Nianze kwa kusema kabisa kwamba chondechonde madalali kutumia akili ni jambo jema, nguvu si uungwana hata kidogo, inafedhehesha taaluma yenu na kuwafanya watu wawaogope kwa ujinga na siyo kwa heshima kama ilivyo kwa taaluma nyingine.
Leo nimeamka nikifikiria sana masakata ya madalali wa aina nyingi, lakini nimejikita zaidi na madalali ambao wana leseni maalumu kisheria za kufanya kazi hiyo. Dalali ni mtu muhimu sana katika jamii yoyote ile, na dalali ni mpatanishi wa pande mbili zilizosigana, dalali siyo sehemu ya uchochezi na ukomavu wa ugomvi kwa pande mbili zilizosigana.
Miaka kadhaa ya nyuma niliwahi kukutana na sekeseke la madalali kutaka niondoke ninapoishi kwa muda wa nusu saa, mahali hapo nimeishi kwa miaka thelathini na nimewekeza vitegauchumi na mali zangu mbalimbali, lakini nilitakiwa niwe nimepasafisha na kuhamisha mali zangu katika muda wa nusu saa, ni mjinga tu inaweza kumuingia akilini kwamba anaweza akahama katika muda huo.
Kabla ya kupata uhuru tulikuwa na kodi ya kichwa, hii ilijumuisha mali kama vile baiskeli na mashine za kusaga, wachache wanaweza kukumbuka, kodi pekee ambayo watu waliweza kuhama na kuishi misituni ni kodi ya kichwa, maana unaondoka nacho hakibaki na kuonekana dhahir shahir, na wakati huo wa mkoloni ilikuwa ukishikwa kwa kosa la kutolipa kodi unapelekwa kwa jumbe na jumbe anatoa idhini ukakabidhi mali inayolingana na kodi unayopaswa kulipa.

Ni wakati wa ukoloni na ustaarabu ulikuwa juu sana, waliokimbia hawakufukuzwa kama wezi badala yake walikamatwa na haki ya kimsingi kusikilizwa kabla ya kuhumiwa ilifanyika, hiyo ilikuwa ni wakati wa ukoloni na waliokuwa madalali wa kufuatilia masuala ya kodi walikuwa wananchi ambao uwezo wao kielimu nadhani kila mtu anajua.
Siku za hivi karibuni, kumeibuka ujangili wa madalali kufanya kazi kwa njia ya uadui na wateja wa watu wengine, kwa ufupi wanachafua taswira ya taasisi muhimu za Serikali na mashirika mbalimbali ambayo yana heshima yake kwa jamii.
Wamekuwa wakifanya kazi kama askari aliyeziba masikio, hasikii la mwadhini wala la mnadi swala, wamekuwa kero kubwa sana hata kwa watu wengine ambao hawahusiki na matukio yoyote ya kudaiana, ni vurugu ambayo imeibuka hivi sasa na kusababisha hasara na watu kutojiamini. kwa ufanyaji kazi wao, kumeibua kundi jingine ambalo linafanya kazi kama wao lakini hao ni wezi.
Siku za hivi karibuni, tumeshuhudia madalali wakishindwa kutumia busara ndogo sana isiyohitaji shule wala umri, kujua ni jinsi gani wanaweza kutatua tatizo lililopo bila kuleta athari ya kisaikolojia na heshima ya Taifa na vyombo husika. Tumeshuhudia watu wakikamata magari kwa mgongo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mikopo ya benki, ukifuatilia kuna baadhi ya makosa ambayo yanafanyika kwa baadhi ya wadaiwa.
Tumeshuhudia nguvu badala ya busara, tumeshuhudia ujinga badala ya hekima na baadhi ya watu wamediriki kutangaza kuwa kumekuwa na dhuluma na upotevu wa mali na muda, kwa mambo ambayo hayakustahili, hivi ndivyo vyombo vyetu vilivyosajiliwa kisheria vikifanya mambo ya aibu kwa karne hii.
Naunga mkono juhudi zote za Serikali kukusanya mapato, lakini pia siungi mkono kwa baadhi ya taasisi kuzipatia kazi ya kukusanya kodi ambazo hazina uelewa na mawasiliano na wadaiwa kwa kuamini wao ndiyo kila kitu. Taifa linawategemea walipakodi na walipakodi wanalitegemea Taifa, kwa hiyo wanategemeana.
Nadhani kuna haja ya makampuni na taasisi mbalimbali kuangalia wanampa nani dhamana ya kufuatilia madeni na jinsi wananavyoshughulika katika ufuatiliaji, ni aibu kubwa na wanaleta fadhaa kwetu na kwa majirani.
Lakini mbali na yote, imefikia mahali unaposhindwa kutofautisha yupi ni jambazi na yupi ni mtu salama kutokana na utendaji wao, inafika wakati unashindwa kuelewa uelewa wa kila anayeitwa dalali iwapo hafungui mwanya wa kutaka kusikilizana, ni ujinga kuikamata gari yenye mgonjwa mahututi anayepelekwa hospitali kwa deni la laki moja, thamani ya utu tunaitupa kwa fedha!
Leo nimeanza na hili kidogo, nitaandika barua rasmi kwa vyombo husika ili wajue jinsi dhamana zao walivyoziweka rehani kwa wahuni.

Wasaalam
Mzee Zuzu
Kipatimo.