayo yalishindikana katika miaka yetu ya nyuma, nimewaza kama tungeweza kuyafanya haya tangu zamani, labda leo Tanzania mpya ingekuwa Tanzania ya kutoa misaada kwa nchi maskini nyingi barani Afrika na hata katika nchi za Ulaya.
Najua kuwa yapo mambo mengi makubwa ambayo siwezi kuyataja hapa kwa kuhofia kuchoma mioyo ya watu, lakini lengo langu si kuwaumiza watu ni kuonesha jinsi gani kama Taifa tumeliwa na tunatakiwa kuchukua hatua kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo.
Siyo rahisi kuanza na kila kitu na wakati mwingine ni vema tukaanza na jambo ambalo lina ushahidi wa kutosha juu ya udanganyifu au wizi, itasaidia kuondosha lawama za kuonewa na kuondoa sura ya malalamiko ya dhuluma.
Nchi yetu imekuwa na mikataba mingi ambayo inalifanya liendelee kuwa maskini kila siku, kuna mikataba ya dhuluma ambayo ipo kisheria na bado itaendelea kuwapo iwapo hatutakuwa na watu wenye uamuzi wa dhati ya moyo na kujitoa mhanga kwa ajili ya wengi.
Iwapo tutaweza kukabiliana na mambo yote yanayofanyika katika Taifa letu, basi ni dhahiri kuwa tutakuwa tumeanzisha mfumo mwingine mpya wa mapato zaidi ya yale ambayo tulizowea kabisa kuyakusanya katika vileo, mazao, ushuru wa bandari na kadhalika.
Kwa makinikia pekee yake ambayo Watanzania wote sasa wanajua tumedhulumiwa kiasi gani, yangeweza kuendesha bajeti ya nchi yetu kwa miaka kadhaa kwa bajeti iliyokamilika kabisa na kutekelezeka, hivyo basi ina maana kwamba fedha ambazo Bunge linaidhinisha zingeweza kuwa za matumizo mengine kwa maendeleo ya Taifa letu.
Nimejaribu kufikiria kama bajeti ingekuwa inajitosheleza ni jinsi gani ambavyo hospitali zetu zingekuwa zinatoa huduma bora kabisa kwa maana ya dawa, vifaa tiba na malipo mazuri kwa madaktari na wahudumu wa afya, lakini tulishindwa kwa sababu ya mikataba mibovu katika mradi mmoja tu kati ya mingi.
Nafikiria kama tungeweza kukusanya mapato yetu vizuri ni jinsi gani ambavyo wanafunzi wetu wangepata elimu bora kwa maana ya kuwa na walimu wanaolipwa vizuri na kufanya kazi kwa motisha, jinsi ambavyo madarasa yangekuwa bora kwa wanafunzi kukaa kwa amani na furaha, jinsi ambavyo wanafunzi wangeweza kupata lishe na huduma muhimu za shule kwa kuwa Serikali inaweza kukabiliana na huduma hizo.
Nafikiria iwapo tungeweza kukusanya vizuri kodi katika madini, hoteli, utalii, viwanda na kadhalika Serikali ingeweza kufufua viwanda vyake na kuongeza pato la Taifa na ajira kwa vijana hapa nchini, naiona taarifa ya ajira kutafuta wafanyakazi kichwani na siyo wafanyakazi kutafuta ajira kama ilivyo sasa.
Nafikiria kama tungezingatia maadili ya uzalendo uliokuwapo enzi hizo, basi ni dhahiri kila kitu kingekuwa chetu na siyo chao, kila maendeleo yangekuwa yetu na siyo yao wachache ambao wanadhulumu hadi haki ya watoto wadogo waliozaliwa katika ardhi waliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa utajiri uliotukuka.
Najua wapo Watanania ambao limewagusa kama ambavyo limewagusa baadhi ya viongozi waadilifu, Watanzania hawa wana hasira ya mambo mengi sana, wapo ambao ndiyo kwanza wanakaribia mwisho wa maisha yao na bado hawajafaidi matunda ya Taifa lao.
Wapo ambao wanadiriki kufikiria hali ya hatari zaidi, kwamba waliotufikisha hapa wametumia rasilimali za Taifa letu kuwasomesha na kuwatumikia kwa gharama za Taifa kama mishahara na malipo ya uzeeni, lakini pia wapo waliojijengea kinga ya kutotoka madarakani wakiendelea kuingia mikataba mibovu kwa taifa, wanataka kujua hatima yao ni nini.
Leo ndiyo najua kwa mara ya pili kwamba Taifa hili ni tajiri na huenda likawa tayari ni maskini kwa kuwa wachotaji wa rasilimali walianza zamani kutufilisi, wametufiliki katika madini kwa kiwango kikubwa lakini pia hatujui juu ya wanyama wetu, ardhi yetu, viwanda vyetu, watu wetu, elimu yetu na mengineyo.
Chambilecho tusiishie katika hili moja tutupie macho na mengine yanayosemwa ili tufufue uchumi wetu.
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.