Nimeamka nikiwa najiandaa kuanza kusikiliza michango ya wabunge inayotokana na hotuba ya Rais John Magufuli, ambayo kwa aliyeisikia anaweza kudhani kwamba michango ya waheshimiwa wengine inaweza kuchafua hotuba iliyokuwa na mashiko zaidi kwa kipindi chake cha kulifungua Bunge mwaka jana.
Kila Mtanzania alikuwa akisubiri kwa hamu kujua changamoto na mpasuko wa hotuba ile itakapotua juu ya meza na kugeuka kuwa ajenda ya kuzungumziwa, kwa maana ya kuipongeza au kuiponda kwa wale wenye mlengo wa kushoto wa kutokubaliana na lolote linalozungumzwa na mtu yeyote aliye tofauti na chama chake.
Watanzania tulikuwa tukisubiri tujue mbichi na mbivu hasa katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wanasiasa wamepotea katika ulingo wa siasa na baadhi wameibuka na wanakuja na gea mpya ambayo hatuijui ina kasi gani.
Wapo wanaoamini kuwa kuna majembe makali zaidi ambayo yameingia baada ya kuyaangusha majembe makali ambayo yalikuwa yakiaminika enzi zile za Bunge la kutishiana nyau na mbwembwe nyingi za kuomba miongozo na taratibu za Bunge kila wakati, hilo tutaliona baada ya hili kwisha.
Hoja iliyopo mezani ni kujadili hotuba ya Rais Magufuli ilhali Televisheni ya Taifa ikiwa haioneshi wanaochangia kwa sura, kila mtu ana mtazamo wake katika jambo hili na ndiyo maana kila mtu ana sababu zake katika kulitetea hili. Serikali imesema inataka kubana matumizi ya fedha za walipakodi kwa kutotoa fursa kubwa ya kulipa mabilioni ya shilingi kwa taasisi yake ya TBC.
Wapo wanaosema wanataka kuwaona wanaochangia, sina hakika kama wanataka kuwasikiliza wachangaiaji. Wapo wanaosema mbona taasisi hiyo ni ya Serikali hivyo wana haki ya kupata habari kutoka katika chombo chao cha Taifa na si vinginevyo. Wapo wanaosema hotuba ile isijadiliwe bila kuwa laivu – zote ni sababu na kila moja ina nguvu yake kutokana na mazingira ya mhitaji.
Serikali imetoa hoja yake na kwa upande mwingine na hasa ukirejea Bunge lililopita, utaona kuna mantiki kwa maana ya kuokoa gharama ya muda unaotumika kutoa hoja za kubishana ambazo kimsingi mwananchi wa kawaida asingependa kuzisikia kutokana na ukali wa maisha aliyonayo, huku wabunge wa wakati huo wakijadili kero zake kwa mbwembwe nyingi.
Lakini, vyovyote iwavyo kila mtu ana sababu yake ya kimsingi, wapo wanaotaka kuonesha kwamba wapo, wapo wanaotaka kujulikana, wapo wanaotaka kuwajua, wapo wanaounga mkono bila kujua wanachounga, wapo bendera fuata upepo, wapo ambao kazi ni kupinga hata kama jambo lenyewe ni la msingi. Hii ndiyo siasa, hasa ya vyama vingi na watu wengi.
Mimi nakubaliana na watu wote kila mmoja kwa hoja yake, nakubaliana nao kwa kuwa nalijua Bunge la kwanza hadi hili la sasa, nalijua Bunge la kwanza ambalo mijadala yake tulikuwa tukisoma katika gazeti baada ya wiki moja, nalijua Bunge la kupata habari baada ya mwezi, nalijua Bunge ambalo tulikuwa hatupati habari zake hadi linapokwisha.
Suala la maendeleo jimboni kwetu tulikuwa tukishuhudia bila kujua kama mbunge wetu ameomba ama la, inawezekana tulikuwa tunadanganywa, hatukujua, inawezekana mbunge alidai kwa nguvu sana, lakini tulikuwa hatujui, siasa ilikuwa ya chama kimoja kwa hivyo upinzani haukuwapo wakati huo.
Sasa tupo kwenye wakati mgumu sana kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo za kisiasa, na mfumo mzima wa kiutawala unaweza kuleta demokrasia inayopitiliza na kusababisha kukwama kwa maendeleo. Siasa ni kazi na siyo propaganda.
Kwa mtazamo wangu na hasa baada ya kuona Serikali imekataa kulipia kuonesha ‘laivu’ kikao cha Bunge, ni vyema tukajiuliza maswali machache ili tuishinikize Serikali kutupa fursa ya kuona vikao vya Bunge, je, vile viti ambavyo waheshimiwa baada ya kuvuta posho vitaendelea kuwa vitupu?
Je, masuala ya miongozo na taratibu itakuwa sehemu ya kikao? Je, suala la ndiyo na hapana litatufanya tuwe na amani sisi wananchi? Matusi, kejeli, ngumi kelele ni shoo ambazo tungependa tuzilipie kwa kodi zetu?
Ima, baada ya kuona kila hoja iliyopo mezani, tujiridhishe kwamba Bunge liwe ‘laivu’, lakini pia haki ndani ya Bunge izingatiwe na waheshimiwa wavumiliane kwa hoja na siyo matusi ili kila mtu aweze kutimiza matakwa yake ya wapiga kura na kunadi chama chake, suala la wengi wape lisiwe kigezo cha kutawala Bunge!
Nasubiri uamuzi wa viongozi wangu kuliona ‘laivu’ Bunge langu au kusikiliza na kusoma baada ya mwezi.
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.