Kabla sijaanza na salamu ni vema nikatumia fursa hii kutoa pole nyingi sana kwa wafiwa na watoto wote waliopoteza marafiki zao wa utotoni. Wapo watoto ambao kwa kitendo hiki huenda ndoto zao pia zikawa zimekufa kutokana na wenzao kutendewa matukio ya kutisha.
Najua ninazo salamu lakini kule Njombe katika kipindi hiki naamini hawahitaji salamu, bali wanahitaji pole ya matatizo yaliyowasibu. Katika waraka wangu ujao nitatuma salamu za wiki hii.
Wiki jana vyombo na mitandao ya kijamii iliandika sana juu ya mauaji ya kutisha yanayofanyika Njombe kwa watoto wadogo, yakihusishwa na imani za kishirikina, jambo hili linasikitisha sana.
Unaweza ukafikiri kwamba bado uko dunia ya kwanza kwa imani potofu na mbaya kama hizi. Kwa yeyote aliye na mtoto anaelewa ninazungumza nini na anaelewa uchungu alionao mzazi wa mtoto aliyefanyiwa ukatili huo.
Najua wengi wenu na wasomaji wa waraka huu hamuijui Njombe, mimi naijua kwa sababu katika ujana wangu nimetembea sana nchi hii takatifu, nchi ambayo iliishi katika hali ya kuheshimiana na upendo uliopitiliza, ni nchi ambayo ilijengwa katika misingi ya utu, naijua Njombe ile na Njombe hii ya muingiliano.
Nyamuyuya iliyokuwa makao makuu Mdandu kabla haijawa Njombe kama wilaya na sasa mkoa, naijua sana, ni mkoa uliokuwa wenye rutuba sana na miti mingi ya asili, ni mkoa ambao mvua zake zilikuwa za kutosha na hali ya hewa kama Ulaya.
Ni mkoa ambao Wazungu waliweka makao yao maeneo ya Kibena, Bulongwa, Uwemba, Lugalawa na sehemu zingine nyingi, sifa moja kubwa ya Njombe ni kwamba ukienda kufanya kazi utahamia.
Sifa ya Njombe inabebwa na wenyeji ambao ni wakarimu sana, hasa kama utampata mwenyeji, si mhamiaji. Njombe unaweza ukaenda lakini kurudi ni suala la majadiliano.
Muulize yeyote aliyepata kwenda Njombe ile ninayoijua mimi, Njombe ambayo haikuingiliwa na waovu na Njombe iliyokuwa na neema kabla ya wawekezaji uchwara hawajaamua kuwaumiza wenye mkoa wao.
Njombe kwa asili yake haikuwa na imani za kishirikina na ndiyo maana watu waliishi kwa tiba mbadala kutoka kwa watu maalumu ambao walikuwa wakijulikana kwa matibabu yao kabla ya kwenda katika zahanati wakati huo.
Njombe ilikuwa inajua baadhi ya watu kutoka sehemu zingine kwamba ndio wanaomiliki tabia za ushirikina, hili nalizungumza kwa sababu niliishi huko wakati wa ujana wangu kabla ya kuja Kipatimo.
Najua imani za kishirikina zinajengwa na vibali vya uganga vinavyotolewa na wananchi wenye kushiba ushirikina. Kwa Njombe naamini ni rahisi sana kama kumsukuma mlevi kuwajua waganga wa kienyeji, ni suala la uthubutu wa viongozi walioko huko kuamua kuwauliza wananchi wawataje ili wachukuliwe hatua.
Najua kwa Njombe ni suala la muda mfupi kutokana na jiografia yake na utamaduni wa watu wa Njombe. Tukiweka siasa pembeni na sheria za haki ya binadamu ambazo zinawalinda wahalifu wakati fulani kwa kigezo cha ushahidi, sioni kwanini jambo hilo lichukue hata siku mbili bila kupata suluhisho.
Kwani viongozi mnasemaje katika hili, hamjui kuwa waganga wapo miongoni mwa jamii hiyo? Hamjui kuwa wana mabango ya matangazo maeneo hayo? Hamjui kuwa wengi wao wanatoka katika mikoa fulani kiasi cha kukosa uchungu kutokana na maagizo yao? Hivi kuna tatizo gani kama mkiwashirikisha wananchi?
Sijui ni lini itakuwa hatima ya matukio haya hapa nchini, hasa ukizingatia yanapata baraka kutoka kwa baadhi ya watu, tena wengine ni wenye mamlaka. Iwapo litadhibitiwa Njombe, naamini litahamia mikoa mingine, na hii inatokana na ukweli kwamba maisha ni magumu na watu wanatafuta njia rahisi za kutajirika kwa imani za kishirikina na ndipo wanapokutana na waganga matapeli wasio na huruma.
Nataka kujua tu, hivi kuna kiongozi ambaye mtoto wake amechinjwa na akaleta siasa katika jambo hilo? Mbona jitihada za waliotekwa zilizidi kuliko wachinjaji? Sina nia mbaya, lakini natamani mtu mzima mwenye dhamana achinjwe na hao wanaodanganywa na waganga waliopewa baraka na haohao wenye dhamana, labda ujinga huu utakwisha.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.