Tangu zamani dhana kwamba mtu mzee ndiye mchawi katika jamii, imejengeka sana miongoni mwa walio wengi wenye upeo mdogo wa kufikiri na kuiaminisha jamii yenye maadili mema kuwa na imani potofu kwa sisi wazee.
Wanangu, leo nimeamua kuandika barua hii nikiwaeleza mawazo ambayo jamii iliyonizunguka inawaza juu yangu. Nabashiri mambo kutokana na uono nilionao baada ya kuishi miongo mingi ya kutosha – miongo ambayo nimeona na kushuhudia mambo mengi mazuri na mabaya.
Mara nyingi nafikiriwa nafukuza mvua kutokana na kauli zangu kwamba pamoja na wingu kubwa lililopo mvua haitanyesha. Hii ni kutokana na uzoefu wangu kwamba hapa Kipatimo wingu la magharibi halina madhara ya mvua. Wingu hilo linapita. Mvua ya Kipatimo inatokana na wingu zito la kaskazini-mashariki na si vinginevyo.
Nahisi kuwa sasa ni mganga wa kienyeji kwa sababu kuna mambo nayabashiri, na kwa kweli yanatokea katika jamii yetu, kwa yale mema inachukuliwa kama ni baraka za uzee; na kwa yale mabaya nachukuliwa katika sura nyingine kwamba sasa ni kigagula.
Pengine kuna siku wananchi wenye hasira watasema nina macho mekundu kwa hiyo sistahili kuendelea kuishi. Najua kwamba nitakufa japokuwa sijui ni lini, lakini kwa uhakika zaidi naona siku si nyingi.
Siku zinakaribia iwe kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu au kwa kuchomwa na moto na hao wanaoniona na macho mekundu na pengine kupelekwa Msitu wa Pande na watekaji kutoka Kenya.
Naomba nibashiri mambo machache kama mvua ya Kipatimo inayotokea kaskazini-mashariki, mwaka ule tunafanya uchaguzi wa vyama vingi niliwahi kuota ndoto kwamba Azimio la Arusha litakufa kifo cha kusemwasemwa, kwamba lipo kama halipo, linazikwa kama halizikwi na mwishowe tutahitimisha kwa kuanua tanga kwamba Azimio la Arusha lilikwisha kupoteza maana katika mfumo wetu wa kujitegemea. Ubashiri unaelekea kukamilika.
Nilibashiri kuwa baada ya kufanya kila kitu ni utandawazi, basi viwanda vya umma vitapoteza mwelekeo. Naomba tujiulize tuna viwanda vingapi vya umma tulivyonavyo bado vinafanya kazi. Tukilijua hilo, basi tunaweza kufanya tathmini kama naelekea kuwa mchawi au mbashiri feki.
Miaka michache iliyopita nakumbuka nililalamika sana juu ya nguvu kazi iliyoamua kujikita katika kazi zamani zilizokuwa zikifanywa ama na wazee au watoto – kazi za unyozi, kuuza bidhaa ndogondogo na kadhalika, na hatimaye madhara yake ndiyo haya ambayo kilimo kile chetu cha kufa na kupona kimepotea na kuzaliwa kilimo cha majukwaani kiitwacho kilimo kwanza.
Huu ni ubashiri kwamba jinsi siku zinavyokwenda tutakuja kutumia kompyuta kulima mashamba yetu huku Kipatimo. Naomba kwa nguvu zote tufikie malengo hayo.
Naendelea na utabiri wangu ambao siku moja mtasema mzee wa Kipatimo akamatwe apelekwe Mabwepande akashughulikiwe, kwa kuwa ni mchawi anayesema mambo yatakayojitokeza.
Nchi hii muda si mrefu itakuwa jangwa. Hii inatokana na kuamini katika biashara na si kilimo. Mnakata miti ya mbao tuliyopanda kina Mzee Zuzu, lakini hamtaki kupanda miti yenu.
Mnavuna mitipori kwa ajili ya mkaa, lakini hamkumbuki kupanda yenu, mnaharibu vyanzo vya maji kwa kisingizio cha maendeleo, siku ya siku ikifika mtatufuata makaburini kutuuliza tuwape ushauri.
Mzee Zuzu naendelea kutabiri kuwa kutakuwa na wimbi kubwa la watu kutaka utajiri wa harakaharaka bila kutoka jasho. Wapo watakaoaminishwa kuwa elimu si kitu cha maana sana zaidi ya fedha, hivyo watahitaji fedha kwa nguvu.
Watakwenda kwa waganga wenzangu na kupewa masharti magumu ya kuua walemavu na hata watoto. Tutakuwa na kundi kubwa la vijana majambazi watakaoamini katika kuvuna bila kupanda.
Nchi itagubikwa na mtihani mgumu wa rushwa ambao kutatua kwake itakuwa ni vigumu kutokana na mfumo utakaokuwapo wakati huo. Hii inatokana na mwenendo tunaokwenda nao kwamba kizazi cha watoa rushwa hakitazaa kizazi cha wakataa rushwa.
Nahofia madhara makubwa zaidi kwamba rushwa inaweza ikafika mahala ikawa hata katika kaya ya familia kunahitaji kutoa chochote ili jambo fulani likamilike.
Kutokana na rushwa, mambo mengi ya msingi yatafinyangwa, makandarasi watatengeneza barabara mbovu, wana usalama wataangalia mkono mrefu zaidi kuliko sheria, leseni zitatolewa kama njugu, hata mimba zinaweza kupewa leseni na matokeo yake ni vifo vya ajali kila siku kama vile hatuoni.
Huu ni ubashiri unaoweza ukaanza mara moja. Na kwa kuwa nchi hii itaamini zaidi katika biashara, na si kilimo na viwanda, basi itaalika wageni wengi kwa mgongo wa uwekezaji hata kama hawana fedha.
Watawekeza kupitia nguvu za wazalendo kwa malipo kiduchu, watawanyanyasa wenye ardhi yao kwa maelezo ya uwekezaji na kwa kuwa mdudu rushwa atakuwa amekithiri, hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya wawekezaji hao.
Baada ya miongo michache vilembwe vyangu vitagundua kuwa nchi hii iliwahi kupata Uhuru wake katika karne ya 20 miaka ile mingi iliyopita, lakini Uhuru huo utakuwa haupo tena. Tutaamuliwa mambo yetu na watawala wapya tuliowakaribisha kama wawekezaji.
Kutokana na matatizo hayo na mengine mengi yatakayosababisha wapigania uhuru waongezeke maradufu na siasa uchwara, wananchi masikini watakata tamaa ya maisha na kutotaka tena mambo ya siasa.
Hivyo kwa kosa hilo, mfumo mzuri wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kwa nia nzuri ya kuleta upinzani kwa mtawala aliyeko madarakani, utakufa na hapo ndipo mwisho wa demokrasia ya kweli utakapokuwa umetimia kwa mujibu wa maono yangu.
Kwa sababu nitaendelea kutabiri ili Mabwepande ikamilike vizuri, namalizia kwa kutabiri mambo mawili zaidi. Kutakuwa na pengo kubwa sana la wenye nacho na wasionacho.
Hawa ni wanaojiita wazawa na wawekezaji ambao kimsingi watakuwa raia wa nchi hii kutokana na mfumo wa utendaji wetu wa kazi ulivyo, kwamba anayetaka uraia anaweza akapata bila pingamizi.
Masikini wa nchi hii atakuwa ni yule aliyetenda haki katika utumishi, uzalendo na kupigania Uhuru. Hatakula matunda ya taifa lake kwa kuwa walaji wajanja watakuwa wametangulia mbele ya kisheria na uamuzi ambao yeye hana pingamizi nao.
Mwisho, lakini kwa leo kwa vile nitaendelea kufanya utabiri, nchi hii itaunga mkono suala la ushoga ili kukamilisha masharti na vigezo vya hao wanaoitwa wafadhili wetu.
Tutakubaliana na ndoa za jinsi moja na huenda hata mimi na uzee wangu huu nikatolewa posa na kijana mdogo kwa vile ana rungu la fedha na mamlaka juu yangu. Nikikataa watatumwa wanaume wa kazi nipelekwe Mabwepande ili iwe mwisho wa historia yangu.
Wanangu, wakati huo watakaokutana na maswahibu hayo vitakuwa vilembwe vyangu. Naomba nikiri wazi kuwa sitakuwa tayari kushuhudia Sodoma na Gomara yenu kwa kisingizio cha kwenda na wakati, kwamba unazaa mtoto wa kiume ambaye hujui ataoa au ataolewa.
Najua wapo watakaoniita mchawi, lakini naomba nisichomwe moto nipelekwe Mabwepande nikapate hukumu ninayostahili. Hii ya kuchomwa moto nitakutana nayo ahera.
Wasaalam,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.