Kama siku zote ninavyosema salamu ni ada, na ni uungwana kujuliana hali, nawashukuru sana wote wanaonitumia ujumbe wa simu kunieleza yale ambayo yamewakuna.
Hata kama litakuwa si jema kwako, naomba unijulishe ili nijue kuwa nimekukera, sisi ni binadamu, hiyo ni hatua ya maisha na lazima niipitie ili niweze kukiri, hakuna binadamu mkamilifu, karibu wote ni dhaifu.
Kuimaliza wiki ukiwa salama si kitu cha mchezo, na ukiona unamaliza wiki haujafikwa na mtihani wa mawazo ujue bado uwezo wako wa kutafakari ni mdogo. Katika maisha haya msongo wa mawazo lazima ukufike na matokeo ya msongo ni mengi.
Unaweza ukavuka barabara ukakutana na magari, unaweza ukaingia nyumba ya mtu bila kujua, pia unaweza kuingia majaribuni ukachukua kitu cha mtu, kwa maana ya kuiba mali ya mtu kwa kisingizio cha kupitiwa na shetani.
Leo nimewaza mengi. Kwanza ni wiki ya Pasaka, wiki ya mwendelezo wa toba zetu. Lakini pia nimerudi nyuma miaka mingi sana, nikakumbuka enzi za nyumba yetu na jirani wa mbali, enzi hizo nyumba yetu na jirani ilikuwa kama kilomita moja hivi, si kama leo, jirani mnagombana kwa mpaka wa mita moja, haya ndiyo maajabu mengine ambayo nayaona katika kipindi kifupi cha miaka kama sitini tu.
Kuna tofauti sana ya maisha yetu ya zamani na siku chache zilizopita, sasa hivi maisha yamebadilika. Kama ingekuwa ndiyo tunapata uhuru, ningesema haya ndiyo mambo ya kujitegemea, lakini tulishapata uhuru na tukautumia vibaya bila kujua kuwa uhuru ni kazi kama ilivyokuwa kaulimbiu yetu enzi zile. Tukageuza uhuru ni kukaa vijiweni na kupiga soga, tukafanya uhuru ni kugawana mali za umma na uhuru ni kupiga dili.
Maisha sasa yamekuwa ya bajeti, kuanzia serikali kuu hadi serikali za nyumba, kwa maana ya baba, watoto na wajukuu. Yaani kwa ufupi, hakuna kitu kinachoshikika bila kutoa jasho, na hili linataka kuwa sanjari na agano letu la uhuru enzi zile, tulisema tunataka tujitegemee na dalili za kujitegemea naziona, sasa hivi mambo yamekuwa si ya leo tena, tunarudi kwenye mazingaombwe na utapeli uliosahauliwa, baadhi ya wavivu wameamua kubuni njia mpya za mapambano ili mkono uende kinywani. Hata vibaka hawaoni kitu cha kuiba kwa kuhofia thamani ya anachoiba na damu atakayomwaga.
Nimefurahi sana, yale maisha ya lete kama tulivyo huko baa, sasa hivi yanafanyika nyumbani kwa familia zinamwagwa soda za kugawana na watoto na mama chanja, upendo umeshamiri hata kama kuna ugomvi ni wa hapa na pale na unahusu fedha na si kitu kingine.
Viongozi wa dini hawana kazi kubwa kama zamani ya kupatanisha ndoa kwa sasa hivi. Kiufupi msemo wa mjini kwamba mshambuliaji karudisha mpira kwa beki ili wajipange sasa naelewa maana yake nini.
Jinsi mambo yalivyo ni kama kuna kamati maalumu ya roho mbaya, lakini ndiyo uchumi inawezekana unataka hivi, yale mambo ya kuwa na fedha bila kufanya kazi kwa kutoa jasho hakuna tena. Yale mambo ya kukaa kijiweni na kufungua ofisi za udalali ndiyo kwisha kabisa, hata ule mtindo wa kuwa makuwadi na kupata cha juu naona kama umezikwa rasmi, kiufupi mizizi ya nyumba ndogo na vibeniteni ndiyo inafukuliwa na kuchomwa moto, ukisikia mwisho wa dunia ya Tanzania kwenye utegemezi ndio huu.
Nadhani hata matatizo ya migongo ni lazima yatakwisha, kwa sababu yale mambo ya kukunja milioni na kukalia hayapo tena, yale mambo ya kutofanya mazoezi naona yanapotea, sasa hivi kila mtu ni mazoezi na vyakula vya asili, ni mambo ya tiba mbadala na ushauri nasaha, maisha yanabadilika upesi sana.
Mimi nipo huku shamba, napata taarifa za mjini, najua mnaniomba niwaombee kitu. Kama babu ninasema mkuu ukiweza legeza kidogo, ikiwezekana dalili za mbwa kumla mbwa naziona, tulioishi miaka mingi tunajua njaa ya miaka ya sabini. Watu wako wameanza kunyooka na kujua thamani ya kufanya kazi kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yao, vinginevyo watalamba reli hawa watu.
Najua unajua mkuu kuwa kwa mara ya kwanza tangu uhuru Mtanzania mpiga dili naye anapitisha bajeti ya wiki sasa kama serikali inavyopitisha bajeti ya mwaka wa fedha.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.