Siku mbili tatu hivi uliposema kuna watumishi wa Serikali wanaishi kama malaika, tulikuelewa kwamba unaelewa kinachotukera waajiri wao ambao ni sisi wananchi. Tulielewa kuwa kero yetu imekufikia na wewe ndiye tuliyekuajiri uwe bosi wao na unatakiwa ujue nini mahitaji yetu.

Mpaka leo tuna imani na wewe meneja wetu kwamba hii biashara  ya kuiendesha hii biashara ya serikali ili iweze kuwa na tija na maendeleo, tulikuwa tunahitaji mtu wa aina  na kaliba yako kwa sasa. Tunaelewa kuwa una kazi kubwa na nzito ambayo kamwe huwezi kuifanya peke yako na ndiyo maana tukasema teua timu yako itakayokusaidia kuikamilisha vema.

Mpaka sasa hakuna tatizo, lakini tatizo linaloweza likawa kubwa sana kuonesha kwamba timu yako inashindwa kukusaidia ni matatizo ya kuvuka daraja la awamu moja kwenda awamu nyingine. Kuna tatizo la mazoea ya watumishi kutoka awamu zilizopita na awamu ya mabadiliko ya utumishi kutoka kwako.

Mheshimiwa, ulipokuwa ukisema unataka kuwatumikia wananchi wengi hawakukuelewa, uliposema unataka kutumbua majipu sugu kuna watu hawakukuelewa unamaanisha nini, leo wameanza kukuelewa na wanaokuelewa vizuri ni wale unaowatumbua na wanaosubiri kutumbuliwa, hutumbui kwa nia mbaya unatumbua kwa ajili ya maisha halali ya kwetu tuliokuajiri.

Mheshimiwa, majipu ni mengi mno, kwa ufupi huwezi kutumbua peke yako, unahitaji usaidizi wa kweli bila haya kama ambavyo wewe unafanya, unahitaji kuambiwa kwa kuwa majipu ni mengi mno na yapo sehemu nyingi na nyingine zilizojificha sana.

Wenye wajibu wa kufanya hivyo ni sisi wananchi wenyewe tuliokuajiri, hii siyo kazi unayoweza ukaifanya kwa ufanisi pekee yako, inatakiwa sisi tukushike mikono na kukuonesha maovu yanayofanyika katika sehemu zetu za kupata huduma, tukitegemea wewe uwe mfalme njozi, baada ya miaka kumi utatoka Ikulu ukiwa umeacha nusu ya majipu; na bila shaka zaidi hutakamilisha malengo yako.

Nia njema uliyonayo dhidi ya wananchi itaishia kuwa lawama kwako kwamba ulikuwa nguvu ya soda kutaka kufanya kazi, na mwisho wa siku utaambiwa umenunuliwa. Hili nalisema kwa kuwa nawajua waajiri wako vizuri kwa kubadilisha maneno, nawajua waajiriwa wetu wengi kwa kujaribu kukurubuni kwa njia za kukupoteza.

Nakupa ushauri wa bure unaoweza, kwa namna moja ama nyingine, kukuonesha majipu bila kuyatafuta.

Mosi, fungua ofisi maalumu ya kuletewa taarifa kwa njia za siri juu ya majipu, ajiri wapokea taarifa na kukupa wewe au ofisi yako, sifa kubwa ya waajiriwa wa ofisi yako iwe wacha Mungu, wenye kukerwa na madudu ambayo wewe yanakukera, wawe wasiri na wenye kuleta taarifa mapema sana juu ya meza yako ili yafanyiwe kazi na vyombo vya uchunguzi ambavyo wewe unavisimamia. Wawe wenye kukerwa na maovu kama ambavyo wewe yanakukera, ukiwatazama usoni waoneshe kuwa wanakerwa.

Pili, weka uwiano wa utumishi wa umma, wasiwepo miungu-watu, futa posho ambazo kila mtu alistahili kuwa nazo lakini kwa sasa kuna tabaka maalumu linalofaidika na posho hizo, posho za ukuu wa idara ambazo kuna mahali zinazidi mshahara, posho za vikao vyao wanaojiita wakubwa, futa,  hiyo ni sehemu yao ya kazi.

Futa posho za nyumba, gari, mawasiliano, kukaimu na kadhalika. Angalia uwiano wa mishahara katika ngazi za utumishi na utaona kuwa hilo ni jipu kubwa linalowafanya watumishi wengine kutokuwa na morali ya kazi. Imarisha mabaraza ya wafanyakazi ili waweze kuwa wawazi kwa hao wenye kuamua mambo yao kinyemela, punguza madaraka ya hao wanaojiita wakubwa na kujiona marais katika taasisi, idara, kampuni na mashirika yetu ya umma.

Tatu, kila anayepatikana na hatia awekwe hadharani na ahukumiwe na Mahakama kwa makosa yake, hii ni nchi yetu na wao ni kama sisi, tuliwapa dhamana na wameichukulia dhamana kimakosa huku wakijua wanafanya makosa.

Kila wakati nitajaribu kusema lile ninaloliona linaweza kuisaidia Tanzania yangu, Tanzania ambayo niliifahamu tangu wakati wa uhuru na utumishi uliotukuka, Tanzania ambayo ilikuwa inajitegemea, Tanzania iliyoheshimu misingi ya utumishi wa umma.

Mungu ibariki Tanzania mpya, Mungu akubariki Magufuli, Mungu wabariki Watanzania wenye Tanzania yao.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.