Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wote kutokana na kifo cha Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Nelson Madiba Mandela.

Kifo hiki kinanifanya nione ombwe la watu makini duniani likiendelea kuwapo, watu wa watu, wanaojua kuwa wapo kwa ajili ya watu, wanaojua kuwa madaraka ni dhamana na si mtaji, watu waliojitoa uhai wao kwa ajili ya wengine. Poleni sana.

Nimelala na kufanya tafakari kabla sijaamua kushika kalamu na kuanza kuandika waraka huu, kuhusu kile ambacho naona hakitendewi haki katika nchi yetu.

Nasema hakitendewi haki kama Mtanzania mzalendo wa wakati ule, Mtanzania ambaye naweza nikadiriki kusema wakati wetu wa ndege hata wewe Mwakyembe ulikuwa unaweza ukajua kama angani sasa imepita ndege ya Tanzania.

Leo naanza na shutuma moja kwa moja. Kwamba katika hili kuna mkono wa mtu kama si watu wengi, hakuna mjadala katika jambo hili wala kuogopana, haiwezekani nchi iliyokuwa na ndege nyingi wakati wa Ujamaa hadi kufikia ndege 14, leo tubakie na kandege kamoja, tena kadogo! Kuna ugonjwa gani?

Mwakyembe nilipoambiwa wewe ni waziri mwenye dhamana katika  sekta hiyo, nilishtuka, si kwa sababu ni Mwakyembe no, kwa sababu ni waziri ambaye anaweza akafanya kazi katika kiwango cha utendaji na si kiwango cha siasa. Nilipenda dhamana hiyo uliyopewa kwa sababu unatanguliza mbele utaifa.

Tanzania ni nchi gani ambayo hatutaki kujifunza kutoka kwa wenzetu, badala yake tunazidi kudumaa siku hadi siku? Ni nchi gani ambayo tunadhani tunatakiwa kuwekeza hata katika mambo ambayo ni ya msingi kwa Taifa kama mmiliki halali ili kujiwekea mazingira mazuri ya kiuchumi?

Hainiingii akilini ninapoona mataifa mengine, njia kuu za uchumi zinamilikiwa na Serikali, sisi tunaamua kuzibinafsisha. Kama Taifa usalama wetu uko wapi? Kama Taifa mapato yetu ya uhakika katika usafiri wa anga tutayapata kupitia nani? Kama Taifa tunajivunia nini katika usafiri wa anga? Je, ni hako kandege kamoja ama viongozi walioko madarakani kwa sasa hapo ATCL mpya?

Hapana, katika hili naamini kuna mikono ya watu tena mirefu sana, maana hata hiyo ndege moja imegeuka kuwa ya masazo, kwamba baada ya ndege za watu kubeba abiria ndiyo yetu inatumwa kama kuna abiria wamebakia, why? Kwanini hao wawekezaji wasije nyuma ya hako kandege ketu?

Huu ni ushindani wa kibiashara najua vizuri, lakini swali la kujiuliza ni, tuna haki ya kugawana hata kilicho chetu kihalali?

Mwakyembe, suala la nchi kuwa na usafiri wa uhakika ardhini, majini na angani si suala la majadiliano, na si suala la kuhitaji kuliacha kwa wawekezaji, wao wawe washindani na Taifa, lakini tusiwamilikishe wafikie hatua ya kutuloga namna hii, inakera sana!

Tanzania maskini ya miaka ya 1970 ya wasomi wa ngumbaru iliweza kumiliki usafiri wa uhakika wa reli, anga na ardhini, na Tanzania ya leo yenye wasomi wa Phd tunashindwa kumiliki nguzo hiyo ya kiuchumi huku tukisema bila kuwa na rasilimali hiyo Taifa haliwezi kusonga mbele!

Tanzania imejaa siasa. Suala la ununuzi wa ndege japo kumi na tukashika njia muhimu kwa Taifa letu ndani na nje inawezekana ni suala la uamuzi wa dakika chache kwa viongozi makini wanaoweza kuweka siasa kando ya uamuzi makini.

Kwa kufanya hivyo hatutakuwa tumewapa nafasi watu wachache kumiliki uchumi wa nchi na kuuyumbisha wanavyotaka wao. Tunajifunza mengi kwa kuyaona, lakini hatutaki kuchukua hatua madhubuti kukabiliana nayo. Tumeona migomo ya usafiri wa mabasi ilivyowakera wananchi, wenye mabasi wanataka bei yao na Serikali inaona uchumi wa msafiri ni mdogo, umaskini unazidi kutandawaa kwa huyu mwenye nchi. Zamani tulikuwa na Kamata, UDA, Relwe, na kadhalika.

Tumeona migomo ya malori na nguvu yao katika sekta ya usafirishaji wa mizigo. Mwenye kumbukumbu atakumbuka miaka yetu ya elimu ya ngumbaru tulikuwa na magari ya Serikali na ushirika mangapi na leo baada ya hizo Phd tunayo mangapi. Je, haya ndiyo maendeleo?

Je, tunataka kuona migomo ya usafiri wa anga na nguvu yao katika sekta ya usafirishaji?  Ni kweli kwamba ifike mahali kama Taifa tuanze kuwasujudia wawekezaji hata katika mambo muhimu kama ya usafiri huo? Tanzania yenye Phd nyingi leo tunakwenda wapi?

Nchi ndogo zenye maliasili chache zinaweza kumiliki ndege kadhaa, sisi tunashindwa nini Mwakyembe? Tafakari, chukua hatua na mjiulize.

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.