Wanangu, nawashukuruni kwa kusoma mambo ya zamani pamoja na kwamba yanawakera, kwa sababu wengi wenu mnaona kama historia na ambayo labda mengine hayakuwahi kuwaingia vichwani kwamba yaliwezekana na yalitekelezeka.

 

Niliwahi kuwaandikia barua hii kuwakumbusha juu ya barua ambazo tulikuwa tukiandika, na ilichukua mwezi au zaidi kumfikia aliyeandikiwa. Barua hiyo ilikuwa na ujumbe mzito haiyumkiniki zilikuwa habari za uzazi, ndoa, vifo, majanga na hata tukio la furaha kijijini kwetu.

 

Baada ya miaka kadhaa ya Uhuru tulianzisha Shirika la Posta na Simu ambalo wakati huo simu zote zilikuwa zikiunganishwa Dodoma kwenda katika mikoa mingine. Hii ilikuwa njia ya haraka sana ya mawasiliano, lakini haikuwa kwa watu wote, bali wachache tu waliochukulia jambo lao ni la haraka sana.

 

 

 

Mawasiliano kwa wakati wetu hayakubagua mtu. Yeyote aliruhusiwa kutumia kutokana na uwezo wake, lakini pia serikali ilihakikisha kuwa suala muhimu kama mawasiliano linadhibitiwa kisera, katika kupunguza gharama kwa mtumiaji. Haya ndiyo matatizo ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kwamba chetu ni chetu.

 

Barua  ya wiki iliyopita niliwaandikia juu ya moyo wa uzalendo tuliokuwa nao. Hilo ni moja tu kati ya mambo mengi tuliyoyapa kipaumbele kama sehemu ya manufaa kwa Watanzania wengi, kutokana na imani kwamba nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi ambao kimsingi kipato chao kinalingana.

 

Nakumbuka mambo mengi, siwezi kuyasema yote kwa barua moja. Naweza kuwa nawadondolea mojamoja kila nipatapo siha njema kuweza kushika kalamu, lakini leo tulizungumzie hili la wakulima na wafanyakazi. Kwangu hili ni la muhimu sana. Wakulima gani hawa na ni wafanyakazi gani hawa tunaowazungumzia, wako katika hali gani, umri upi na afya gani?

 

Wanangu, leo nianze kwa kuwapongeza kwa kukaribia kusherehekea Sikukuu ya Wakulima, yaani ile ambayo nyie mmeamua kuigeuza kuwa sikukuu ya biashara. Mmeamua kufanya maonyesho makubwa ya kibiashara tena za nje zaidi kuliko za ndani. Yawezekana ni kutokana na siasa yenu ya utandawazi, “anyway” mimi hainihusu sana, lakini niwapongeze kwa kuidumisha siku hii.

 

Saba Saba ambayo kimsingi ilitokana na tarehe ambayo kilizaliwa chama chetu cha Tanganyika African National Union (TANU), ilikuwa siku maalumu kwa wanaTANU wote, kwa kuwa chama kilikuwa cha wakulima na wafanyakazi, hivyo tulitumia siku hiyo kuadhimisha yale tuliyokuwa tumeyafanya kwa mwaka mzima. Tulionyesha mazao yetu, mifugo yetu, bidhaa zetu za viwandani kwa kifua mbele kuthibitisha uthubutu tuliokuwa nao.

 

Hii ni mada kubwa sana kwangu, lakini yawezekana wapo watakaoshindwa kukubaliana na mimi kutokana na dhana ile ile ya kwenda na wakati, huku wakijua dhahiri kwamba tunazidi kuuza uhuru wetu na thamani ya vitu vyetu, tunapoteza hadhi ya uasisi wa chama chetu na baada ya miongo kadhaa lengo hasa la Saba Saba litapotea kwa kizazi kisichotaka kutunza kumbukumbu.

 

Wakati tukipata Uhuru nchi hii ilikuwa ni moja kati ya nchi masikini duniani, lakini tulikuwa ni matajiri wa itikadi yetu kati ya nchi chache duniani. Tuliamua kwa pamoja kwamba tufanye kazi kwa bidii ili tutoke hapa tulipo na tusonge mbele kiuchumi na kiitikadi zaidi.

 

Tulikubaliana kwamba nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi. Suala la biashara halikuwa kipaumbele na hatukuruhusu mtu afanye biashara kama vile ni sehemu yake ya mapato kwa mwaka. Huyo aliyethubutu kufanya hivyo tulimchukulia ni mnyonyaji na hafai katika jamii yetu, ndiyo maana tuliruhusu maduka yafunguliwe kuanzia saa 10 jioni baada ya kutoka shamba au kazini.

 

Kwa ujamaa wetu tulijua kuwa wanaopaswa kuwa wanyonyaji ni watoto, walemavu wasioweza kufanya jambo lolote, lakini wenye uwezo wa kusuka, kuchonga na kadhalika bado waliona haya kukaa na kulishwa bila kufanya kazi. Vilevile wazee ambao nguvu zao zimetumika katika maendeleo siku za nyuma, tuliwapa nafasi ya kupumzika na kutoa mawazo yao kwa vijana na watoto ili kuimarisha nguvukazi na moyo wa kujitolea.

 

Baadhi ya wazee waliamua kufanya kazi walizojua kuwa hazihitaji nguvu sana, nia yao ilikuwa kuhakikisha kuwa hawawi wanyonyaji katika jamii iliyokuwa inawazunguka. Baadhi walikuwa mafundi wazuri wa baiskeli, cherehani, majembe, miundu na mitego.

 

Baadhi yao walikuwa vinyozi waliofanya kazi hiyo kwa malipo kidogo ili waweze kujikimu kimaisha. Walifanya kazi hiyo pasi na ufundi, lakini siku zilizidi kusonga mbele na hadi mauti yalipowakuta hawakuwa wategemezi kwa kisingizio cha kukosa jambo la kufanya.

 

Tunaelekea katika Sikukuu ya Wakulima na Wafanyakazi, siku iliyokuwa ni yetu kwa wakati wetu kabla hatujabadilika na mfumo wa utandawazi tulionao. Tunakumbuka wakati wetu kwamba siku hiyo ni ya kutembea kifua mbele kuonyesha umahiri wa yale tuliyofanya kwa nguvu zetu wenyewe bila kuwa tegemezi.

 

Tulijenga utamaduni wa kuchekana kama huna cha kuonyesha kwa watu, huna shamba la mfano, huna mifugo ya mfano, huna kihenge cha chakula na huna ankara katika ushirika kuonyesha mapato yako yatokanayo na utendaji wako wa kazi.

 

Hii mara nyingi ilikuwa kwa vijana ambao wengi wenu leo wanaitwa vijana taifa la leo na kesho ambao kimsingi ndiyo walionisukuma kuandika barua hii; ambao wengi wao ni wafanyabiashara ndogondogo almaarufu kama wamachinga, vijana ambao leo wengi wao wamegeuza muziki kuwa sehemu ya ajira yao, wengi wao ambao leo wamekuwa vinyozi na kuacha kutumia nguvu kazi yao katika kilimo au kazi za ukweli.

 

Wanangu, nawaandikia kuwaambia kuwa inakera sana kwa mtu wa zamani kuwaona vijana wenye nguvu zao wakijishughulisha na kazi za wazee wa enzi zetu na wakati huo huo tukilalamika na umasikini tulionao. Kumuona mtu mzima anauza pipi barabarani wakati angeweza kushika jembe na kulima au kufuga; inasikitisha.

 

Wanangu, narudia kusema inakera na kuudhi umuonapo mtu mzima mwenye nguvu ya kuzalisha mali akigeuka kuwa kikongwe anayefanya kazi ya ukinyozi tena bila haya akidai hiyo ni kazi anayoijua vizuri. Sitaki kupingana na ukweli kwamba sasa tumegeuza biashara kuwa uti wa mgongo na si kilimo tena.

 

Wakati wetu tuliwahi kusema fedha si msingi wa maendeleo. Tulisema fedha ni matokeo ya kazi. Usemi huo naamini ukweli upo hata kama baadhi watakataa! Tulisema kilimo ndiyo msingi wa maendeleo. Tulikuwa na chakula cha kutosha kwa sababu wenye nguvu ya kufanya kazi walifanya. Hawakuwa wamachinga, wanamuziki, wapigadebe, wala vinyozi.

 

Nataka tukubaliane kutokukubaliana na hali halisi ambayo tumeamua kuingia kutokana na mfumo wa siasa tuliyonayo, kwamba madalali wanapewa kipaumbele na siasa za kutaka kura kutowalazimisha vijana wafanye kazi za maana na badala yake watumie nguvu zao katika kazi ambazo hazina tija au za wazee enzi zetu.

 

Tujiulize taifa hili linategemea nini likiwa halina wakulima, halina viwanda vya kuzalisha, halina bidhaa zake lenyewe kama nguo, mafuta, vifaa vya ujenzi, vitu ambavyo ni mahitaji muhimu kwa binadamu, dawa za mifugo na kilimo, dawa za binadamu zaidi ya kumiliki siasa yetu ya kujijenga majukwaani.

 

Tunaelekea katika sikukuu ya wakulima na wafanyakazi tarehe 7 Julai. Tujiulize, je, tunaitendea haki siku hiyo au ndiyo tumeamua kuwa ni sikukuu ya wafanyabiashara na kwamba taifa letu litaendelea kwa kufanya biashara badala ya kilimo na kufanyakazi?

 

Pasi na yote hayo tuangalie hatima yetu na bidhaa kutoka nje na madhara tunayoyapata kwa kugeuzwa dampo na sehemu ya majaribio kwa vijana wetu kupewa bidhaa, ili waziweke sokoni kwa faida ya wenye viwanda na bidhaa.

Mungu ibariki Tanzania tukumbuke kwa dhati Siku ya Wakulima na Wafanyakazi

 

Mzee Zuzu,

Kipatimo.