Nianze waraka wangu wa leo kuwashukuru sana wasomaji wangu wa barua zangu ambao mmenipa moyo sana wa kuandika kila iitwapo Jumanne, ili kutoa mawazo yangu ya kizuzu japo mengi ya mawazo ni yale ambayo mnanishauri ninyi wasomaji wangu.

Tuendelee kukumbushana kila wakati mambo ambayo ni ya kitaifa na yanatuhusu sisi, huu ndiyo uzalendo tunaopaswa kuwa nao bila kujali itikadi ya vyama vyetu kwa kuwa Taifa litaendelea kuwapo na vyama vinaweza kufa kama vingine vilivyokufa na kuchipua upya.

Hii ndiyo nchi yetu ambayo kimsingi ni kipande cha ardhi ambacho Mwenyezi Mungu aliamua kutukirimia sisi Watanzania, vyovyote itakavyokuwa itaendelea kuwa nchi hata kama sisi tutaamua kusema hapana kwa tamaa za madaraka na ufisadi, historia itasema ukweli kwamba hii ni nchi yetu.

Leo nimekumbuka uzalendo wa nchi yetu miaka dahari iliyopita, nimekumbuka uzalendo kwa maana ya kila mtu kuwa mlinzi wa mali na amani wa Taifa letu, nimekumbuka uzalendo wa kujali haki ya kuishi kwa kila Mtanzania, haki ya kutembea na kufurahia maisha ndani ya mipaka ya nchi inayoitwa Tanzania.

Leo nimekumbuka jinsi tulivyojengewa imani na upendo wa Taifa letu, tulijengewa kuipenda nchi kwanza, tulijengewa kuwa na hofu ya mambo ya hatari na Taifa letu, tulijengewa kuilinda nchi kama mali yetu, kutomwonea haya adui, kutompenda adui na kumchukulia hatua pasi na kupoteza muda, huu ndiyo uliokuwa uzalendo wa kuipenda nchi yetu.

Nimekumbuka jinsi tulivyowatafuta majangili kama maadui wa Taifa, jinsi tulivyohangaika na wavivu kama wanyonyaji wa Taifa letu, jinsi majambazi walivyokuwa na wakati mgumu kuishi katika nchi hii, jinsi walanguzi walivyokuwa wakiishi mguu ndani mguu nje kila iitwapo leo ya wakati ule.

Nimekumbuka jinsi wahujumu uchumi walivyokuwa wakiishi kwa maisha ya kujificha na kujiona kuwa hawana haki ya kuonana na waungwana kwa matendo yao, jinsi walivyojiona wapweke katika ulimwengu wa watenda haki na jinsi tulivyowabagua kwa matendo yao.

Nimekumbuka jinsi tulivyochukua hatua stahili kwa watoa rushwa wakati huo, nakumbuka maisha ya ndege waliyoishi hao waitwao watoa rushwa, tulikuwa wakali na tulithibitisha kuwa hatutaki watu waishi katika nchi yao kwa kutawaliwa na dhuluma bila kujali uzalendo. Huo ndiyo uliokuwa uzalendo wetu kwa Taifa letu ambalo mmelikuta likiwa na historia ya kuchukia mambo maovu katika jamii.

Leo naiasa jamii yetu irudie misingi ile ya uzalendo, naiomba kutokana na ukweli kwamba kuna mtu kaonesha uzalendo na tunapaswa kumuunga mkono, ule ujinga wa kuwaangukia watu wachache ambao siyo wazalendo tuuache ili tuweze kurudi kwenye ile nchi ya ahadi tuliyopewa na Muumba.

Leo naiona familia iliyopogoka maadili kusujudia majizi, matapeli, wauaji, wahujumu uchumi, watoa rushwa na kila aina ya uvunjifu wa sheria. Nawaona watenda makosa walivyoweza kuinunua haki kwa fedha, nawaona wasio na maadili walivyogeuka kuwa walinzi wa watenda maovu, siyo Tanzania ninayoijua mimi kwa enzi zetu za uzalendo wa kweli.

Kama ambavyo Mwalimu Julius alivyosema ukizowea kula nyama ya mtu huwezi kuacha, ndivyo ilivyo sasa kwa wale ambao walizowea maisha ya mkato, kuishi kwa wizi, mauaji, bila kulipa kodi, kuhujumu uchumi, utapeli na kadhalika; wataendelea kuishi hivyo, na tusipowafichua kwa kuwakataa basi wataendelea kututafuna maisha yetu yote.

Ni lazima uzalendo wa kusema sasa yatosha uwepo ili tuweze kusonga mbele. Hawa wasiopenda kuishi kama watu wema ni wachache lakini wanatuumiza tulio wengi, huku wengi wetu wakigeuka na kuwa walinzi wao katika kutenda maovu, wametugeuka sisi kwa sababu ya tamaa zao za fedha zinazotokana na uvivu.

Chonde tuwe wazalendo, nchi hii ni yetu, kosa linalofanywa  leo athari zake zitaendelea kuonekana miaka yote, kosa la leo ni adhabu ya kesho, na tuseme yatosha na tumuunge mkono Rais kupambana na wale wote walioamua kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.