Nimewahi mara kadhaa kuzungumzia juu ya utamaduni wa Mtanzania wa Tanzania, wakati huo nilikuwa sijawahi fikiria kama Serikali yetu ingeweza kuja na njia mbadala wa kutunga sheria ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya simu na mifumo ya habari.
Kwa kweli, nimefarijika sana na sheria hii hata kabla haijaanza kutumika, sheria ni kitu kingine na kutumika ni kitu kingine, uwepo wa sheria peke yake ni ishara kwamba wapo watanzania wenzangu ambao wameona kasoro katika matumizi ya mitandao hapa nchini, kwa hili nawapongeza sana.


Kwa kawaida, Mtanzania ninayemjua mimi, yule wa zamani alikuwa na maadili yake na utamaduni wake ambao kwa hakika aliweza kuimudu vyema familia na jamii kwa ujumla inayomzunguka, aliweza kuwa mzazi na kiongozi wa utamaduni wake.
 Utamaduni wa Mtanzania ulikuwa  ni wa kipekee, kabla haujaanza kubomoka katika kipindi cha miongo michache iliyopita, Mtanzania alikuwa ni mwoga hata katika suala la uvivu, alikuwa anajua kuwa jamii yetu kwa utamaduni wake haikubali hata suala la uvivu.


Miaka michache iliyopita, yameanza kuja maendeleo, kwanza maendeleo ya demokrasia ya ubishi, watu kujifanya wanajua kila kitu na watu kujifanya wanataka kwenda na wakati, watu kuanza kutafuta sheria za kulinda uhalifu na kutafuta sheria za haki ya binadamu.
Maendeleo yakafika mbali zaidi katika miongo miwili iliyopita baada ya Watanzania kuanza kutafuta usawa na utamaduni wa Kimagharibi ndani ya ardhi ya nchi yetu, ukaja utamaduni mpya wa muziki, mavazi, uongeaji, utendaji na hata uamuzi wa mambo.


Maendeleo haya yakatufikisha kuhoji baadhi ya mila na desturi zetu kama zipo sawasawa, vyama vya kiraia vikaanza kujitokeza kwa nguvu huku vikianzisha uanaharakati wa kufananisha mambo na Ulaya bila kuzingatia utamaduni wetu ukoje.
 Ndoa zikaanza kuvunjika, wanaume wakaanza kuolewa, mavazi yakawa ya wote, utegemezi ukarudi, uvivu ukawa sifa ndani ya nchi yetu, haki sawa ikaja, uongozi ukawa wa kugawana, sheria ikawa kinga ya wahalifu, mahakamani kukageuka sehemu ya kushinda kutafuta haki, mapori yakaanza kukomaa kwa kutolimwa, vyakula vikawa vya kuagiza, hatukufuata tena maghala badala yake tukaanza kula vyakula vya makopo.


Mwanzo wa kuvurugika utamaduni ukawa umewadia, hakuna aliyekuwa nyuma ya wakati kila mtu hakutaka kuonyesha kama yeye ni mshamba, kila jipya linalokuja lilivamiwa, akina dada wakawa hawautaki Uafrika wao wanataka uzungu, akina kaka nao wakaanza kubadili umiliki wao wa nguvu na kuzikabidhi kwa watu wengine, tukawa tegemezi kitaifa.


Leo yapata miongo kumi tangu tupate uhuru, mabadiliko ni makubwa sana yamejitokeza, Watanzania wanamiliki mitandao mikubwa ya kijamii, Watanzania zaidi ya robo tatu wanamiliki simu za mikononi tena za gharama kubwa na zikiwa na mifumo ya mawasiliano ya mbali.
 Leo Watanzania wanapata habari katika muda mfupi sana, habari za kimataifa, haya ndio maendeleo yaliyokuja katika kipindi kifupi, kwa jinsi ninavyokumbuka mimi miaka kama thelathini iliyopita mtanzania alikuwa anaweza akapata nafasi ya pekee sana kumiliki redio na kusikiliza taarifa ya habari kila siku.


Mtanzania alikuwa hapigi simu kwa ndugu yake aliye mkoa mwingine hata kwa miaka mitatu zaidi ya kuandikiana barua ambazo zilikuwa zikisafiri kwa miezi kadhaa, Mtanzania alikuwa hasomi magazeti ya nje ya nchi kwa kukosa fursa ya kuyapata, Mtanzania alikuwa hajui nini kinachoendelea nje tu ya mpaka wan chi yetu, ni maendeleo ya tekinolojia ndio yametufikisha hapa.


Leo Mtanzania anajua habari za dunia katika kipindi cha nusu dakika, anajua ajali, anajua mapinduzi, anajua muziki mpya, anajua vifo, anajua mapenzi, anajua mali za mtu, anajua hali ya hewa kwa ufupi anaweza akajua kila kitu akiwa chumbani na anaweza akaishi akiwa chumbani na anafanya kazi ya kumuingizia kipato bila hofu ya kuanza kubomoa mapori ili apate riziki yake, huyu ndiye mtanzania aliyepata maendeleo ya kisasa.


Watanzania wamefika mbali zaidi kwamba sasa wanaweza kufanya uhalifu wakiwa vitandani kwa kutumia simu, Watanzania wamepoteza utamaduni wao kwa kuiga mambo kutoka kwa wengine, Watanzania sasa wanaona filamu na fasheni shoo kwa kupitia simu zao.
Leo wanavaa nusu uchi, ni maendeleo pasi na utamaduni wetu, wanaoana kwa kutumia simu za viganjani, wanafundishana mambo kwa kutumia simu bila kujua umri na utamaduni wetu, wanauza na kununua mambo mengi kwa kutumia simu, wanawavuruga watu wengi kwa kutumia simu, utamaduni wa Mtanzania haupo tena, utamaduni wa kuheshimiana umeota mbawa.


Haya ndiyo maendeleo tuliyokuwa tunayataka miaka michache iliyopita tukiona kama tumepitwa na wakati. Naipenda sheria na ianze kazi mara moja ili kurudisha heshima ya Mtanzania.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.