Nianze kwa kuwashukuru sana wazazi wangu walionikanya wakati naoa kwamba maisha ya ndoa ni kama glasi ndani ya kabati, ipo siku lazima kabati litayumba na glasi zitagongana, na ikitokea hivyo katika maisha yangu ya ndoa lazima nitumie kuta nne za chumbani kwangu kumaliza kelele zetu za glasi, ugomvi na sintofahamu yoyote ile.

Nayafananisha maisha ya ndoa katika kujenga nyumba ya familia na taifa lolote lenye kutaka kujitegemea na kuwa huru, liweze kufanya mambo yake katika kukabili umaskini na kuwaletea wananchi wake maendeleo, wananchi ambao ni kama watoto katika familia fulani wanaosubiri kumsikia baba akitoa tamko lolote la maana katika familia.

Leo kwa bahati mbaya, kichaa cha kukumbuka tulikotoka kimenipanda baada ya kuona Taifa letu linazidi kuwa kichekesho katika jamii nyingine ya mataifa huru na yanayotaka kufanya maendeleo, ni Taifa ambalo haliwezi kutumia kuta zake nne za ndoa kumaliza matatizo ama furaha ya ndoa, kuzungumzia siri za familia na badala yake tunatumia baraza na mitaani kutangaza ugomvi wetu unaowapa faida wapita njia na wageni mtaani kwetu.

Zamani tulipata kusema nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi, hatukuwakataa wafanyabiashara lakini tuliwadhibiti wafanyabiashara kwa kuwa na vikundi vyetu vya kijiji kuweza kumiliki mali iwe yetu sote. Tulifanya hivyo ili tuweze kusonga mbele kimaendeleo, lilikuwa lengo maalum kuweza kushika njia zote za uchumi na kuwa wasiri ndani ya ndoa yetu ya taifa.

Tanzania ya sasa kama Taifa tumekuwa malimbukeni wa kuropoka siri zetu bila kujua nani anasikiliza kwa faida gani, Tanzania tumepoteza uzalendo wa kutunza siri zetu tuweze kufanya jambo letu kama Taifa na kujivunia mbele ya mataifa mengine liwe la kimaendeleo ama la kutafuta maendeleo.

Kuna mengi ya kujifunza katika hili kutoka kwa wenzetu, mataifa makubwa ambayo yakitangaza kitu maana yake wanacho mkononi, sisi tunatamka kitu tusichokuwa nacho, tunashirikiana na majirani kutafuta hicho ambacho tumetangaza tunacho. Majirani wanashiriki kutupatia ushauri jinsi ya kukipata na wanatumia fursa hiyo kutugombanisha wenye mali ambayo haijapatikana.

Mifano ipo mingi, lakini nitoe michache itakayoswihi na ile ya wakati wetu wa Tanzania ya uzalendo. Kuna madini, tumetoka nje ya nyumba yetu na kupayuka kuwa tuna dhahabu nchi nzima, mpayukaji hakuzingatia anamweleza nani.

 

Matokeo yake dhahabu yetu imechimbwa na watu wa nje na manufaa kama Watanzania hatuna, tumebakia kupigania haki ya kodi tu, wapi tunakwenda! Hivi tulikuwa na sababu gani ya kutovumilia hadi tuwe na uwezo wa kuchimba wenyewe na ikatusaidia kama Taifa?

Mbona hatukujiuliza tuliwezaje kuchimba wenyewe almasi huko Mwadui na tukajenga viwanda vyetu wenyewe na tukaweza kuuza nje bila kutegemea jirani yeyote katika mchakato huo? Hivi baada ya siri ya muda mrefu tumeishia wapi katika almasi yetu, au huo mdomomdomo umetuponza katika almasi pia?

Majirani wanatugombanisha baada ya sisi wenyewe kuweka siri zetu nje, wanatumia fursa hiyo kutujua, kutufahamu, kututambua na kwa ujumla kutusasambua kiakili, kimwili na kiroho. Leo tumetangaza tunayo gesi nyingi, tumetangaza bila kujua gesi hiyo ipo sehemu gani huko kusini, wageni wamekuja wametuonesha tunapoweza kutolea. Kwa kutumia akili ndogo na umaskini wetu wameweza kutugombanisha, tumevua uzalendo tumerudi katika dhana ya umimi.

Tunawategemea watu wa nje wawe washauri wa mali zetu, tumekuwa vilema wa akili na maungo kushindwa kuhimili maliasili tuliyopewa na Mwenyezi Mungu katika ardhi yetu. Wageni wamegeuza nchi yetu kuwa shamba la bibi, shamba la kuvuna na kuondoka bila kuacha japo shukurani ya mwenye shamba. Tumekubali kuwa walinzi wa ngedere hadi mazao yakomae na kuwaacha wenye mikono ya kuvuna wafanye kazi hiyo.

Tujiulize ni lini tumepata siri za mataifa mengine kama China na utengenezaji wa nyuklia, Libya na uwezo wa kujitegemea wenyewe hadi ndoa yao ilipoingia dosari ya kuanza kuropokaropoka maisha yao ya ndani na wapita njia kupata fursa ya kutoa ushauri na kuiingilia ndoa hadi ikavunjika na kuacha mali mikononi mwa wambeya?

Naamini katika sera ya kujiwezesha na kutowezeshwa, sisi si vilema na mataahira tunaoshindwa kuhimili utajiri tulionao. Siamini katika kutoa siri zetu za kimaendeleo na kutoonewa wivu na mataifa mengine, naogopa wanaoweza kukurupuka na kusema chochote bila kuwa wazalendo na kujua athari zake, na wasiwasi na  Tanzania na maendeleo ya mdomo wa uswahilini, haitawezakana.

Tujifunze kuwa wasiri na kuwa na moyo wa kutekeleza kwa kujitegemea, hakuna haja ya kujivunia umri wa Uhuru kama hatuko huru kifikra na kujitegemea. Tanzania  niliyoitarajia leo ni ile ya kuwakopesha wote  tuliowasaidia kupata Uhuru wao na si sisi kuwa tegemezi kwao, angalau tuwe na siri na aibu kidogo ya umaskini wetu.

Tanzania ya uzalendo wetu naamini tungekuwa meza moja na China, Afrika Kusini na nchi zote ambazo tumekuwa wote maskini kwa wakati mmoja miaka ya 1960. Chonde, tuache umbeya na mdomomdomo, si kila jambo ni la kuzungumza ili tuilinde ndoa yetu iwe imara na ndipo tutakapokuwa Taifa madhubuti na lenye maendeleo.

 

Wasaalamu,  
Mzee Zuzu, 
Kipatimo.