Uswahili ni uungwana na hata kama jana tumeonana si vibaya leo tukajuliana hali na salamu, ukizingatia maisha ni mafupi na mtu husafiri na kifo chake, hii si busara kujua unahitaji kuangalia uzao wako na sasa mmebaki wangapi mtaani au kijijini kwenu.
Usiangalie wamezaliwa wangapi, angalia mliozaliwa wote, mkacheza wote na mkasoma wote, wako wapi sasa, ndipo utakapojua kuwa kifo ni kikatili sana na kimekubakiza wewe kwa makusudi ili ufanye jambo la maana la kusimuliwa na hiki kizazi kilichopo.
Wengi tunakufa na kuacha historia mbaya nyuma yetu, tunakufa tukiwa tumetenda mabaya kwa wenzetu, tunakufa tukiwa hatuna amana ya upendo tuliyoiacha, tunakufa tukiacha watu wakifanya starehe badala ya kusikitika.
Haya ndiyo maisha ya kimaendeleo yaliyoacha nafasi ya kumjua Mungu na kutenda yaliyo mema. Ni wachache wanaokufa wakaiacha jamii ikisikitika kuhusu kuondoka kwao, kwa ufupi tuna vituko mpaka kimekuwa kichekesho kwa uhai wetu.
Mara kadhaa huwa najiuliza, nini kimetokea sasa hivi mpaka binadamu anakuwa hana thamani tena katika maisha yake na hasa jamii inayomzunguka? Ni kweli kwamba maisha ya binadamu yamekosa utashi wa kujua mema na kuwa wazalendo kwa ardhi ambayo Mwenyezi alitukirimu kwa upendo wake?
Wakati tukizaliwa sisi nchi hii ilikuwa ya wakulima na wafanyakazi, wanasiasa walikuwa wachache sana, hasa siasa za majukwaani na katika vyombo vya habari. Zamani siasa ilikuwa ni kilimo, siyo siasa ajira kama sasa hivi. Swali langu kubwa kila siku ni kwanini Watanzania walio wengi kwa sasa ni wanasiasa ambao si wakulima na wafanyakazi? Wengi wao huamka na vikao vya posho na kulala na miadi ya vikao vingine kesho yake, tena vyenye miposho huku wakituahidi kutupa maendeleo na kutatua matatizo yanayotukabili kupitia vikaoposho vyao.
Nafahamu tuliingia katika mfumo wa vyama vingi, na ipo kikatiba na kwamba siasa ya vyama vingi nchini ipo kisheria na ni demokrasia, shida yangu si vyama, ni malumbano badala ya kazi, shida yangu si viongoziposho ni viongozi maendeleo, huu mfumo wa vyama na wanasiasa naona kama umeingiliwa na kitu ambacho wengi wetu hatujakitambua, kuna kitu kinachoitwa kivuli cha uvivu wa kufanya kazi na hata kusingizia demokrasia.
Nimefuatilia mambo mengi yahusuyo mkabala wa taifa letu nikaona kuna haja ya kila mtu kuwa mchambuzi wa masuala ya siasa, ahata kama haupendi siasa, ni lazima uwe mchambuzi, kwa sababu habari nyingi zinapotoshwa na kupikwa, iwe ndani au nje, nimejua kwamba ninahitaji kuwa mfuatiliaji kwa muda ili nijue yupi ni mwanasiasa kilimo na yupi ni wanasiasa uchwara.
Katika hili bado siwaamini wanasiasa wengi waliojisajili kama wanasiasa, mimi nawaona kama wapambanaji na njaa zao kwa kukimbia jembe letu.
Sasa hivi kila mtu anaweza akaitisha mkutano wa hadhara kwa kigezo cha kuongelea siasa, sasa hivi kila mtu anaweza kuwaita waandishi wa habari na kuanza kuongea mambo anayoyaita ya nchi na siasa, mimi kama mkazi wa kijijini bado nashindwa kuelewa nimsikilize nani na nimpuuze yupi.
Wapo wanaoongelea mambo ya kutisha ambayo tangu nikiijua nchii hii haijawahi kuingia katika mambo hayo, wananitia hofu tu, nadhani tuwe na vyanzo vyetu vya habari makini na visajiliwe ili tuweze kuvishtaki kwa kutukosesha amani kwa taarifa zao.
Najua kwamba uwazi unahitajika, hili halina mjadala, wala halipingwi. Najua kwamba habari ni haki yangu kuipata, hii imo hata katika Katiba yetu. Najua kwamba kuelimishwa ni haki yangu, labda kama nitakuwa sitaki kupata elimu, lakini swali ni kwamba ni habari gani napewa na elimu gani ya msingi kabisa naipata kupitia vyombo vya habari, tena vilivyosajiliwa kisheria na vile ambavyo vipo kwa ajili ya kuvamia habari bila kupata usajili?
Naomba niache wosia kwa wanangu wote kwamba tuendako kuna giza kama sheria hazitatamalaki kwa kuwadhibiti wanasiasa na wanahabari ambao kazi kubwa ni kuzusha maneno yanayotufanya tuishi kwa mashaka kila siku.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.