Sijui ni kwanini leo nimeamua kuandika waraka huu, najua wapo ambao watakumbuka kama mimi, tulipotoka ni mbali, hilo halina ubishi, lakini leo naona ni kama sekunde tu kuyakumbuka na ndiyo maana hata kutoa salamu naona kama nitakuwa nawapotezea muda.

Najihisi kama mzee, najihisi kama kijana lakini najihisi kama mtoto, nakumbuka juzi tu nilikuwa mtoto ambaye nilikuwa nikichunga mbuzi na kuwinda ndege, nakumbuka wakati nikianza darasa la kwanza na daftari langu moja tu mpaka darasa la tatu, muda mwingi tuliandika chini na kutumia vidole kufanya hesabu, ni juzi tu.

Nikawa mkubwa, nikaoa, nikawa na familia yangu na sasa nimejukuu na ninawaona wajukuu zangu kwa umri wao kama wangu wakiwa tofauti kabisa na mimi, hawachungi tena na sasa mbuzi wanawaona katika mabanda ya maonyesho.

Hawawindi tena na wanawaona ndege na wanyama wengine tuliowinda enzi zetu katika televisheni, hawaanzi darasa la kwanza tena siku hizi, bali wanasoma shule za awali na wana madaftari mengi kuliko sisi.

Yapo mengi ya leo kuhusu shule tofauti na sisi lakini kila jambo lina changamoto zake, wakati sisi walimu walikuwa ni wazazi, waelimishaji, leo napata kigugumizi kwa baadhi yao, wakati sisi walimu walikuwa ndio mwisho wa elimu, lakini leo kuna walimu baada ya walimu, kiufupi kuna shule baada ya shule, siku chache tu zimebadilisha mfumo wa elimu kiasi cha kutisha, haya ndiyo maendeleo ninayoota na kuyakumbuka kwa tofauti zake.

Zamani kulikuwa na vitabu maalumu ambavyo vilitumika na vilitusaidia sana, leo kuna maktaba ya vitabu ambavyo mwanafunzi anapaswa kuwa navyo popote awapo ili kuweza kufundishwa.

Vitabu vinakwenda sambamba na rundo la madaftari ambayo mwanafunzi anapaswa kuyabeba kila siku, leo mtoto anahitaji kagari kadogo kwa ajili ya kubeba vitabu na madaftari na kama hana ni tatizo la kubeba mgongoni mpaka atakapomaliza shule na pindi akimaliza anaanza kuhudhuria matibabu ya mgongo hadi mwisho wa maisha yake.

Nimekumbuka zamani enzi za daftari letu moja mpaka darasa la tatu na madaftari saba mpaka tumalizapo shule ya msingi.

Nakumbuka redio zetu kama mwalimu mwingine zaidi ya yule wa darasani.

Kulikuwa na vipindi vizuri sana na kila shule ilikuwa na redio yake ya mbao ambayo ilikuwa inakaa kwa mwalimu mkuu pamoja na saa ya shule, nakumbuka jinsi redio ilivyokuwa ikihama kutoka darasa moja kwenda jingine, nakumbuka vipindi vya jioni na watangazaji ambao walikuwa walimu, kimaadili na kielimu, tumetoka mbali.

Leo hii ni shule chache sana zenye redio na wanafunzi wengi wanaishi na redio muda mwingi kupitia simu zao na hata nyumbani kwao, naona jinsi mwalimu wao mpya anavyowafundisha mambo makubwa na mapya tofauti na sisi.

Naona wingi wa madaftari na masomo anayopata shuleni na wingi wa masomo anayopata kupitia redio au televisheni, hapa ndipo ninapowaza mpaka kichwa kinaniuma.

Nakumbuka michezo yetu ya riadha, kandanda, kuruka, shabaha, mieleka, kutupa tufe na michezo ya kujificha.

Leo hakuna michezo tena, sehemu zote tulizochezea sisi zimejengwa viwanda na majengo ya wenye hela, leo kandanda linachezwa midomoni na vijana wanaoangalia mpira katika televisheni, leo vijana hawakimbii tena, kila kitu kimerahisishwa kwa kitu kiitwacho gemu katika kompyuta au televisheni, leo vijana wanacheza kwa kukaa kitako na ndipo ninapoona maisha yanakwenda kasi kuliko ninavyojiona nikizeeka.

Nadhani tumefika mahali ambapo tuna kizazi ambacho kinaishi maisha ya kiteknolojia zaidi katika kipindi kifupi mno, ni kizazi cha wazazi wenye kushindwa kujua umuhimu wa michezo na mambo ya kutumia ubongo zaidi kufikiria badala ya kuamrisha roboti huku wakiwa kitako.

Ni watoto wanaobebeshwa mizigo ya madaftari na kulishwa masomo ya ajabu kwa kuamini siku moja watakuja kujitegemea. Ni kizazi ambacho kina walimu zaidi ya mwalimu mwenye maadili, ni kizazi cha kompyuta, muziki, sanaa za maigizo na maisha mepesi ya kuomba na kuamini maisha ya kujipatia mafanikio bila kusubiri na kutoa jasho.

Kizazi cha ustaa na kuhusudu watu maarufu duniani badala ya kupambana wao wenyewe, ni kizazi kisichojua kulima, kupalilia, kuvuna na kuhifadhi. Mimi nakumbuka zaidi zamani, haya ya sasa naona yananipita kwa sababu sioni tija yake.

Hata ukiniuliza vitabu na sinema, nitakumbuka vya zamani, ukiniuliza vipindi na magazeti, nitakutajia vya zamani, ukiniuliza walimu na viongozi, nawakumbuka wale, ukiniuliza michezo na masomo ni dhahiri nitakutajia yetu, haya ndiyo maendeleo.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.