MAGUFULIKwanza nadhani walifikiri ni mabadiliko ya chama, walibweteka wakawa hawajihusishi na siasa, kumbe walisahau kale ka wimbo ketu ka TANU kwamba chama kinashika hatamu, na kwamba watumishi hawa waliamini kuwa Serikali na chama ni vitu viwili tofauti.

Nimeanza kwa kukupongeza kwa hatua mbalimbali ambazo umezichukua na ukitoa taarifa awali kwamba ni mwanzo wa kazi inayoendelea, yaelekea safari bado ni ndefu ya maumivu kwa watumishi wa umma waliogeuza ofisi za umma kuwa vijiwe vyao vya kujipatia mapato.

Kuna pongezi nyingi nyuma ya lawama chache zinazokuzwa na hao wasiotaka mabadiliko, lakini walikuwa wa kwanza kuimba kibwagizo cha mabadiliko bila kujua kuwa mabadiliko waliyokuwa wakiyataka walikuwa hawajui ni mabadiliko gani.

Kutokana na uzoefu wangu, watumishi wa Serikali walikuwa ni miungu watu, walikuwa na ukiritimba mkubwa uliokithiri kiasi cha kuwafanya wananchi waamini kuwa Serikali wanayoichagua kupitia vyama huenda ni nyingine na ile ambayo inaongoza baada ya uchaguzi.

Mheshimiwa Rais, ulipoanza na hospitali watu hawakukuelewa na wapo waliodhani kuwa unafanya kazi ambayo siyo yako, wapo waliosema unafanya kazi na vyombo vya habari kwa kuwaonesha wapiga kura na kwamba hiyo ni nguvu ya ‘soda’, nguvu  ambayo itanunulika na wenye nguvu ya pesa.

Kwa jinsi unavyowaomba Watanzania wakuombee kwa Mwenyezi kwa  dhati ya moyo wako ili uweze kukabiliana na kupambana na vita kubwa ya umaskini, nakufahamisha watu  wengi wanafanya hivyo, lakini pia wapo wanaoomba uishiwe nguvu iwe nguvu ya soda waweze kufanya yao, waweze kuirudisha serikali yao ya ukiritimba.

Mheshimiwa Rais, kuikabili Tanzania yenye sura ile ya ufisadi, rushwa, ukiritimba, uzembe, uvivu, umwinyi na kadhalika ni kazi ngumu sana, unahitaji kuwa na roho ngumu kwelikweli, wapo ambao wanasema wapo nyuma yako lakini nakuahidi ukigeuka huwaoni kutokana na dhamira za kinafiki walizonazo juu ya kupambana na hatari iliyoko, mimi nakushauri uwe unageukageuka ukiona kuna mtu haonekani basi mtoe mapema katika safu yako.

Hawa watumishi siyo kwamba wamebadilika, bali wanafanya kwa hofu, wanatafuta njia nyingine mbadala ya kuishi, waligeuza ofisi za umma kuwa vioski vyao vya kuuza huduma kwa wananchi, waligeuza miradi ya ofisi kuwa mali zao, waligeuza mapato ya Serikali kuwa ni sehemu yao ya kujilimbikizia hadi wengine wakakufuru.

 

Una mtihani mzito Mheshimiwa Rais, unatupiwa mawe pande zote za dira ya kulifilisi Taifa hadi sasa unajitahidi kuyakwepa, lakini unaweza ukachoka na ndiyo maana Watanzania wengi wanakuombea ushinde hilo na uweze kufikia malengo yako ambayo ndiyo kiu yao ya siku nyingi tangu na baada ya Uhuru.

Magufuli, nchi ilioza, ilioza kwelikweli na ndiyo maana unafahamu kwa kuwa ulikuwamo na ingelikuwa vigumu kujifanya wewe si miongoni mwao na ndiyo maana kutokana na utumishi wako katika baadhi ya wizara umekufanya uwe hapo ulipo kwa kumsukuma mlevi.

Dhima kubwa uliyokuwa nayo ni kuthibitisha kuwa unaweza ukapambana na machifu ndani ya Serikali, Serikali ambayo imeajiriwa na wapigakura, hawa wapigakura na wengine walimwona mtumishi wao Serikali amechukua madaraka kwa nguvu na kuanza kuwatisha badala ya kuwahudumia.

Watumishi wanatakiwa waelewe kuwa wao ni waajiriwa wa wananchi na kwamba wananchi wanahitaji kupata huduma pasi na kutokusumbuliwa, ile dhana ya kwamba wao wapo juu ya sheria iwe mwisho lakini pia wajue kuwa wanapaswa kujibu kwa mwajiri makosa yao wakati wanapokosea.

Magufuli, ukiritimba uliokithiri katika Serikali yako utaisha siku moja tu iwapo wewe kama kiongozi mkuu utasema inatosha, utaisha kwa wengine kuona kama wanaonewa kutokana na mazowea, utaisha wengine wakitengeneza makundi ya kutafuta uhalali wa kuwa umewakosea, utaisha kwa wengine kujipatia maendeleo yanayowahusu kupitia Serikali yao.

Ombi langu, bado una kazi ngumu katika vitengo vingi vya Serikali, kuna vijimungu watu katika vitengo ambavyo umeweza kuvifanyia kazi ama uko katika mchakato wa kuvifanyia kazi, kwa hiyo tembea na watu upate viatu, wananchi watakwambia yanayojiri katika Serikali waliyoiajiri.

Sisi tupo pamoja nawe, lakini usikubali kiongozi anayekwambia yupo nyuma yako na ukigeuka humuoni, tuamini sisi wananchi lakini siyo tuliowaajiri.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.