Anaamka asubuhi kama mbwa koko anayefikiria siku hiyo itaishaje na rizki yake iko miguuni mwake, ni sala tu ya Muumba wake kumuamsha akiwa na siha njema pasi na maradhi ya kumlaza kitandani. Ni Mtanzania mwenye haki zote za kibinadamu; ana mke na watoto, ana wazazi na wategemezi kadhaa.

Anaamka akiwa hana chapa ya senti kwa kuwa mguu wa jana ndiyo ulioifanya familia ikalala bila kutazama paa. Anaamka akiwa ametetewa na vyama vyote vya kazi, kama ni mwajiriwa basi katetewa na vyama vya wafanyakazi na kama si mwajiriwa basi katetewa na vyama vya haki za binadamu.

Ameamka akiwa maskini kama jana, na atalala akiwa maskini kama leo, ndoto za kubadilisha maisha na kuwa na uafadhali ziliisha alipoamua kuoa na kuanza maisha ya familia, kwa kuwa angeamua kusubiri mafanikio ni dhahiri asingeweza kuoa na kuwa na familia yake.

Mheshimiwa Rais, huyu ndiye Mtanzania anayekutambua wewe kuwa mkombozi wake katika maisha magumu yanayomkabili kila iitwapo leo, ni mpigakura wako, ni mtu wako ambaye anakutegemea kwa utengamano na amani katika nchi hii.

Mtu huyu anaamka akiagana na nyonga kwa ahadi kedekede anapoondoka ndani ya banda linalofanana na kuanguka muda wowote, anaitazama familia yake kwa matumaini makubwa lakini si matumaini yake ni matumaini ya watoto wake walioondoka kwenda shule kwa kifungua kinywa cha mkandaa. Anamuomba Mungu isitokee dharura ya aina yoyote kabla hajatia kibindoni akiba ya mlo wa siku hiyo.

Mke anaanza na mtaji wa kodi ya meza ya shilingi elfu kumi ambayo imeachwa na mume jana usiku, atanunua maji japo madumu manne kwa shilingi elfu mbili ili wapate kupika, kufua, kunywa na kuoga japo mara moja kwa siku, atapita sokoni na siyo buchani kupata mboga ya kulazimisha kushushia ugali kama mlo kamili wa mchana na jioni, hapo itamgharimu kama elfu mbili nyingine.

Atakwenda dukani kununua unga nusu na robo kwa ugali wa mchana na jioni ili sala ya jioni kumshukuru Mungu iwe na maana kwa kuipitisha siku hiyo, elfu mbili nyingine inahusika katika muamala huo wa unga, ataiweka elfu mbili nyingine kwa ajili ya usafiri wa mumewe kesho kwenda kutafuta riziki ambayo haijulikani kama itapatikana ama la.

Elfu mbili ya mwisho kukamilisha mizania ya elfu kumi itakamilishwa kwa mahitaji madogomadogo muhimu kama mkaa, mchango wa luku, dawa ya jiko, panadol ya mume, viungo vya mboga, na michango midogomidogo ya shuleni ambayo watoto wataagizwa.

Huyu ndiye Mtanzania ninayemjua mimi kiuhalisia, Mtanzania asiye na mjomba fisadi na mwajiriwa serikalini kwa kima cha chini ama cha kati, ana watoto wanne wanaosoma wakimtegemea, ana mke ambaye ni mama mjasiriamali asiye na mtaji wa kumuwezesha kufanikiwa katika biashara yake.

Ana ndugu wanaomtegemea katika ada, harusi, misiba, maradhi na kadhalika, ana majirani wanaohitaji michango ya maendeleo ya mtaa, anatakiwa kushiriki mambo ya ibada na kutoa zaka kila iitwapo siku ya Mungu, anahitaji mavazi, sabuni, mafuta na mahitaji mengine.

Anahitaji kuweka akiba japo ya dharura lakini hawezi, anahitaji kubadili mlo japo mara moja kwa wiki lakini ni mtihani mgumu kwake, anahitaji kuwasaidia wazazi wake lakini wanawe wanamuelemea, anahitaji kuwa na ziada ya maendeleo lakini anapiga hatua moja mbele na mbili nyuma.

Sala yake kila iitwapo leo ni kumuomba Mungu amuepushe na maradhi yeye na familia yake na hata ndugu, ibada imekuwa kimbilio lake, amejikuta akisubiri miujiza isiyotokea kutokana na roho yake kujaa chuki  za maisha.

Mtanzania huyu anasubiri kauli ya kinywa chako kuongeza mshahara na kudhibiti mfumko wa bei katika bidhaa muhimu kwake, anasubiri hatua kali unazochukua zenye nasaba na ahueni ya maisha yake, anapata hasira anaposikia mwingine akijilimbikizia mapato kwa namna ya wizi, anakunywa panadol aliyotayarishiwa na mkewe mchana na kulala.  

Pigana uwezavyo Mheshimiwa Rais Magufuli, lakini  hawa ndiyo Watanzania niwajuao mimi, ukiwaona kwa nje ni fahari ya Taifa lakini kwa ndani mioyo yao imepondekapondeka kwa ugumu wa maisha, wafanyie wepesi kwa kuwa jicho lao linakutazama zaidi ya kumuona Rais.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.