Wiki jana niliandika barua kama hii nikisema huyu ndiye mwenye sifa za kuwa Rais wa awamu ya tano, niliainisha sifa chache kutokana na ujinga wangu, sifa ambazo baadhi ya watu wanaweza kusema kwa utaratibu wa maisha ya sasa ya utandawazi siyo rahisi kumpata kiongozi mwenye sifa hizo.
Julius aliwahi kuongea na waandishi wa habari na akatoa sifa za mtu anayeweza kuwa Rais wa nchi hii, baadhi ya waandishi walimuuliza kama anadhani kwa mawazo yake kuna mtu mwenye sifa hizo na alijibu akisema kuwa yeyote anayedhani kuwa hakuna mtu mwenye sifa hizo ni mjinga, mimi nakubaliana naye.
Katika waraka wangu wa wiki jana nilisema nitakuwa na mfululizo wa mawazo yangu juu ya kiongozi bora wa awamu ijayo, Tanzania ni nchi maskini ambayo kila awamu inafanya kazi yake vizuri lakini haiwezi kumaliza matatizo yote yaliyoko katika nchi hii.
Mimi kwa ujinga wangu bado naamini katika msemo wa kila kitu kinaweza kufanywa haraka, na kwamba haraka haraka ina Baraka, naamini katika kuleta mabadiliko ya ghafla yenye tija kwa taifa lakini mabadiliko hayo lazima yatawaumiza walio wengi na kuamini katika polepole ndio mwendo au huo kuufanya kama siyo utaratibu wa uongozi.
Lakini Tanzania ninayoijua nafikiri tunahitaji kiongozi japo wa kutupeleka haraka kidogo kimaendeleo hata kama yatawaumiza akina Zuzu wachache na iwe faida ya wengine wengi ambao wanayataka matunda ya uhuru wayatumie sasa.
Napenda sana Rais ajaye afanye mambo mengi, lakini hawezi kuyafanya kama hana vigezo vya kufanya kazi hizo, Rais wa awamu ya tano lazima awe na uwezo wa kubadilisha mfumo wa elimu, kutoka elimu tegemezi ya kusubili ajira na kuwa elimu ya kujiajiri na kujitegemea, awe na uwezo binafsi wa kutekeleza hili.
Napenda sana Rais ajaye awe na uwezo wa kutufanya Watanzania wote kuwa ni kitu kimoja, tuwe na umoja, tuwe wazalendo na kusiwe na matabaka ya kikabila, kikanda, kimapato na kielimu, kwa ufupi apoteze ile hali ya wenye nacho na wasio nacho kwa kutumia sheria ambayo itawabana waliokwepa kodi na kujilimbikizia mali wasalimishe kwa taifa.
Ningelipenda Rais ajae afanye uteuzi wa wasaidizi wake ambao hawezi kuwaonea haya, wakivurunda awafukuze bila hata kujadiliana, iwe kama hii awamu inayoishia, akiweza avunje mabaraza hata mara mia lakini tupate watendaji walio bora na si bora kutenda, ningelipenda kiongozi ajae awe na uwezo wa kujiuzulu kwa kushindwa kufanya kazi au watu wake kushindwa kufanya kazi.
Rais ajae naona ni yule mwenye uwezo wa kuamua mambo ya msingi yeye mwenyewe bila kutegemea ushauri wa mtu ambaye anaweza kuwa na maslahi kwa jambo ambalo anashauri, awe Rais mwenye kutoa uamuzi pasi na kutomwogopa mtu, nchi yetu imeoza kiutendaji na hasa serikalini, tunahitaji Rais mwenye mamlaka na anajua kuyatumia.
Napenda Rais ajaye awe ni yule mwenye kuweza kusema Watanzania tujitegemee, tusitegemee wafadhili kwa kuwa wataendelea kututawala kwa bajeti zao, mifumo yao, utamaduni wao, na mwisho wa yote hata uongozi unaweza kuwa wao.
Napenda Rais ajae naye awe mfuatiliaji wa mambo ya wananchi, awe mfutiliaji wa viongozi ambao si watendaji, awe uwezo wa kumchukulia hatua kiongozi anayefuja mali ya umma, anayetumia vibaya madaraka yake, anayedhani cheo ni mali yake ni si cheo kuwa ni dhamana.
Napenda Rais ambaye hatafungamana na upande wowote wa kimakundi, Rais ambaye anaweza kusema ndiyo kwa vyama vya upinzani na Rais ambaye yuko tayari kupokea mawazo ya watu walio nje ya mfumo wa kiutawala, kiongozi anayekubali kukosolewa ndiye kiongozi bora, kiongozi anayeweza kusikiliza na asiyependa kusikilizwa.
Awe Rais ambaye atasema wazi kwamba mikataba mibovu inayofanywa na wasaidizi wake haikubaliki, awe muwazi kwa wenye nchi, awe bahiri kwa manufaa ya uchumi wa taifa letu, awe na uwezo wa kuamurisha mambo ya msingi kwa taifa letu, apuuze anasa za wachache kwa manufaa ya wengi.
Ninayo mengi sana ya kumchagua Rais wa awamu ya tano na nitaendelea kusema kwa barua kadhaa zijazo lakini kwa leo mwishoni napenda Rais anayeweza kusema yatosha bila haya wala kumuonea haya mtu, rafiki, ndugu na jamaa yeyote yule. Mungu ibariki Tanzania.
Wasaalam,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.