Huwa napata taabu sana ninapojaribu kufananisha mambo yetu na yenu. Huenda ni maendeleo ama ni mimi kupitwa na kitu kinachoitwa ‘kwenda na wakati’. Kwa hakika sijisikii vizuri lakini sina budi kukubali matokeo.

Leo nimeanza na kitu kilichokuwa ni muhimu sana enzi zetu — jembe. Ilikuwa fahari kuyaona majembe ndani ya nyumba zetu yakiwa yamehifadhiwa katika kona ya nyumba kuonesha ushujaa wa ukulima wa nyumba bora.

Pamoja na maendeleo kuwapo na kuja kwa haraka enzi hizo, bado majembe ya kisasa kama ya kuvutwa na ng’ombe yalikuwa na maana sana na majembe ya kuvutwa kwa trekta yalikuwa na maana sana katika jamii.

Haya ndiyo yaliyokuwa maisha ya kilimo kwanza cha kweli, kilimo cha kufa na kupona, kilimo cha Ujamaa na Kujitegemea, kilimo cha maendeleo, kilimo cha kuendeleza vyama vya ushirika na kilimo cha kuendeleza nchi yetu.

Ni kwa jeuri hiyo ndiyo maana tuliweza kuhimili vita ya kumng’oa nduli Idi Amin mwaka 1978. Tulimpiga kwa sababu kwanza hatukuwa na tatizo la njaa, pili tulikuwa na uwezo wa fedha wa kuweza kununua silaha, tatu tulikuwa na uzalendo uliotokana na ushirika na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Najua yote haya tuliyafanya kutokana na wakati na juhudi zetu, lakini jambo muhimu zaidi ni mtazamo wa viongozi juu ya vipaumbele tulivyokuwa navyo wakati huo — viongozi hawakuona bora maendeleo bali maendeleo bora.

Sasa ni miongo kadhaa imepita, imepita na mambo yake, hakuna majembe tena wala shughuli yake muhimu, shughuli ya kilimo cha kufa na kupona. Leo kazi kubwa ya majembe ni kama sehemu ya mahari ya kuoa mwanamke mjini. Leo watu wanamiliki televisheni kubwa za kisasa na siyo majembe tena, wanamiliki kama vitegauchumi vyao vya kuonesha mipira kwa kiingilio na picha za ngono mchana wa jua kali, tena kwa vijana na watoto ambao hawaendi shule wala shambani. Haya ndiyo maendeleo.

Leo watu wanamiliki magari ya kifahari kwa ajili ya kuendeshea maisha yao kwa kukodisha kwa ajili ya harusi, misiba na sherehe na siyo matrekta ya kilimo tena. Haya ndiyo maendeleo tunayotaka ambayo nguvu kazi tumeilimbikiza huko.

Leo tumeacha ushirika wa kilimo, ufugaji, ushonaji, uvuvi na badala yake tumeanzisha ushirika wa makundi ya starehe kama vogodoro, usutaji na kazi rahisi za midomo badala ya jembe, ushirika ambao unafanya mambo yasiyo na tija kwa mwananchi wa kawaida au Taifa kwa ujumla wake. Tumeamua kuwekeza katika shughuli nyepesi badala ya shughuli ngumu ili kujikomboa kama mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Leo vijana wengi wenye nguvu ndiyo wachuuzi wa pipi barabarani, ndiyo wachuuzi wa kuuza maeneo ya wazazi wao, ndiyo wachuuzi wa kutoa ushauri wa kisheria kwa watu badala ya kutumia muda huo kufanya kazi nzito za viwandani, mashambani, ufugaji na uvuvi na kadhalika ili kuingiza kipato kikubwa.

Tumeweza kuzalisha idadi kubwa ya vijana wenye nguvu kuwa madalali, waganga feki wa kienyeji, matapeli, wanasiasa waongo, wachungaji matapeli, wezi, majambazi, majangili, malaya na hatimaye wapotoshaji wa maadili na utamaduni wa Mtanzania wa kweli.

Leo vijana wanamiliki simu zaidi ya moja, tena simu za mamilioni. Wamekiacha kilimo kwa kuwa wanatumia simu kupata riziki yao, wanatumia simu kutapeli, kucheza michezo (games) kwa mashindano na kuwa kamari badala ya kulima.

Tunapoteza nguvu kazi kwa kigezo cha maendeleo.

Watu wanakaa vijiweni na kutafuta namna rahisi ya maisha kwa kutumia mawasiliano. Wananchi wanaumia kwa matumizi mabaya ya simu, lo! Maradhi yameongezeka kwa sababu watu hawajishughulishi kama zamani. Tumeona bora maendeleo na siyo maendeleo bora. Haya ni matokeo ya viongozi kutoa vipaumbele bila kuzingatia maadili na utamaduni.

Leo tunatafuta ajira nyepesi kwa maisha mepesi, hatumiliki majembe matatu bali tunamiliki simu tatu, hatuna viwanda wala mashamba, hata ngalawa za uvuvi wala majosho ya mifugo, kila mtu kawa dalali.

Tumeuza mashamba, viwanda, nyumba zetu na sasa tunauza utu wetu kwa kukosa kuamua kutumia nguvu zetu katika kujikomboa. Huwa nafikiria yale ya 1978 yakirudi tutawezaje kupambana nayo!

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.