Wanangu nianze kwa kuwapa kongole kwa kazi za kuliendeleza taifa ambalo linamkosi mkubwa na jambo linaloitwa maendeleo, linamkosi kwa sababu kwa kipindi cha miaka hamsini ya tangu kuzaliwa kwake bado linachechemea, kwa ufupi ndio kwanza linaanza kusimama dede ili lipige hatua ya kwanza lakini dalili zote za kushindwa zinajidhihirisha.

Nimeaamua kuwatumia salamu hizi kwa sababu wakati tukizaliwa tuliweza kutambaa vizuri tena kwa muda mzuri wa makuzi ya mtoto, tukaanza kusimamia vitu meza, ukuta, viti na kusogea taratibu katika vitu vingine, mawazo ya wazazi ilikuwa muda mfupi mbele tungeweza kutembea bila kujishikilia mahali na hatimaye kukimbia.

 

Wazazi wetu wanasema tulizaliwa pamoja na wenzetu wengi, kizazi chetu kilibarikiwa wengine walizalizawa Kenya muda mfupi baada ya sisi kuzaliwa, lakini pia wapo waliozaliwa Ughaibuni, leo wenzetu siyo tu wameaanza kutembea lakini pia wanakimbia na kujitegemea.

 

Wanangu nawaandikia barua hii kuwapongeza kwa maradhi ambayo mmepigana nayo kwa muda mrefu, maradhi ya udumivu kama siyo kwashakoo ambayo labda ingeweza kupoteza uhai wenu lakini hadi leo mmeweza kushindana nayo nguvu huku mkitapatapa.

 

Nawapongeza sana kwa sababu pamoja na maradhi yaliyopo na sisi bado tupo na tunaendelea kukataa kutumia dawa ya vitamin ambayo tuliacha wakati wa kuzaliwa kwetu na kukua kwetu sanjari na wenzetu ambao waliamua kutumia ili wakue vizuri.

 

Wanangu katika kipindi chote cha maradhi yenu mmekuwa mstari wa mbele kupingana na watabibu juu ya dawa ambazo mnapaswa kuzitumia ambazo baadhi yake mlikataa mlivyoanza kutambaa mkidai bora mtumie dawa za asili na maombi ili muweze kupona.

 

Nawapongeza kwa moyo huo wa ushujaa ambao mnao pamoja na kuona mimba zingine na watoto wakizaliwa miaka kadhaa  baada yenu wakitumia dawa na kuwa na afya njema na wanakua na kuanza kutambaa, kutembea na kukimbia huku wakiwaacha nyie bado mkiendelea kusota chini kama vile walemavu msioweza kutembea tena.

 

Wakati tukizaliwa sisi tulipata chanjo ya Ujamaa na Kujitegemea ikifuatiwa na nyongeza ya dawa ya vitamin ya Azimio la Arusha na tulipaswa kuendelea kutumia dawa hiyo kwa muda maalumu ili tuweze kuwa na afya njema kwa kipindi chote cha maisha yetu.

 

Tuliamua kuacha dawa zote ili tuweze kutumia dawa mbadala tukiamini zitatusaidia kuliko hizi dawa za kweli, tukaamua kutumia dawa za miti shamba, dawa zisizo na vipimo maalumu, zenye madaktari ambao ni waganga wababaishaji, ambao dakika za mwisho wakiona hali yenu kiafya inazidi kudorora wanaweza wakatukimbia  na tusipate msaada zaidi ya kuingia kaburini.

 

Wanangu naandika barua hii leo nikiwa na mambo mengi kichwani ambayo yanakinzana na ukweli wa maisha ambayo kama siyo watanganyika basi ni watanzania walipaswa kuwa nayo hivi sasa tofauti na hali halisi ilivyo.

 

Nchi yetu wakati ikipata uhuru ilikuwa ikifanana sana kiuchumi na mataifa mengi ya afrika na nje ya afrika, baadhi ya mataifa hayo hivi leo yanajitegemea kiuchumi na yanaweza kutoa misaada kwa mataifa maskini mengi likiwamo na taifa letu.

 

Hebu tuziangalie nchi kama Afrika Kusini, Botswana, Kenya, Rwanda, Libya na zinginezo za afrika, hebu tuziangalie nchi kama Brazil, Korea Kusini na Korea Kaskazini, China, Cuba, Mexico, Singapore na zinginezo ambazo miaka ya 1961 hatukupishana sana kiuchumi na zingine zilikuwa bado zinatawaliwa na wakoloni.

Wanangu mambo yote haya ninayoyazungumza leo narejea katika utawala wa mataifa hayo na utawala wa taifa letu, nafanya tathimini ya uchumi wao na uchumi wa taifa letu na hatimaye najiuliza tupo wapi na tulitoka wapi na wenzetu.

 

Haya maswali wanangu kila anayesoma waraka huu ajiulize anategemea nini kulifanyia taifa hili lenye ugonjwa mbaya wa kudumaa kiafya kutokana na kukataa dawa za kitaalamu kutoka kwa wataalamu na kuamua kutumia njia za mkato na zenye nguvu za giza kuweza kukabiliana na maradhi tuliyonayo.

 

Sababu mojawapo ninayoiona katika fikra zangu za kizee ni kwa vijana kukataa kufanya kazi za maendeleo na kukaa vijiweni kuanzisha mijadala ya siasa badala ya kufanya kazi, sababu ya pili ni kwamba tuna wataalamu ambao wengi wao hawaijui taaluma hiyo wanayoifanyia kazi na matokeo yake tunapata dozi ambayo si sahihi kwa umri wetu.

 

Wanangu, sisi ni maskini sana na hasa kama umewaona wenzetu ambao tulianaza nao kusimama dede, ni maskini ambao hatuwezi japo kupata huduma bora za kijamii kama matibabu, miundo mbinu, mawasiliano, umeme, elimu na makazi.

 

Wanangu tumelogwa kwa imani kwamba tunahitaji mazingaombwe tufike pale ambapo wengine wamefika kwa kufanya kazi kwa bidii sana ili wale matunda ya uhuru wao, tumebaki kulalamika na kumtafuta mchawi kutoka kwa wenzetu wa mataifa yaliyoendelea.

 

Haya ndio matokeo ya kuacha dawa yetu ya ujamaa na kujitegemea na chanjo muhimu ya azimio la arusha, wapo watakaokataa kwa imani kwamba dawa hizo zilipitwa na wakati lakini wapo watakaokubaliana nami kuwa huo ndio ulikuwa mzizi wa fitina katika kukabiliana na matatizo na maradhi ya umaskini tuliyonayo leo.

 

Wanangu wakati tukiingia katika vita ya Uganda siku chache baada ya kupata dozi ya azimio la arusha  tulikuwa na amana ya kuweza kuiendesha nchi hii kwa miaka kumi na moja, ndoto za kutumia amana hiyo zilifutwa na nduli idi amini, lakini naamini tungeweza kutawanya barabara nzuri  kwa ajili ya kusafirisha mazao na waanchi, tungekuwa na hospitali, shule nzuri nakadhalika.

 

Wanangu ni ujinga ule ambao ulitutawala katika vichwa vyetu, ujinga wa kuamini katika siasa ya ujamaa na kujitegemea, ujinga wa kuamini katika kufanya kazi na kulima na ujinga wa kuamini kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa hili na kwamba fedha si msingi wa maendeleo.

 

Mpaka leo wanangu naamini katika kudumisha  fikra za mwenyekiti wa chama, naamini katika kilimo na viwanda, naamini katika kumiliki njia kuu za uchumi, naamini katika siasa ni kilimo, naamini katika kumiliki mali ya taifa kwa pamoja, naamini katika kufanya kazi pamoja ni muumini wa siasa ya zamani ambayo najua ingetufikisha mahali sisi wazee tungekuwa na maisha ya kujivunia kwa kizazi hiki.

 

Wanangu mnapaswa kujiuliza mmepitiwa wapi hadi laana hii iwakumbe na ituletee umaskini uliokithiri, tushindwe kuwa na amana ya kutosha, tushindwe kuboresha huduma za jamii, tushindwe kujitegemea na badala yake tuwe tunakopa kila siku, tushindwe kumiliki mashamba na viwanda vyetu wakati ongezeko la vijana ni kubwa kuliko enzi zetu.

 

Tutafakari mfumo wa siasa tulionao, mwenendo wa uchumi, na mstakabali wa taifa katika siku za usoni na tujiuluize baada ya kujitawala na kusimama dede tunataka turudi kuwa watoto wa kubebwa miaka yote?

 

Tunashindwaje kusema yatosha dawa za kienyeji sasa basi tunahitaji dawa za wataalamu hata kama ni chungu kama shubili lakini tunywe na tuweze kusimama na kukimbia ili wazaliwao nyuma watukute kaka zao tukiwa mbele na tuwasaidie.

 

Wanangu labda mnishone mdomo lakini kwangu mimi fikra za Mwenyekiti wetu wa TANU kamwe sitaziacha na kuzisahau, nitasema hadi mauti yanifike Zidumu Fikra za Mwenyekiti wa TANU, Kidumu Chama Cha TANU na Lidumu Azimio la Arusha kama bado lipo.

 

Laiti kama ingelikuwa bado kama wakati ule na dawa hizi naamini leo tungekuwa na wadaiwa wengi sana.

 

TANU oyee

Wasalaamu

Mzee Zuzu,

Kipatimo