Pamoja na kwamba natukanwa sana na vijana wa dotcom, wakiamini kuwa wako sahihi kwa matusi yao na uhusiano wa kile ambacho nakizungumzia au kukiandika katika waraka huu, najua iko siku nao watakuwa BBC, yaani ‘Born Before Computer’ kwa kizazi chao kitakachokuwa kimekengeuka kuliko wao.

Hivi sasa wao wanajiona wamejitoa akili, wakiamini huko waliko ndiko sahihi na huku tunakoshauri sisi BBC siko kwenyewe, kumepitwa na wakati. Mimi naona sawa tu japokuwa kunakera unapoona mbegu ya bangi inapandwa katika shamba la mahindi na kujiuliza tunatarajia kuvuna nini – chakula ama ulevi?

Leo nimeamua kuandika barua hii kwa sababu, siku chache zilizopita nilijaribu kutoa ushauri juu ya baadhi ya vipindi vyetu katika redio na televisheni. Nilitumia mtandao wa jamii katika kutoa mawazo yangu lakini majibu niliyopata kutoka kwa wadau yalinikatisha tamaa, kwani wachangiaji wengi walikuwa wanataaluma hiyo hiyo ya habari.

Walitumia muda mwingi kunifahamisha juu ya taaluma yao kwamba kazi kubwa ya vyombo vya habari ni kuburudisha na kuelimisha, na katika kuelimisha wanazingatia sana mahitaji ya jamii husika kwa wakati huo yanataka nini.

Kimsingi nakubaliana nao kwa hoja ya ubinafsi wa rika na taaluma ya habari ya leo ya kutotambua maadili ya kuburudisha na kuelimisha, lakini mimi binafsi naamini kama vyombo vya habari vingekuwa na msimamo wa kweli wenye mlengo wa dhati katika kuelimisha na kuburudisha, isingekuwa taabu kwa Serikali kuufanya mmoja kati ya mihimili yetu mikuu.

Wahenga wenzangu watakubaliana na mimi jinsi maadili yalivyoporomoka kupitia muhimili huu unaong’ang’ana kwa hoja ya udhaifu wa majukumu yao, wanaoliangalia soko kwa wakati bila kuangalia maadili na utamaduni wa Taifa letu. Taifa lolote lisilo na utamaduni ni Taifa mfu, nachelea kusema kwamba tu mahututi kitandani kuelekea kifo cha Taifa letu.

Miaka yetu kila kilichotangazwa kuanzia asubuhi hadi jioni wakati wa kufunga matangazo kilikuwa na maana kwa Watanganyika na Watanzania. Tulijifunza katika kilimo, biashara, afya, usafi, mazingira, utamaduni, elimu ya kisomo chenye manufaa na kadhalika. Tulipata burudani katika miziki ambayo ndani yake kulikuwa na mwendelezo uleule wa yale tuliyosikia tangu asubuhi hadi jioni.

Nakumbuka nyimbo nyingi sana za kilimo, afya, mazingira, utamaduni na kadhalika. Hatimaye tulitia fora katika maonesho ya mtu mweusi Expo 70 kule Japan tukiwa na ngoma, mavazi, watu wetu na utamaduni wetu.

Leo napata taabu kusikiliza muziki wa kwenu, muziki wa mahadhi ya Kimagharibi na tabia za Kimagharibi. Nawaona kama watoto yatima wasio na wazazi wanaoweza kuwaiga tabia zao. Nawaona watoto yatima mtakaowaachia watoto wenu tabia mchanyato ambayo si ya Kitanzania.

Navichukia vyombo vya habari kwa kutukuza ujinga tunaolazimishwa kuusikiliza, ujinga ambao haufunzi na unaopotosha maadili ya Taifa letu ambalo tulililenga liwe la amani na upendo, uzalendo na kuheshimiana.

Jamani, niseme tu kwamba nimechoka na manyimbo yenu sasa, ambayo hayafundishi maadili mema na yanayowafundisha matusi na uvivu. Tunatukuza visivyotukuzika, tunatukuza mambo ya kijinga na kuacha mambo ya maana. Tunashindwa kuheshimu waliofanya mambo ya maana tunaheshimu wajinga. Mimi naomba nipewe lawama kwa jambo hili, katu siwezi kuwa pamoja na ninyi katika mawazo na ujinga huo, mmechafuka.

Ningelipenda siku moja kwa kauli moja tuseme yatosha hatuwezi kuwa na ajira za mtu kutoa matusi na tukamshangilia, tukasahau nyimbo zenye mafunzo kutoka kwa mabingwa wa ukweli mnaoshindwa hata kuwaenzi kwa ujinga wenu.

Mimi nawasalimu kwa salamu hizo kama mzazi kwa nia ya kutaka mjitafakari na mjiulize nini matokeo ya hizo burudani zenu za matusi na kushereheshwa na vyombo vya habari kama kitu muhimu sana cha kuelimisha hiyo jamii yenu ambayo haitaki kusoma, kulima, kujitegemea, kujitolea, na kadhalika.

Tuna jamii ya walevi, wagomvi, makahaba, wavivu, wajinga na kuishia kuilaumu Serikali. Kama maisha ni magumu mnashindwa kula kwa kuwa matusi yenu hayanunuliwi, bora lawama.

Tujiulize akina Mbaraka, Marijani, Hamza, Cosmas, Maneti, Fresh, Bi Kidude, na bendi kama Cuban, Nyanyembe, Kilwa, Nuta, Afro 70, Vijana, Bima, UDA, walifanya nini, kwa lipi tunawakumbuka ama ndiuo msimu wa mbuzi kulamba reli na mbwa kala mbwa?

Mzee Zuzu, 
Kipatimo.