Tarehe kama ya leo mwaka jana tulianza kufurahia madaraka yako, uliisha tumbua majipu kadhaa ambayo wengi wetu tuliamini kwamba mambo yanakwenda vizuri kabisa, kwa upande wangu bado naamini ili furaha bado haijapotea.

Tarehe kama ya leo ulikuwa ukingoni kulitangaza baraza lako la mawaziri, wengi walikuwa tumbo joto kama wamo ama hawamo, wapo ambao walitutangazia huku mitaani kwamba wamo lakini uliwabwaga kwa makusudi kama ulikuwa umeafikiana nao, wengine uliwastukiza siku uliposema unatangaza baraza la mawaziri.

Tarehe kama ya leo wateule wako wengi walikuwa matumbo joto hawajui nini kitatokea kwao kwa kuwa ile dhana ya hapa kazi tu ilishawatenga katika dhamira zao, matokeo yake tunayajua wengi tupo nao katika vikao vya kahawa bila kununua tukihoji utendaji kazi wako.

Tarehe kama ya leo mwaka jana wengine ndio ilikuwa mara yao ya mwisho kwenda njia panda ya ulaya yaani uwanja wa ndege, wengine hawakumbuki pasipoti zao ziko wapi hadi leo, madhara ya safari zile kwa upande wangu sijaziona  labda wahusika waibuke na kutuambia nini tumekosa kwa kukosa kwao kwenda ughaibuni.

Tarehe kama ya leo tulikuwa bado tukinywa na kusaza vileo na visivyo lewesha  na kuongea mengi juu ya siasa  na mustakabali wa taifa letu kwa miaka mitano baada ya uchaguzi kwisha, wengi wetu tulikuwa tukikuna majeraha ya hapa na pale kutokana na uchaguzi uliofanyika na kukuibua kidedea.

Mheshimiwa umemaliza mwaka sasa hapo ikulu, huku nje mambo si shwari kabisa, wengi wetu tulikuwa tukiimba wimbo tusioujua, tulizowea yale maisha ambayo wewe ulipokuwa huku ulikuwa huyataki, maisha ya anasa bila kufanya kazi, maisha ya kuwanyanyasa wengine, maisha ya kufanya biasha ra bila kulipa kodi, maisha ya kutumia bila bajeti, maisha tegemezi.

Mheshimiwa huku mambo si shwari tena, umepindua meli na watu tunatota kwa kukosa hewa ya maisha ya kifisadi, maisha ya mipango na dili, mheshimiwa baadhi yetu tumekosa majembe sasa tunalimia meno kichuguu, hii ni Tanzania nyingine, ni Tanzania ile ya kuchapa kazi, hebu geuka tuangalie kwa jicho la huruma ya uvivu wetu.

Mheshimiwa huu ni mwaka mmoja tu tangu umeingia hapo jengo jeupe, sisi watu wazima tunavurugwa na tumefikia mahala hatujitambui tunamwaga shikamoo hata kwa watoto wadogo, huku mzunguko wa bia mezani umepungua hata katika harusi, huku mitaani tumebadilika tunafanya mazoezi kutafuta afya, huku mitaani sasa hivi tumegundua vyakula ambavyo ni sumu katika miili yetu, tumenyooka.

Mheshimiwa mimi nilidhani kunahitajika nguvu sana kufuata sheria, najua hujui lakini sasa hivi chanjo ya suala la kansa ile ya mlungula inaelekea imepatikana, mpokeaji na mtoaji sasa wameanza kuogopana, hujui ni lazima nikujuze kwamba watu tumeanza kuogopana, zile kauli za kawaida kama vile unanijua mimi nani? Nakuapia siku hizi hakuna.

Ni mwaka tu umepita lakini utafiti wangu unaonesha idadi ndogo sana ya ndoa halali ambazo zimevunjika, lakini umevunja rekodi ya kuvunja ndoa feki za michepuko mpaka sasa hivi, wanawake wengi waliokuwa katika ndoa halali nasikia wanadai kuwa wapo fungate na waume zao ambao walikuwa busy mwaka jana tu.

 

Mheshimiwa sina hakika mwakani kipindi kama hiki tutakuwa tunasemaje lakini ukweli hapo ulipokaza nahisi ndio penyewe, wapo wachache wanaochukia lakini wapo wengi ambao wanakuunga mkono hata wale wenzako wa upande ule wa pili. Japokuwa kukaza huko ni kama umetushitukiza hata sisi ambao tulikuwa tunakuunga mkono.

Najua unaelewa vizuri huku tuliko na wengi wetu tunaipenda hii nidhamu lakini nahisi huu msafara wa kenge na siye mijusi tunatia akili, kama ukiweza basi tuchambue mijusi tusikwazane na kenge ambao ndio wahusika wenyewe.

Sina hakika mkuu na hizi sikukuu za safari hii na sina hakika na huo mwezi dume wa Januari utakuwaje lakini kiufupi tumenyooka tukunje utakavyo tutakunjika na tuwe na utulivu, nilikuwa sijui kama nchi hii ina waumini wengi lakini sasa najua.

Kwa ufupi sasa tumenyooka mkuu tukunje utupange utakavyo lazima tuheshimiane.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo.