Kwanza nianze kwa kuwashukuru kwa kusoma waraka wangu na niwatakie siku njema ya leo na ikawe na baraka kwenu nyote. Mimi si mtu wa kusali sana, lakini ninajua kuwa Mungu yupo na anatulinda sana. Kwa sisi wachache ambao tumefanikiwa kuishi miongo mingi tuna kila sababu ya kumshukuru na kumuomba atujalie uhai kwa miaka michache tena ili tule matunda ya maendeleo.

Kuna watu wengine wanaamua kukatisha maisha yao kwa kunywa sumu na wengine kwa kujinyonga, achilia mbali wale ambao wanajipiga kwa silaha au kupigwa kwa silaha. Hawa wanakuwa wamezongwa na mambo mengi sana. Wapo wanaoamua kujipunguzia maisha kisa mapenzi na wapo wanaokatisha maisha kisa matatizo. Kama wewe si miongoni mwa wanaofikiria kufanya hivyo, basi niseme kwamba hauna haja ya kufanya hivyo kwa sababu maisha yanabadilika na maisha ya leo si ya kesho. Kikubwa ni kumtanguliza Maulana.

Leo nimeamua kushika kalamu si kwa lengo la kumlaumu yeyote, bali kupeana taarifa juu ya suala la usalama wa raia kwamba ni suala mtambuka. Wapo wanaosema kuwa hilo ni jukumu la Jeshi la Polisi. Hiko ni kweli, lakini kwa asilimia kubwa suala hili limo mikononi mwetu kama wananchi kwanza ndipo polisi waweze kuwa msaada kwetu.

Naandika waraka huu nikiwa na mambo mengi sana kichwani, hasa ukizingatia kwamba wananchi wote tunaamini kwamba usalama wetu kama raia ni lazima polisi wawepo. Kwanza, kwa sababu wanalipwa kwa kodi zetu; pili, kwa sababu ni waajiriwa wetu.

Mimi nimebahatika kutembea kidogo katika nchi za wenzetu na nimeona jinsi ambavyo jukumu la polisi linavyochukuliwa, hasa katika matukio ambayo si tu ni rafiki bali kuwa hatari miongoni mwa raia. Wakati wenzetu wanageuka kuwa sehemu ya msaada kwa polisi hapa kwetu ni tofauti kabisa.

Nadiriki kusema hapa kwetu hata kama umefanyiwa uhalifu inaweza kuwa shida kutoa taarifa kituo cha polisi, kwa sababu aliyefanyiwa uhalifu naye anaweza kuwa mhalifu.

Kuna swali la kujiuliza, kwanini hili lipo na hakuna utaratibu ambao unaeleweka? Jibu ni rahisi sana, kwamba wakati wa kuwatumia polisi na wakati wa polisi kuwatumia raia ulikosewa kwa mambo mengi. 

Wapo askari waliodhani kwamba kuwatisha wanaoshitaki ni kupunguza uhalifu au kufanya upelelezi kwa haraka zaidi, lakini hatukujua nini athari katika siku za usoni.

Sasa hivi raia kumsaidia mtu aliyepata ajali kwa maana ya kumpeleka polisi ili awahi matibabu imekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye jamii tunayojipambanua kama ndugu. Mtu anagongwa na gari na hawezi kupata msaada mpaka pale polisi watakapofika na kila mtu anajua uhaba wa ikama ya Jeshi la Polisi.

Hili hatukulifikiria mapema kwamba rafiki namba moja kwa Jeshi la Polisi ni raia mwema. Iwe kwa kutoa taarifa hata kama hazina usahihi sana, kusaidia mtu aliyepatwa na tatizo hata kama hataweza kusaidiwa kwa kiwango cha polisi, hawa ndio ninaowaona kama polisi jamii kwangu na kwamba ni msaada mkubwa sana kwa Jeshi la Polisi katika kipindi hiki ambacho idadi yao na matukio ya uhalifu havina uwiano.

Iwapo mtu amevamiwa na jirani ana silaha anataka kusaidia, ninaamini huwa anajiuliza maswali mengi sana kabla hajatumia silaha kuokoa maisha ya jirani yake na hatimaye huamua kucha kutumia silaha ambayo kimsingi ilipaswa kusaidia kuokoa maisha ya raia mwingine. 

Hili linazungumzwa sana kwa sababu tayari linapotokea tukio la namna hiyo mtoa msaada anajuta kwa kupoteza muda na fedha katika kituo cha polisi.

Tunaziona ajali za pikipiki sasa hivi na wengine ni watoto wadogo ambao wanapaswa kukimbizwa hospitalini ndipo taarifa itolewe polisi, lakini imekuwa tofauti sana kiasi cha kuwafanya waliokuwa wasamaria wema kuwa maadui wa watu wema, kwa sababu tu ya aina ya upelelezi ambao unashindwa kubadilika na kwenda na wakati. Polisi msipokwenda na wakati kazi itakuwa ngumu sana kwenu na kwa jamii.

Tuangalie namna ambavyo wananchi watashiriki katika kuleta amani kwa sababu ninaamini kabisa kwa idadi ya askari iliyopo haina uwiano mzuri na matukio ya uhalifu unaoendelea. Iwapo tutakubali kuwatumia raia wetu, ninaamini kazi itakuwa rahisi na tutapunguza uhalifu kwa asilimia kubwa. Hata hivyo niwapongeze kwa kujitahidi.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.