Mwaka 1932 nilianza darasa la kwanza katika Shule ya Kati Bulongwa. Nilikuwa na miaka kumi na nne. Nilipata nafasi hiyo baada ya nenda rudi ya miaka miwili, mkono ulikuwa haufiki sikioni.

Namkumbuka Mwalimu Schreger, Mwalimu Sanga ambaye baadaye alihamia Tandala Middle School ambako aliwafundisha wengi akikaribia kustaafu kama akina Tunginie na Tuntemeke Sanga.

 

Wakati huo, suala la kwenda shule lilikuwa ni jambo geni katika jamii yetu. Wapo walioamua kuachana nalo kutokana na sababu mbalimbali, baadhi yao ni kuingia katika maisha ya ndoa mapema ama kuajiriwa kama manamba katika mashamba makubwa ya chai, tumbaku au katika migodi huko Zambia na Rhodesia.

 

Mimi nilikuwa kama prince kutoka katika familia ya Kichifu, Chifu Nsongoma (1), hivyo ilikuwa ni kashfa kwenda kufanya kazi ya kitumwa, japokuwa nilikuwa napenda sana wenzangu wanavyorudi na vitu vya thamani kama visu vya mkunjo, gramphones, na magari kama yale mnayoyaona katika sinema zenu za vituko vya sasa ya ‘Gods Must be Crazy’,  Land Rover 109 series I short chasis.

 

Mzazi wangu, Chifu Nsongoma alihakikisha naenda kusoma ili nikija kurithi uchifu niwe japo na akili ya kulinda himaya yake, niwe na uwezo wa kujua nifanye nini ili watu wake waishi kwa amani na niweze kutatua migogoro kama ya ardhi, ndoa, ugomvi na mengineyo muhimu katika jamii iliyostaarabika.

 

Nilifanikiwa kufika darasa la nne kwa nguvu ya chifu na mimi mwenyewe kujituma kwa bidii katika masomo, nilipendwa na walimu wangu, nilipendwa na jamii inayonizunguka na tulipokuwa shule tulipendana sana na wenzangu. Huo ndiyo uliokuwa ustaarabu wa wakati huo wa zamani. Nilifanya vizuri katika mitihani ya Cambridge lakini chifu hakutaka niende Makerere kwa kuwa hali yake ya afya ilikuwa inadorora.

 

Miaka michache baadaye, alipoteza maisha nikashika mikoba kwa muda kabla Julius Nyerere hajafutilia mbali utawala wa kichifu nchini, falme nyingi zilipoteza nguvu na kuingia katika utawala mmoja wa siasa nchi nzima.

 

Barua yangu ya leo sikusudii kueleza historia lakini nimefanya hivyo kwa makusudi, ili niweze kueleza vizuri kile ambacho kinanikwaza katika akili yangu ya kizamani. Huu mtindo wa elimu uliopo sasa, sisi tulisoma shule ambazo hazikuwa zetu, zilikuwa za wakoloni ambao walitutawala lakini zilikuwa zinatoa elimu ambayo kamwe leo huwezi kuipata katika shule yoyote ya serikali au binafsi.

 

Hivi sasa hakuna shule yenye sifa ya kuitwa shule, hakuna walimu wa kutosha, hakuna madawati ya kutosha, hakuna vitendea kazi, hakuna chakula, hakuna maktaba, hakuna maabara, hakuna sheria za shule, hakuna nidhamu. Badala yake kuna majengo yasiyo na sifa za madarasa, kuna matofali ya kukalia badala ya viti, kuna walimu wachache wanaoshinda wizarani kuulizia mitaala mipya na mishahara yao, kuna maktaba ya vitabu vya hadithi na si vya elimu, kuna sheria mikononi kwa wanafunzi dhidi ya walimu na mwisho hakuna upendo.

 

Wajibu wa serikali katika kusimamia suala la elimu limeyumba kwa sababu nyingi ikiwamo nguvu ya wazazi katika kusimamia shule hizo na watoto wao, kushindwa kuimarisha miundombinu muhimu ya elimu ikiwamo kuandaa walimu bora wa kwenda kuwafundisha wanafunzi ambao tunategemea wawe walimu wazuri siku zijazo, na mwisho serikali kuwachukulia walimu kama chaguo la karibia na mwisho kwenda katika vyuo vya ualimu.

 

Sifa ya mwalimu ni kubwa sana, na ni kazi ya heshima sana katika mataifa yote yaliyoendelea. Taifa haliwezi kustaarabika na kusonga mbele bila nguvu ya mwalimu, walimu ndiyo wanaowafundisha hao mnaowaita viongozi, madaktari, mainjinia, marubani, wahasibu na kadhalika. Sioni mantiki ya hao waliofundishwa na walimu wawadharau tena walimu wao.

 

Wakati wetu kuwa mwalimu ilikuwa ni sifa na heshima kubwa sana. Mwalimu alipendwa na aliheshimiwa na serikali, wazazi, wanafunzi na jamii inayowazunguka, mwalimu alipewa msaada kama ndugu wakati wowote na mahali popote, mwalimu aliweza kulala na kula nyumba yoyote yenye mwanafunzi na hata isiyo na mwanafunzi, alijisikia fahari kila anapoonana na mtu njiani kutokana na sifa ya kuwa mwalimu.

 

Hivi sasa naumiza kichwa kujaribu kufikiria mustakabali wa sekta ya elimu kwa kuwaangalia wadau mbalimbali wa elimu ikiwamo serikali yenyewe, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla.

 

Naiangalia elimu ya kambo, elimu ya mtawala kikoloni, elimu yetu na faida kwa kizazi hiki, naangalia mateso tuliyopata sisi umbali wa shule, mathalan mimi nilikuwa natembea maili nane kila siku kwenda na kurudi shule, Julius zilikuwa maili kumi na nne kutoka Mwitongo hadi shuleni kwake. Humo njiani tulionana na wazazi mbalimbali ambao ilibidi tuwapokee mizigo kwa kuwa ndiyo uliokuwa utaratibu wa mafunzo.

 

Hivi leo tunawafundisha nini wanetu? Tunawajengea nini wanzetu kwa faida ya wengi? Wanafundishwa nini na jamii? Wanatuonaje walimu? Mitaala yao ikoje? Wasimulie nini siku zijazo ili wawe mfano kwa nani siku zijazo? Wamsaidie nani kwa elimu yao?

 

Haya ni maswali mengi yanayonikoroga. Tuendelee kujadili wanakaya wenzangu. Kama una maoni, chonde nitwangie.

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

Mtanzania Mwenzangu,

Yahoo.com/hotmail.com/excite.com/www.http,

Tanzania Yetu.