Kuna raha ya matamko unaposikia na hasa kama tamko limetoka kwa anayestahili kutoa tamko ili lifanyiwe kazi, raha ya tamko ni pale linapotekelezeka pasi na kuingiza ujanja wa mjini wa kucheza na maneno. Leo tunashuhudia na kusikia matamko kutoka kwa wahusika wenyewe na mbio zake tunaziona zikifanyika.
Unaposikia tamko, mathalani, walimu wakuu wote waliosababisha kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne wachukuliwe hatua za kinidhamu hapohapo walipo ikiwa ni kushushwa vyeo na kubakia maeneo hayohayo ya shule, inatia moyo kwa wazazi ambao watoto wao bado hawajafanya mitihani, lakini inamtia huzuni mwalimu ambaye amechukuliwa hatua kutokana na tamko lililotolewa.
Matamko yanayohusisha utendaji wa nafsi zaidi ya moja ni hatari sana kwa sababu kuna maswali mengi ambayo tunapaswa kujiuliza nyuma ya pazia kabla ya kuchukua hatua, huu wa walimu ni mfano tu ambao nimeutoa kutokana na matamko, lakini maswali tunayopaswa kujiuliza kutokana na matamko hayo ni mengi.
Mathalani, kwa walimu waliosababisha wanafunzi wa kidato cha nne wakafeli, tumejiuliza nyuma ya pazia maswali haya? Kulikuwa na motisha gani kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kutoka kwa walimu wao kwa masomo tofauti tofauti?
Walimu walikuwa na moyo kiasi gani cha kuifanya kazi yao waipende na kusababisha watoto waipende shule na masomo? Je, wanafunzi mmoja mmoja walikuwa na msingi gani wa kusoma tangu awali na nafasi ya wazazi iko wapi katika kuwasisitiza wasome, huyu mwalimu mwajiri wake amemtengenezea mazingira gani ya kumfanya aipende kazi yake?
Hapa nakumbuka baadhi ya matamko ya wenye dhamana kwa walimu kwa miaka kadhaa na matokeo ya kutotekeleza mahitaji yao au kusuasua kwa kutekeleza kutokana na kutokuwa na rasilimali fedha za kutosha. Fedha ni tatizo katika mambo mengi kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi wa nchi yetu, baadhi ya watoa matamko hawaangalii uwezo wa kuzikabili changamoto zilizopo.
Matokeo yake baadhi ya walimu wameingia katika mtego wa kuadhibiwa kutokana na makosa ya watu wengine, huu ndiyo utaratibu wa utendaji mahali popote duniani kwamba mkuu anahusika moja kwa moja na makosa ambayo yametokea chini yake, huo ndiyo uwajibikaji lakini kwa upande wa pili tumeangalia suala la uwezeshaji?
Wiki jana nimetumiwa ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani kuombwa kuzungumzia suala la wazee wastaafu wa iliyokuwa EAC iliyovunjika mwaka 1977, wakidai kupunjwa mafao yao ambayo kimsingi inaonekana walipewa japo kilikuwa kiasi kiduchu, nilionywa katika arafa hiyo kwamba Serikali isifanye makosa kuwadhulumu hao wazee. Hili pia ni tamko la mtu.
Sikumbuki kama kuna tamko lililotolewa na kiongozi yeyote lakini waliotamkiwa huenda bado wanaamini kuna siku watafanikiwa, ushauri wangu matamko haya yanawagusa wengi na kuwaathiri kimaisha.
Hiyo siyo meseji ya kwanza kutumiwa, zipo nyingi sana, zipo zinazonilaumu kwa barua zangu kuonekana ninapendelea upande mmoja, zipo zinazonipongeza wengine wakidai nimezungumza ukweli lakini ndiyo ugumu wa kazi ya kuwaandikia barua wanangu huku nikijua mna vionjo tofauti na mawazo tofauti.
Duniani sasa hivi kuna viongozi wengi na kila kiongozi anatoa tamko lake, wazo langu ni kuwaomba watoe matamko sanjari na utekelezaji, kwa hili la sasa hivi naamini ni haki yao lakini kuna siku machozi yao tutashindwa kuyafuta.
Ili kuweza kwenda sawa na matamko yetu, ni vema tukajipima mahali tulipo kiuchumi kwa maana ya uwezeshaji na mazowea kwa maana ya watendewa, wengi wetu hatutaki kubadilika, tunawaathiri wale wenye kubeba dhamana zetu katika uongozi, kuna siku tutajikuta tunaongea wimbo uleule kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi.
Lazima tubadilike kwa matamko yenye tija kwa jamii yetu, siyo kweli kwamba kila kitu kinategemea rasilimali fedha lakini hata pale panapotegemea fedha hatuna budi kuwekeza ili tuweze kusonga mbele, ni mkosi na laana kubwa kuendelea kuwa maskini au kudumaa palepale kwa kisingizio cha hali mbaya ya kiuchumi.
Matamko haya hayatolewi kwetu tu bali hata ughaibuni, sasa hivi naona mabadiliko ya utendaji wa serikali kubwa kabisa duniani kiuchumi, moto wa kazi umelipuka, kuna mshikemshike wa miaka minne ya kazi na matamko ambayo wengi hawakuyazowea.
Wasaalam
Mzee Zuzu
Kipatimo.