Lazima nianze na salamu na kongole kwa wote ambao mmefunga mwezi huu mtukufu, ni kama vile tumepishana kidogo na wenzetu Wakristo ambao wametoka kufunga, hii ni neema na ninaamini kuna kitu chema kinakuja mbele kutokana na imani za kidini na waumini kuongezeka katika siku za hivi karibuni.
Niwe mkweli kabisa kwamba imani ni kitu kizuri lakini inategemea imani yako umeiweka wapi na je, huko kuna mjibizo wa hiyo imani? Na kama hakuna, basi kuna nini au matarajio yako ni yapi? Maana ni afadhali hata wale ambao wanaomba mvua katika misitu yao kwa imani za kishirikina na mvua ikanyesha.
Nimeamua kusema hivyo kwa sababu kuna uchipuzi uliokithiri wa manabii wa kuchomeana mishumaa vichwani na wanataka tuwaabudu wao badala ya Mungu, naomba tuepuke kikombe hicho kama ikimpendeza Mola.
Basi na niseme naomba kwa pamoja tuunganishe maombi yetu binafsi na kuliombea taifa letu ambalo sasa linaendelea kupita katika kipindi kigumu, kipindi ambacho watu wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu na taifa lao, ni kipindi ambacho tunapaswa kumtoa nyoka meno bila kutuathiri.
Mheshimiwa Rais, mimi ni mmoja wa watu niliokuelewa hata kabla hujachukua fomu ya kugombea urais, huwa narudia kuangalia kale ‘kaklipu ka kule’ kwenye madini ambako ulisema ukigombea urais na ukapata ridhaa ya Watanzania kuna watakaolimia meno, sikaelewi vibaya kwamba lengo lako lilikuwa ni kutukomoa, la hasha, naelewa kwamba ulikusudia tunyooke kutoka katika uzembe na tufanye kazi kwa maana ya kujitegemea, ulisema kama utani lakini nadhani moyoni ulikuwa ukimaanisha.
Najua kuwa malengo yako ulitaka yatimie katika kipindi kifupi sana lakini matarajio yamekuwa si hivyo, laiti kama wakati ule upo mgodini na mimi ningekuwepo ningekuuma sikio la kusema angalia sana wasaidizi wako ambao utawateua au ambao utawakuta, nchi ilifikia pabaya na ulihitaji watu kama wewe maelfu wa kukuunga mkono.
Sasa hivi ukiangalia sana unaweza kuona kama wapo ambao wanakusaidia sana, lakini ukweli ni kwamba wewe mwenyewe kila siku unagundua kuwa kuna baadhi wanakuhujumu, sasa fikiria hauko huku uswahilini ambako tunaona na kusikia mengi, tunakumbana na viongozi ambao mkono wako uko mbali sana kuweza kuwagundua, hao bado hawajaanza kulimia meno isipokuwa walio chini yao wanalimia fizi sasa hivi kwa uongozi wao.
Kwa kauli ile uligundua kuwa tuna kila kitu katika nchi yetu, ulijua kuwa nchi hii ni tajiri kwa mali tulizonazo, hivyo hutaki ukoloni, kwa maana ya kutawaliwa tena, tunaweza kuvuna tulichonacho na tukafanya maendeleo kiasi cha kuwasaidia wengine, nayaona maono yako ya kuwa Tanzania yetu ya miaka ile kutoa misaada katika mataifa mengine ya kusini mwa Jangwa la Sahara.
Najua kichwa kinakupasuka kwa sababu ni kama kila kitu kinafanywa na wewe, lakini umesahahu kuwa moyo wako siyo wangu au wa mteule wako yeyote, huwa naona unavyotatua kero za wananchi kila unapopita, lakini jiulize maeneo hayo huna wawakilishi wako? Je, huna wasaidizi uliowateua? Tatizo ninaloliona ni mizizi ambayo ilikuwepo na haijachimbuliwa. Pole
Ulikuwa na malengo mengi ulikuwa hutaki kufanya mambo kwa mazoea kama zamani kwamba Watanzania wanahitaji kudanganywa bila kufanyiwa kazi yoyote, ulikuwa hutaki vijiwe vya siasa kwa kisingizio cha nchi kuwa na demokrasia ya vyama vya siasa, nilielewa kwa sababu wananchi tulikuwa tukikusanywa na kuaminishwa mambo ya uongo, nilielewa ulivyoruhusu viongozi na wanasiasa kufanya siasa katika maeneo yao, nikaona punguzo kubwa la mabomu ya machozi na kuishi kwa amani.
Nilikuelewa na yapo mengi sana ambayo labda kwa uzuzu wangu wengine hawaelewi hutaki kutegemea kutoka nje bali tujitegemee, hutaki unafiki kwa kuwa mnafiki ni mbaya sana, anaweza akaharibu sifa ya mtu kwa sababu ya malengo yake ya ovyo tu, hutaki majungu na ndiyo maana mtu unampa ukweli wake hadharani, hutaki dili na hili limefanya maisha yamekuwa magumu sana, hapa sasa hata madalali wa vyumba huko mjini wanatakiwa kuwa na leseni ili walipe kodi.
Mambo ni mengi muda ni mfupi Mheshimiwa Rais, tusaidie, lakini tunakwama wapi kusogea hatua chache mbele zaidi? Kuna watu wanakuharibia sana kiasi cha kuwaponza wengine lakini wao bado wapo tu, watu hao ni waongo sana, wanafiki sana, wala dili sana na pengine wanajiita na kujiona wacha Mungu.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.