Siyo kwamba mimi ni mzee sana kiasi cha kushindwa kuwa mpenzi wa masuala ya soka au muziki, la hasha. Pia ni mpenzi mkubwa wa soka, tena nikiipenda Simba kwa hapa nyumbani tangu zamani na sasa naipenda Mbeya City kama timu yangu ya mtaa.

 

Pia katika Ligi ya Uingereza naipenda sana Asernal pamoja na mateso yake, kule Hispania naipenda Real Madrid na Ujerumani naipenda Borrusia Dotmund. 
Katika ulimwengu wa soka bado mimi nimo, sikuishia kupenda timu za zamani kama Sunderland ya Tanzania au Cosmo pia ya Tanzania, Walsall ya Uingereza na Porto ya siku nyingi kule Ureno. 
Naupenda muziki wa kizazi kipya, lakini ule unaoghani mashairi ya mafunzo, mashairi ambayo hayana nafasi ya kutangaza mapenzi au mambo ya kihuni, nawapenda wanamuziki ambao hawajioneshi umaarufu kwa ujinga wao, lakini kutokana na kazi yao, napenda miziki karibu yote ya zamani, naipenda miziki iliyopigwa wakati wa sherehe zetu za Muungano, nilifarijika sana. 
Nazipenda sana filamu, ambazo nilianza kutazama nikiwa bado mdogo, nilikuwa natizama katika viwanja vya mpira, leo naangalia filamu nikiwa ndani ya nyumba tena kwa kuchagua ninayotaka, tofauti na zamani ambapo tulikuwa tukitazamishwa filamu ambayo haituhusu, lakini ilikuwa bado ni burudani tosha ya akili. 
Filamu za zamani zilikuwa ni za Kilimo cha Kisasa, Maadui wa Afya, Urafiki na China, Ujenzi wa Reli, Fimbo ya Mnyonge, Chale Chapline, na Chale Mbwambwambwa na nyinginezo. Hatukupata kuona mapenzi hadharani, tuliona kilimo ambacho hakituhusu kijiografia, lakini tulifurahi sana kuwaona Watanzania wenzetu wakifanya kazi kwa ushirika. 
Nimeamua kuweka bayana mambo yangu binafsi kwa sababu kubwa moja; kuieleza dunia kwamba ni watu wachache unaoweza kuwaweka katika kundi la watu wasiojua. Vijana wengi wa leo wanadhani kwamba wao wanajua na sisi hatujui kitu na labda tumepitwa na wakati. 
Baadhi ya vijana wa leo wamefika mbali zaidi na kuleta dharau na kutuona kama watu wa zamani hatujui kitu, leo mmewadharau wazee kama mimi na mmekosa ushauri na maarifa katika mambo mengi ambayo mmeanza kushindwa kuyatekeleza. 
Mmedharau wazee na hatimaye hamna timu nzuri ya riadha na sasa ni kichwa cha mwendawazimu, tuliofanya jitihada ya kuwatayarisha vijana wenzenu wa zamani ambao waling’ara miaka hiyo na kuliletea sifa Taifa la Tanzania. Sisi ndiyo tulioweza kuifikisha timu ya Taifa hadi katika kiwango cha timu bora Afrika miaka hiyo, lakini leo ni kichekesho! 
Sisi ndiyo tulioweza kulima na kuwa na chakula cha akiba kugawa kwa wananchi wenye njaa na mataifa mengine yaliyokumbwa na tatizo la njaa, ni kutokana tu na sinema zile za kilimo bora, hatukuwa na vipeperushi vya kilimo kwanza wala kuhamasishwa kwa mashairi na wanasiasa. 
Leo mna Taifa la wasomi na mlio wengi kwa idadi ya sensa, lakini ndiyo Taifa lenye njaa na kukosa akiba ya chakula ya kuwasaidia wenzenu. Nahisi ni kujua kulikopitiliza miongoni mwenu, hamna kitu kikubwa mnachoweza kujivunia zaidi ya kuwa na kundi la wajanja wanaoweza kuishi kwa mali kauli! 
Katika hali ya kawaida, kuwalaumu watu wa zamani kama wasiojua kitu ni kudhihaki uwezo wao wa kuelewa mambo kwa wakati wao. Tulileta uhuru, wapo wanaodai kuwa tuliwahi sana ilibidi tuchelewe kidogo, tumefanya jitihada za Muungano na kutengeneza mazingira mazuri ya maelewano, ninyi dot.com mmekuja na ajenda ya kuupinga Muungano tena kwa hoja mnazoziita za kisheria. 
Tuliamua Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na tukaleta Azimio la Arusha, lakini matokeo yake ni kundi la vijana kuamua ambacho mnadhani ni cha maana kuliko tulichodhani sisi kwa wakati wetu kuwa cha maana kwenu. 
Kwa ufupi ni kwamba hata mnachokipenda ninyi leo sisi tulianza kukipenda kabla, mnachojua leo sisi tulikijua siku nyingi, mnachotaka ninyi, sisi tulishakipata isipokuwa haya mawazo kwamba hatuna tukijuacho yanaweza kuwafanya mkakosa hazina kubwa tuliyonayo katika vichwa na uzee wetu.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.