Kuna wakati ambao ninawaza mpaka kichwa kinataka kupasuka, si kwa sababu yanayoendelea siyajui, la hasha! Bali ni kwa sababu yanakwenda kasi mno na kuniacha nikiwa bado njia panda. 

Maisha ni safari ndefu na ukibarikiwa umri mkubwa unafanikiwa kuyaona mengi na kuna wakati unatamani kutenda kama ambavyo akili inataka lakini mwili unakataa.

Miaka ya mwanzoni, wakati vyama vya wafanyakazi vikiungana ili kuwa na nguvu moja, kulikuwa na hoja mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kikanda wa vyama vya wafanyakazi na lengo lao kubwa la kuleta hoja ilikuwa ni kutotaka kupoteza nafasi zao za ubwana mkubwa katika vyama hivyo.

NUTA ilipozaliwa ilibidi vyama vingine vife na kwa kweli chama hicho kimoja kilikuwa chachu kubwa sana ya umoja wetu wakati huo wa kudai masilahi ya pamoja kama wafanyakazi lakini kikubwa zaidi ilikuwa ni ile mikutano yetu ya social welfare, vijana wengi wa leo wanazungumzia welfare bila kujua imetokana na nini.

Wakati huo ninakumbuka nguvu ya mzee Kawawa katika kuongoza chama chetu. Nakumbuka Simba wa Vita alivyokuwa akiunguruma katika mikutano ya kazi na kupokea ajenda za umoja wa kuanzisha chama cha siasa. Ni wakati huo ambapo yeye nusura apoteze kazi, lakini pia ndio wakati ambao Julius Nyerere aliambiwa achague jambo moja analoona anaweza kufanya, kufundisha au kuwa mwanasiasa.

Sihitaji kurejea sana kwenye historia lakini itoshe kusema kuna watu waliweka rehani maisha yao kwa ajili ya taifa hili. Hawa wote wametangulia mbele ya haki wakiwa ni maskini tu wa mali lakini matajiri wa roho ya uzalendo. Hatupaswi kuwasahau hata kwa sekunde moja wakati tukizungumzia taifa hili.

Wapo wengi lakini kuwataja sitaweza ila naomba radhi na ninawatambua wazee wale ambao walijitolea kuliko roho zao ili mimi na wewe tuliokuwa katika maeneo yasiyotambuliwa tuwe huru na tujitegemee. Suala la utumwa kwa kizazi hiki nadhani limeanza kupitwa na wakati na wengi hawajui hata madhara yake na maana yake hasa.

Sasa hivi naona mipasuko katika vyama vya siasa. Sina hakika kama mipasuko hii inataka kulingana na ile ya wakati ule miaka ya 1950 wakati vyama vya wafanyakazi vikiungana na wengine wakiombwa wakae pembeni ili mmoja awe mbele kwa niaba yetu.

Walikuwapo waliokataa kwa sababu walijua kuwa kukaa kwao pembeni kutawatoa katika fursa ya kupata ulua na pengine heshima tu, wapo waliotusaliti na wapo waliofanya mipango wakabaki huku wakijua sifa hizo hawana.

Leo tunazungumzia miaka zaidi ya sabini iliyopita, waliopo hai ni kama tunakula pensheni ya umri, maana hatuna hata msaada wa maana zaidi ya kuwa mzigo, msaada pekee tunaoweza kuufanya ni kutoa ushauri tu pindi tunapoombwa na inapobidi.

Leo baada ya miaka yote hii kuna watu ambao wanafikiria madaraka badala ya kufikiria uhuru ambao tuliupata ili tuufanyie kazi. Leo baada ya miaka yote hii kuna watu hawajui juu ya utumwa, bali wanafikiria juu ya kutumia uhuru kujinufaisha katika mchezo uitwao siasa.

Kuna kundi kubwa sana ambalo limejikita katika siasa za ubabaifu, kusema maneno ambayo yanataka huruma ya wananchi katika kuwaweka madarakani, kuna kundi kubwa ambalo ni fuata upepo, halipo kwa ajili ya manufaa ya watu ambao wameahidi kuwaongoza kuwapeleka katika nchi ya Canaan.

Wanasiasa wa hivi ni ovyo sana katika taifa lolote. Ni wanasiasa malaya ambao wanaweza kutuuza muda wowote. Ni wanasiasa ambao wanaamini wao walizaliwa kuja kuongoza wengine, si kuongozwa. Wengi wao wapo tayari kusema uongo na kufitinisha watu ili wao wapate nafasi ya kuongoza.

Sisi watu wa zamani tunaamini uongozi ni karama. Kiongozi anayepatikana kwa kuchaguliwa na watu ni kiongozi aliyechaguliwa na Mungu. Lakini kiongozi anayekataa kuchaguliwa bali anajichagua ama kwa kutotaka uchaguzi au kwa kutumia fedha, huyo lengo lake si sawa na lile ambalo lilitufanya miaka ya 1950 tuungane kudai Uhuru.

Nakubaliana na masuala ya kuhama vyama, lakini ninajiuliza, wataridhika kukaa bila madaraka? Nakubaliana na wanaong’atuka, lakini je, wako radhi kutoa ushauri mwanana kwa wengine?

Wakati tukiwa katika mchakato wa vyama vya wafanyakazi, tuliwaza kuhusu uhuru, lakini leo kuna watu wanawaza kuhusu mshahara, ukubwa, mali na koneksheni; haya jamani mimi ni TANU Youth League wa mwanzoni, suala hilo silielewi, ni kama akili inataka lakini mwili unakataa.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.