Naipenda sana Tanganyika ambayo mwaka 1964 nasikia mliamua kuibadilisha jina na kuiita Tanzania. Nilianza kuijua Tanzania wakati huo na sababu kubwa iliyonifanya niijue vizuri ni wito uliotolewa na wale vijana wawili ambao sasa wametangulia mbele ya haki – Nyerere na Karume.
Suala la kuifanya Tanganyika kuwa Tanzania lilitokana na kuunganisha visiwa vya Zanzibar na Tanganyika, lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na kuongeza umoja baina ya mataifa yaliyo karibu karibu.
Taratibu majadiliano yalianza baina ya viongozi wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta na wa Uganda Milton Obote, lakini hayakufanikiwa kutokana na sababu ambazo leo ama Watanganyika wanazitaja au Wazanzibari wanazitaka.
Wanangu, mimi si mwanasiasa na hata kama nikitaka kuwa mwanasiasa siwezi kuhimili siasa zenu za kuanikana mambo binafsi ya familia na maumbile badala ya kuanika masuala ya kitaifa zaidi. Siwezi siasa zenu kwa sababu sina nguvu ya kupigana na sina fedha za kuhonga ili nichaguliwe, na siwezi kwa sababu sina uwezo wa kuwa mnafiki kwa wananchi.
Wanangu, siasa ni uwezo wa kuwashawishi watu kufanya jambo la kijamii lenye lengo la kujiletea maendeleo katika jamii husika. Siasa si kudanganya, siasa si ajira ya kuwafanya watu wengine waishi kwa mishahara ya kukaa majukwaani na kupiga porojo. Siasa ni sera na kinachotakiwa ni utekelezaji baada ya makubaliano.
Wanangu, leo nimeandika waraka huu kwa sababu nyingi. Mosi, ni hii dhana iliyopo miongoni mwetu kwamba Muungano ni hoja ya watu wawili isiyo na tija. Naweza nikakubaliana na hilo kama kizazi chenu kinatafakari hivyo na kwamba walioamua hoja hiyo labda walitafakari kizamani.
Sina hakika kama barua zangu huwa mnazihifadhi, lakini kwa kufanya kumbukumbu ni vema mkarejea baadhi ya maandiko yangu ninayoyaandika kutokana na umri nilionao na mawazo ya ‘kipumbavu’, mawazo ya kizamani, mawazo ya kizuzu ambayo labda yana tija kwa kizazi kijacho.
Si kweli kwamba kila kisemwacho kina nguvu katika jamii, na si kweli kwamba kila kinachotolewa kama hoja lazima kikubaliwe, lakini tunatakiwa kufanya tafakari ya kina kujua kinachotaka kujiliwa katika siku za usoni, mathalani suala la kuuvunja Muungano au kutouvunja.
Nayasikia mengi sana hasa kutoka Visiwani. Ni kama vile nanong’onezwa na marafiki zangu. Haya ni baadhi ya mawazo yao ambayo nitayanukuu kama yalivyo bila kuongeza chumvi wala kurekebisha herufi.
Nanukuu “Sadakta! hatutaki usanii. Kilichotupeleka katika Katiba mpya si chengine, isipokuwa ni Muungano. Basi kama wao ni wakweli walete mjadala wa Muungano hadharani na siyo Katiba. Kwanza tuoneshwe mkataba wa Muungano baadaye mengine yatafuata.
Hayo maneno tushayazowea, huo ni ujanja tu wa Watanganyika na kwa vile huyo Warioba naye ni Mtanganyika, hatowacha kutetea Watanganyika wenzake kwani si alikuwemo kwenye system muda mrefu, kafanya nini zaidi ya kuizamisha na kuidhalilisha Znz, hatuwezi kumuamini hata aseme nini?
Naendelea kunukuu kama ifuatavyo; “Mujuwe naye pia huyo ni miongoni wa wanasiasa wa Kitanganyika wanaotambua ukweli wote juu ya Muungano. Hapo ni uzushi mtupu. Hakuna ukweli wala uwazi juu ya taratibu za kamati katika kuyahukumu hayo, kwa mfano watu wangapi watatoa maoni na kwa vigezo vipi, wangapi wakisema serikali moja, mbili, tatu, na wasiotaka Muungano, Tume itahukumu kwa misingi ipi, hizo ni sheree, tutakuwa tunarudia-rudia haya mambo kila ujao, dawa ni kuulizwa wa Zanzibar wanautaka/hawautaki, basi. Vyenginevyo ni kutaka kughalalisha gharamu kwa vyovyote viwanyo.
…Na hilo, litaleta malaumiano ya kudumu kama yalivyo kwa huu Muungano uliopo, kwanini hatuwi wakweli? Mimi naona kabla watu hawajaulizwa kama wana utaka au hawautaki kwa kura ya maoni, la muhimu watu wajipange kikamilifu sio jambo la kukurupuka. Pili, bado kuna watu wengi hawana vitambulisho vya Uzanzibari ambao wana haki ya kuwa navyo, badala yake wageni wengi ndiyo walionavyo hivyo vitambulisho.
Mimi wazo langu watu wende wakatoe mawaidha au maoni yao ya Muungano wa mkataba kwa kura ya maoni, ndiyo itakuwa changa la macho. Those who know don’t talk and those who talk don’t know. Sasa hapo kazi.
Ondoa wasiwasi, watu wako tayari, watu wamejipanga, kila Mzanzibari yuko tayari, usibabaike na wapiga filimbi wengi, hebu leo hii watupe hiyo nafasi, watafufuka waliokufa acha waliolala, ondoa wasiwasi, tulio-navyo vitambulisho tunatosha kuamua hatima ya Zanzibar dhidi ya Muungano dhalimu. Tumejiandaa, tumejipanga na tuko tayari. Vita ni endapo maoni yetu yatapuuzwa. Hapo hapatatosha hadi kitaeleweka. We are serious about that, not joking. JAMHURI YA WATU WA ZNZ KWANZA. Mwisho wa kunukuu baadhi ya maoni ya wanaoninong’oneza.
Haya ni mawazo yanayotolewa na wakazi wa Tanzania ambao baadhi wako Zanzibar. Wanajaribu kuonyesha hisia zao za kutotaka Muungano na kwamba Muungano huu tulionao unalazimishwa na watu wa Bara. Suala lililopo hapa ni siasa, siasa uchwara na si siasa makini.
Kuna wakati Nyerere aliwahi kuulizwa swali na mwandishi mmoja wa habari pale ilipokuwa hoteli yetu ya Kilimanjaro. Aliulizwa iwapo Wazanzibari wakiamua kuuvunja Muungano na Watanganyika kung’ang’ania itakuwaje? Alijibu kwa ufupi sana akisema kama tutaamua mauaji ya halaiki kama yale ya Burundi yeye hawezi kutuzuia isipokuwa ana wajibu kama rais wa kwanza wa taifa hili kutueleza yatakayotokea, akamaliza akisema “watch out.”
Sasa nilianza kwa kusema siasa safi ambayo mimi ningeweza kuifanya ni ile ya kutotumia nguvu, pesa wala unafiki. Ningekuwa mkweli daima kwa jambo lolote ambalo ni la msingi kwa vizazi vijavyo, suala hili la Muungano ningekuwa mkali kuliko Nyerere na hapo ndipo ningeonekana mwanasiasa wa kweli.
Naomba wanangu mjiulize hizi sura zinazojiita wanasiasa ni wakweli? Wanayafanya kwa dhati wanayoyazungumza? Wanayatetea kwa uthabiti? Wana lengo gani na ajira ya siasa? Tutafika wapi? Yapi wanayoyakemea kwa dhati? Naomba majibu.
Wasaalam,
Mzee Zuzu.
Kipatimo.