Leo naandika waraka huu kwa mara ya kwanza kuwakumbuka akina pangu pakavu kauka tukuvae, kila mwaka tarehe hii ya mwanzo wa Mei huwa ni hatima ya furaha ya mfanyakazi yeyote, wengi huishiwa na amani na furaha na wapo ambao hujaa furaha bila sababu. Ni wivu tu wa mtu mmoja mmoja.
Tarehe hii huadhimishwa duniani pote sanjari na kuonesha mafanikio ya kazi ambayo yameweza kufanywa kwa mwaka mzima. Ni tarehe muhimu kwa wafanyakazi kuonesha mshikamano wao dhidi ya mwajiri na dhidi ya mapato yao.
Sitaki kuzungumzia mambo ya huko duniani kwingine pangu pakavu pananisubiri nipavae. Tangu tupate uhuru wa Taifa letu, siku hii adhimu kabisa imekuwa ni maalumu kwa ajili ya kusubiri tamko la mwajiri juu ya hatima ya upandishwaji mshahara, suala la kupandisha mshahara ndilo lililojikita katika vichwa vya Watanzania wengi, wengi wetu tunaangalia kama nyongeza ya mshahara kuwa nafuu ya maisha yetu.
Kitaalamu nasikia kuwa ongezeko la fedha mikononi lina athari kubwa kiuchumi, na nyongeza yoyote ya mshahara inamaanisha kuongeza fedha mikononi mwa watumishi ambao bila shaka kabisa linakwenda moja kwa moja mitaani kwa wengine, si kweli kwamba tutakuwa tumetatua tatizo la kumsaidia mfanyakazi kupambana na ugumu wa maisha la hasha huenda tukawa tumeongeza matatizo.
Leo ninaandika baada ya kuwa na kumbukumbu nyingi sana za mishahara ya waajiriwa wa Tanzania. Dhana ya mshahara ilianza kuonekana miaka ya 1980 baada ya kuanza kukaa mbali na dhana ya ujamaa, thamani ya fedha ilianza kuja kwa mtu mmoja mmoja kwa maana ya kujitengenezea maisha yake na familia yake.
Yalipoanza maisha ya kutegemea fedha ndipo thamani ya ajira ilipoanza kujitokeza, taratibu suala la kujiajiri lilianza kupotea, ukulima na ufugaji ukawa unaanza kupotea katika fikra za vijana wenye nguvu na ambao walipaswa kuwapokea wazee wenye kulemewa na nguvu za kulitumikia Taifa kwa maana ya kuzalisha kutoka mashambani.
Kelele za mishahara haitoshi zilianza kusikika, na ilikuwa ni kweli kwa sababu fedha ziligeuka kuwa uti wa mgongo, fedha zilikuwa ndiyo nguzo ya utatuzi wa kila kitu, mambo yakaparaganyika katika sekta mbalimbali na kugeuza fedha kuwa muhimili mkuu wa kuendesha maisha ya kawaida kwa kila binadamu, fedha ikawa moja ya alama za mafanikio.
Tulipoingia katika shimo hili la kuabudu fedha, taratibu tukageuka kuwa watumwa chanya wa fedha, tukawa tunakimbia kutafuta fedha huku tukiacha mashamba na mifugo kama vitu vya shida na ambavyo havipaswi kuangaliwa kwa jicho la pili.
Haya yote yalitokana na msukumo wa waajiri kuwalewesha watu kwamba malipo ya fedha ndiyo muhimu kuliko kitu kingine, kuna kitu nataka kusema lakini nataka mgundue kwa kupitia maandishi yangu, waajiri walitulewesha kwa mishahara ili tuendelee kuwa watumwa kwa kusubiri mshahara, walitufanya tusahau kazi na rasilimali zetu, walipata nguvu kazi iliyopotea.
Lengo langu siyo kudai nyongeza ya mshahara la hasha, ningelipenda kuwashauri waajiri wote kuangalia nafasi ambayo mtumishi anayo katika kuwaendeleza kwa kupata faida, bila kumuwezesha mfanyakazi ni dhahiri kuwa atakuibia ili aweze kukidhi mahitaji yake.
Mwajiri anapaswa kudhibiti mfumko wa bei ili huyu anayemlipa kidogo aweze kustahimili kishindo cha gharama za maisha, mfanyakazi anaweza akakufilisi kwa kukuibia au kutega kazi, kumwezesha mfanyakazi ni moja ya nguzo kuu za kunufaika na nguvu kazi yake.
Tusimfanye mfanyakazi awe anasubiri kauli za waajiri kila Mei mosi, bali Mei mosi iwe ni siku yake ya furaha na kuonesha anaweza kufanya nini kwa mwajiri wake, iwe siku ya kujipambanua kuwa anaweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza, iwe siku ya furaha kuwa mtumishi, iwe siku ya kufurahia utumishi wake na isiwe kinyume.
Mei mosi ni sherehe ya utumishi au kusubiri ongezeko la mshahara, jibu litakuwa limepatikana kwa waajiri kufikiria kuboresha mbinu za kiuchumi badala ya kufikiria kupandisha mishahara, watumishi kusubiri ongezeko la mishahara isiyotosha ni sawasawa na kuendelea kuwaandaa watumwa wa fikra za fedha ni kila kitu.
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.