Wiki iliyopita niliishia kuwaeleza uzalendo wangu wa kuwa mtunza stoo ya kijiji hasa kipindi kile ambacho tulikuwa katika vita ya kumtoa Nduli kule Uganda.
Ni kipindi ambacho nilikuwa nikikusanya vyakula, mifugo na vijana wanaojitolea kwa kuwaandikisha majina. Sikumbuki ni wapi nilikuwa ninawajibika kutoa taarifa ya nilichokipokea na kuandikishiana na mtoaji. Ninachokumbuka ni jinsi ambavyo nilikuwa nikikabidhi mzigo wote kwa wahusika ili waupeleke Mbarara.
Sikuwahi kufikiria kwamba kuna siku tutafikia nchi hii hata kumkabidhi mtoto wako ada yake ya shule itabidi muandikiane mahali kwa ajili ya ushahidi. Hii ndiyo nchi ambayo mimi na wenzangu tulipata kuishi kwa kuaminiana.
Wakati wote wa vita nilipewa jukumu jipya. Kwanza, kupata mafunzo ya msasa haraka kuwa mgambo mahiri lakini la pili nilipewa jukumu la kuandikisha vijana wanaotaka kupata mafunzo ya mgambo katika eneo letu. Zoezi lile lilinifanya niwe nikihamahama kutokana na uhitaji wa vijana wengi kujiandikisha kisha kupata mafunzo baada ya kuchunguzwa afya zao.
Zoezi la uandikishaji na ukusanyaji wa michango ya wananchi vilikuwa vikienda sanjari huku taifa likiwa katika vita. Majukumu yote yalikuwa yakifanyika kwa moyo mmoja bila kudai malipo ya aina yoyote. Asubuhi nilikusanya michango, mchana niliandikisha vijana kwa ajili ya mafunzo ya mgambo na jioni tulichimba mahandaki.
Baada ya vita kwisha na kuwapokea mashujaa wetu waliorudi salama na kuwakumbuka mashujaa wetu waliokufa kwa kutetea taifa letu, tulisubiri kwa hamu kubwa kusikia kiongozi wetu kwa maana ya rais anatuambia kitu gani kifanyike baada ya kumaliza kazi.
Kwanza, alitupa moyo kuwa baadhi ya vijana wetu walibaki huko kuhakikisha kuwa kunakuwa salama kwa taifa letu, hivyo tuanze kufukia mahandaki yetu huku vijijini.
Kwa kauli moja na ya kiungwana tukajua gharama za vita. Tulijua gharama za vita kwa sababu kila mtu alishiriki kwa wakati na eneo lake. Ushiriki ule haukuwa na umri. Kina bibi na babu walishiriki, kina mama na kina baba walishiriki na vijana kwa ujumla wetu bila kujali jinsia tulifanya kazi kubwa sana.
Ikatangazwa hali ya hatari katika vita ya kuinua uchumi wetu. Vita ile tuliamua kutonunua kitu kutoka nje na badala yake tuuze nje zaidi ili kuweza kulipa deni kubwa la silaha na vitu vingine ambavyo tulikopa wakati tukiwa vitani.
Tulijipangia malengo kutoka katika kamati zetu za siasa za shina hadi taifa na ndipo mwenyekiti alipotangaza miezi kumi na minane ya kufunga mkanda.
Ile miezi kumi na minane kitu pekee ambacho kilikuwa kinaweza kupatikana bila foleni ya heshima wakati huo ilikuwa ni chumvi ya mawe kutoka mashamba yetu ya ndani huko pwani. Lakini chumvi ya kisasa yenye kutibu goita nayo kwa kauli moja tulikataa kuagiza kutoka nje. Huo ndio uzalendo ninaoukumbuka sana kutoka katika kizazi cha maelewano.
Wachache walipewa nishani na wengine tulipigiwa makofi ya kupongezwa kwa kazi kubwa tuliyofanya. Tukaanza mazoezi ya kufufua uchumi wa taifa letu. Tukakubaliana kila mtu afanye kazi. Wakulima waongeze muda wa kulima na wafanyakazi serikalini na mashirika binafsi waongeze saa moja zaidi ya kazi bila malipo, lengo likiwa ni kuzalisha zaidi ili tuuze zaidi katika kipindi kifupi.
Kwa mwenye kumbukumbu kama miye, kwa maana ya wa rika langu, mtakumbuka hali ilivyokuwa ngumu kimaisha kuliko wakati mwingine wowote katika taifa hili. Hatukuweza kunywa chai, kupiga miswaki, kutumia magari ovyo, kuchagua kinywaji, na hata kutembea ovyo bila kufanya kazi. Katika kipindi hicho Baba wa Taifa aliongoza kipindi ambacho baadhi ya watu waliingiwa tamaa na kutaka kufanya mapinduzi.
Mapinduzi yale hayakufanikiwa kwa sababu ya uzalendo wa wananchi. Kila mwananchi alikuwa mzalendo wa kweli katika taifa lake. Tuliwalaani waliofanya mipango ile na kuwaona kama watu waliotumwa kuja kuturudisha katika maisha mengine ya utumwa wa mkoloni mamboleo.
Kwa uchovu wa kazi Mwalimu aliamua kungatuka rasmi katika uongozi ili apumzike. Alikuwa amechoka na sisi tulijua kuwa amechoka na hata sisi tulikuwa tumechoka.
Tuliamini vijana ambao walikuwa hawajapitia madhira yale ya maisha ya miaka ya nyuma kuanzia kudai uhuru mpaka vita na miezi kumi na minane ya kufanya kazi wangetupokea na kuanza kulisukuma gurudumu la maendeleo.
Nini kilitokea mpaka tukafika hapa tulipo? Endelea kusoma waraka wangu mpaka mwisho.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.
Mwisho