Wakati nilipokuwa mtoto wazazi wangu walinipeleka katika kanisa ambalo mimi nilibatizwa na kupewa jina ninalotumia mpaka leo. 

Kwa jinsi ninavyosimuliwa ni kwamba sikulia wakati wa kubatizwa kwa sababu maji hayakuwa mengi kama ambavyo siku hizi watu wanalia kwa kubatizwa ndani ya maji mengi. Kumbuka mtoto mdogo suala la kuoga ni kama adhabu, hasa maji yapopita katika shingo.

Leo nimeamua kuandika waraka maalumu juu ya ubatizo. Ubatizo huu ni wakupewa majina, na yapo majina ya namna nyingi sana na kwa wanaojua jina linaweza likashika maana au kuwa na maana sana katika jamii na pengine kuwa binadamu mwenye mamlaka duniani na vyovyote vile iwavyo. Hayo ndiyo majina ambayo wengine tunapewa tunaendelea kuwa Zuzu na wengine wanapewa  wanaendelea kuwa Bahati.

Ubatizo upo wa namna nyingi, lakini upo wa maji machache na maji mengi; upo wa kubatizana kwa utani lakini unasadifu ukweli fulani katika maisha yetu na ndiyo maana leo vijana wengi wana lakabu nyingi za kutaka kutambuliwa kwa nguvu waliyonayo katika jamii. Lakini pia kuna ubatizo wa kuapa na kupewa jina la mamlaka katika maisha yetu ambayo tunamiliki pia majina mengine ya maji au kupewa.

Unapoapa kushika madaraka fulani makubwa, unaapa kuwa na jina jingine ambalo sasa utaheshimika kwa jina hilo, utajulikana kwa jina hilo kwa kazi utakazofanya kwa mamlaka uliyopewa. 

Utakapoapa utakuwa na ngazi moja zaidi ya yule aliyepewa jina au aliyebatizwa kwa maji machache au mengi, wajibu wako katika ngazi hiyo ni kumtumikia mwenye jina ambaye hajaapa kama ulivyoapa.

Siku za hivi karibuni, kama miaka mitano iliyopita, niliwahi kumsikia mtu mmoja mashuhuri sana aliyekuwa akituasa juu ya ubatizo tutakaopitia. Alisema muda wa kiapo cha maji baridi na vuguvugu machache na mengi umekwisha, sasa kuna kiapo cha moto. Sikumuelewa kabisa mtu yule mpaka nilipokaa na kutafakari kwa kina maelezo yale ndipo niligundua kuwa ana maana gani.

Jina la kubatizwa kwa moto ni jina ambalo muda wowote unaweza ukalikana au ukakanishwa na muapishaji. Ni jina ambalo ni dhamana kubwa kwa mbatizaji na wahitaji. Haya majina kama Zuzu huishia tu kwenye kutamkwa lakini halina maana sana kwenye jamii inayokuzunguka hata kama jina hilo umebatizwa kwa moto. Lakini majina yote yanayoanza na Mheshimiwa yanapaswa kuheshimiwa na mwenye jina na hata wanaokutaja.

Pamoja na kwamba zamani wakati tukibatizwa  maji kulikuwa na majina haya ya kubatizwa kwa kuapa, lakini ninadhani waapaji wengi walikuwa na hali fulani ya woga na kuheshimu majina yao katika jamii. 

Nikiwa mdogo na jina langu la maji, kulikuwapo na wenye majina ya kuapa. Hawa walikuwa na heshima kubwa na walitendea haki majina yao.

Miaka inavyokwenda mambo yanazidi kubadilika, sasa watu wengi hawabatizwi kwa maji machache, badala yake wanabatizwa mtoni kabisa, na wale wanaobatizwa majina ya kiapo sasa hivi si wale tena wa majina ya wakati ule kwamba ukipewa jina unakaa kusubiri muda wako uishe na uondoke, kiapo cha sasa ni cha moto, ukileta ulegelege basi unakimbizwa na moto ambao unakuwakia nyuma.

Sasa hivi kukubali jina la kiapo uhakikishe kwamba utatendea haki jina lako. Kukubali jina la kiapo siyo sifa tena, bali inaweza kuwa fedheha kama hukujipanga kulitendea haki jina ulilopewa. Heshima ya jina lazima iende sanjari na kile ambacho jamii inatarajia kukipata kutoka kwako, heshima ya jina inategemea sana moyo wako umepangaje katika kulitumikia jina ulilopewa.

Tumeona ambao wamepewa majina na wakabaki ndani bila kutoka kwenda kujitambulisha kwamba mimi ndiye fulani. Majina yao yamefutwa hukohuko ndani kabla hawajatoka. 

Tumeona ambao wamepewa majina ya viapo lakini wakakosea kiapo na wakafutiwa majina yao hapo hapo. Huo ndio ubatizo wa moto ambao watu wengi hatukumuelewa yule mzee aliposema pale Dodoma.

Kwangu mimi, ninapongeza majina ya moto, yanatufanya tusiwe miungu watu kwa majina ya muda mtu, yanatufanya tuwaone wenye majina wakiwajibika na majina yao na kuacha alama za uongozi katika jamii.

Naomba tu ubatizo huu wa moto uendelee, maana kuna watu wengi majina hayo si yao kwa matendo, maadili, kuigwa na kuvaa uhalisia.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.