Nianze na salamu za makabila ya huku kwetu Kusini kwenye mafanikio ya kununua korosho kwa mkupuo, tena bila mizengwe ya kuzungushana wala kupangiwa bei tofauti.

Kuna salamu ambayo nadhani nikiitumia wengi wataielewa kwamba yajayo yanafurahisha, msishangae kutuona mjini kuja kufanya ‘shopingi’ ya vitu vya maana kama magari na mabati mazuri.

Sisi ndio wakulima wa korosho ambao tumesemewa mengi na wakubwa wasio wakulima na wanasiasa, sasa tunasema ‘kuchere’.

Maisha ni safari ndefu sana na maisha ni kipimo cha hadhi ya mtu kwa wakati wake, kwanini leo ni maisha kwetu wakulima wa korosho?

Ni kwa sababu sasa tunaona mwanga wa matumaini kutoka kwa wahusika kuizungumzia korosho na kutupangia bei ili kutukomboa kutoka katika maisha yale ya kubahatisha kila siku.

Hata kama bei tunaona bado haikidhi, lakini mwanzo wa neema ndio huo waja na tunauona. Tukichanganya baadhi ya mambo muhimu kwa binadamu kama wakulima tuliosahauliwa, tunaanza kuona kuna mwanga wa kuishi kama binadamu.

Kuna daraja letu lililotuunganisha na dunia, kuna bima ya afya, kuna umeme wa REA, kuna maji salama, kuna shule na madawati, walimu tunawaona wakianza kuipenda Kusini. 

Mpaka hapo nadhani maisha yanaanza, zamani nilikuwa napenda sana siasa. Miaka kadhaa iliyopita nilianza kupoteza hisia zangu juu ya siasa na kwa kweli nilianza kuichukia siasa na hili nilisema sana kwa sababu ilifika mahali niliona kama siasa ni mfumo wa watu wachache kutudanganya tulio wengi. 

Siasa kwangu ulikuwa mwiba katika mambo mengi, siasa ilinichelewesha kujua hatima ya daraja la hapo karibu ya Nangurukuru. 

Siasa kwangu niliichukia kwa sababu nilikuwa naishi mbali na viongozi wangu, niliichukia siasa kwa sababu iliwafanya viongozi kuwa miungu watu na waliweza kutununua watakavyo kutokana na shida ndogondogo kama za korosho.

Nilikuwa sielewi kuna tatizo gani hapa kwetu, kila siku kunaibuka jambo kubwa na waibuaji ni watu wachache. 

Utasikia kuna watu wamefanya dili kubwa la hela kupitia migongo yetu au mali ya umma. Nilikuwa sielewi hiki kiburi kinatoka wapi, nilikuwa najiuliza, nini hatima ya taifa letu? Nikawa nakumbuka miaka michache tu iliyopita juu ya uaminifu na uzalendo uliotukuka na jinsi ulivyopotea ghafla, nchi yetu ilikumbwa na kadhia ya uchumi wa hatari.

Wengi hawajui tumetoka wapi, wengi hawajui nchi hii ilikuwa na nini miaka ya nyuma, mimi nakumbuka viwanda vingi sana ambavyo vilitapakaa katika nchi hii yenye neema ya mito na maziwa.

Nakumbuka mashamba makubwa na shehena za vyakula na mazao ya biashara, nakumbuka viwanda vilivyokuwa vikiajiri maelfu ya Watanzania kila uitwao mkoa. 

Nakumbuka uvuvi na ufugaji, nakumbuka hata mshahara wangu wa kima cha chini ulivyoniwezesha kuishi kwa siku za mwezi mzima huku nikipata moja – mbili katika stoo ya bia, yale ndiyo yalikuwa maisha.

Tulikuwa na nini zamani na wapi tulikosea? Nadhani hili swali litawahusu sana dotcom ambao wanadhani maendeleo ni kujilinganisha na kujifananisha na mataifa mengine yenye utamaduni tofauti na wetu.

Nadhani lawama ziwaendee wale wote waliokwamisha jitihada za Tanzania kujitegemea kwa kufanya mambo ya hovyo kama uwekezaji wa kujipendelea na kuuza mali za umma kwa manufaa yao binafsi, hawakuwa wazalendo kabisa.

Naipenda hii spidi japo naona jinsi inavyonikunja vibaya kiasi cha kuivunja nyonga, lakini hakuna namna, ni lazima tufanye hivyo. Ni lazima watu watoke damu na jasho ili tuweze kurudi pale tulipokuwa.

Angalia viwanda vya korosho katika nchi hii vilikufa kwa sababu zipi wakati tuliweza kuvianzisha tukiwa si wasomi na wasomi mlipokuja na u-dotcom vikafa kifo cha maisha.

Swali langu ni moja tu, tutarajie nini sasa kwa nia ya kufufua uchumi wetu? Kama mimi ningekuwa bado mwanasiasa wa kweli wa enzi zile, basi ningehakikisha yale mabaki yote ya viwanda vyetu yanafufuliwa na kuanza kazi.

Viwanda vya nguo, ngozi, nyama, madini, pembejeo, mafuta, redio na betri, viatu, chakula na kadhalika.

Sisi wazee tunadhani tuanze hivyo bila kuoneana haya, watu watoke jasho na damu ili turudi pale tulipokuwa ndipo tuanze hayo mengine ya nje ya nchi tukiwa na chetu mikononi.

Maisha ya leo ndiyo tunayohitaji, yajayo yawafurahishe wao.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.