Nianze na salamu. Najua kwamba tumeanza mwezi wa mwisho wa mwaka huu, ni vema tukatumia fursa hii kwanza kumshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa tulipo.
Pili, kama kampuni ya gazeti, tuna kila sababu ya kuwashukuru wasomaji wetu kwa kutuunga mkono, kwa kuwa nasi kwa kipindi chote hiki. Hata hivyo lazima nikiri kuwa wapo ambao watasema tumewakwaza kwa kutowapa kile ambacho walikitarajia.
Sisi ni gazeti makini, kwa taarifa makini na wakati makini, kwa lolote lile naomba mtuwie radhi na tuendelee kuwa pamoja siku zijazo.
Tumeandika mambo mengi na mengine hayajawafurahisha wenye hisa na mengine yamewafanya watu wafungue masikio ya ukurasa mpya wa taarifa mpya.
Lengo la gazeti hili ni kuwafikishia Watanzania taarifa kwa ajili ya maendeleo yao na kutoa taarifa wapi tumekwama na tunatakiwa kwenda wapi, lengo si kuwa kijiwe cha umbeya au kuanzisha jambo la umbeya ili tukubalike.
Daima tumekuwa makini na taarifa zetu kwa watu makini, tunaamini kila asomaye gazeti hili ni mtu makini.
Leo nimeamua kuzungumzia sheria, unaweza kujiuliza kwanini sheria? Nimeamua kuandika waraka maalumu kuonyesha jinsi ambavyo tumekuwa tukiishi kwa mazoea ya kupindisha kitu kinachoitwa sheria.
Jambo hili hufanyika kwa muda mrefu kiasi kwamba sheria inapotea na mazoea yanabaki kuwa sheria.
Tumeona mambo mengi yakifanyika na kutukumbusha sheria na jinsi ambavyo hatukuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.
Niulize, nani alikuwa anajua kwamba ni marufuku kwa mujibu wa sheria kupiga honi eneo la hospitali au mahakamani? Nani alikuwa anajua kuwa dhamana ni haki ya kikatiba na ni sheria mtu kuipata kwa makosa ambayo yamebainishwa kisheria?
Misingi ya sheria ilikuwepo tangu taifa hili likipata uhuru na kuwa ni taifa huru lenye kujiwekea sheria zake lenyewe, lakini pia ni sheria zenye kanuni zake ambazo zinapaswa kutekelezwa na wananchi ili tuishi maisha yanayokuwa katika mfumo wa usawa na haki.
Taifa lisilo na sheria zake na likatumia moja kwa moja sheria za taifa jingine, hilo ni taifa mfu, Tanzania si taifa mfu, bali sheria zilikuwa likizo kwa muda na sasa zinaanza kukumbushwa kwa wananchi ili wazifuate.
Sheria zipo nyingi na kanuni pia, lakini utaratibu pia unaweza ukawa sehemu ya sheria, kwa maana ya wengi wangependa kitu gani.
Mathalani suala la usafi, muda wa kufungua na kufunga sehemu za starehe, mahali unaporuhusiwa kupiga kelele na muda utakaopiga kelele na kadhalika.
Nimewahi kuishi na watu wenye tabia zao za kuangalia mazingira na utamaduni wao, Tanzania si kisiwa cha watu fulani tu, hapana, ni nchi ya Watanzania wote bila kujali utamaduni na kabila lako.
Iwapo kuna jambo la kiutamaduni na ungependa ulifanye kwenye jamii ya Watanzania wengi, hauna budi kuomba kibali ili upewe muda wa kufanya jambo lako bila kuwabughudhi watu wengine.
Kama ilivyo kwa pombe, hukatazwi kunywa, lakini ni kosa kisheria ukinywa na kuamua kuendesha gari au kuimba matusi mtaani.
Mazoea yetu ni kufanya jambo ambalo haujakemewa na wahusika japo unavunja sheria, unapokumbushwa kuwa unavunja sheria unaanza kuhisi kwamba unaonewa.
Wewe unaishi katika mtaa ambao watu wengi wenye utamaduni tofauti na wako wanaishi pia, lakini kwa kuwa utamaduni wako unasema mtoto akivunja ungo anachezwa, unaleta muziki mkubwa unapigwa kwa sauti kubwa mchana kutwa, usiku kucha.
Kwa kigezo cha uhuru wa kufanya jambo bila kuingilia uhuru wa mtu mwingine, kisheria ni kosa na unapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwahusisha watu wengine katika shughuli yako. Haya ndiyo mazoea ambayo yametamalaki katika taifa letu.
Kuna madhara ya kisheria yanayokinzana na mazoea na hatua zinazochukuliwa na baadhi ya wananchi wanaobughudhiwa na makosa mbalimbali.
Moja wapo ni kuvumilia kupita kiasi na jingine ni kuchukua hatua za kisheria mikononi na madhara yake yanajulikana kwamba ni ugomvi utokanao na kutozingatia sheria na kanuni zake.
Hii ni kansa kubwa sana kwa Tanzania iliyoacha kwa muda matumizi ya sheria na kutumia mazoea, ili sheria ijulikane na kufuatwa itabidi jasho la damu litutoke.
Tusipokuwa makini tuendako ni giza nene, kuna wanasheria wa sheria za mazoea, tunafanya mambo kwa kuhisi, hatuna mustakabali na hatujui kesho kukoje kwa kudharau sheria au kutokujua sheria.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.