Leo nimeamua kutotaka salamu wala kusalimia mtu, nimeamka na hili la mabango ya waganga wenye vibali vya kujitangaza kutibu magonjwa yaliyoshindikana hospitalaini na makanisani.

Hata sielewi ni nani hasa ambaye anaweza akawajibika kwana kesi hii siku ya mwisho pale palapanda itakapolia huko mawinguni na akalakiwa na kupelekwa motoni kwa kuacha dhambi kubwa kama hii ikiendelea kutendeka mbele ya macho yake huku akijua dhahiri kwamba ana dhamana ya kusimamia suala la wizi wa kimazingara unaoendelea.

Inawezekana nikawa nimepitwa na wakati na sijui sheria zinasemaje kuhusu hili kwa sababu siku hizi naona mambo yanakwenda kasi sana, ukilala na kuamka kuna sheria mpya zinatangazwa, hasa huku vijijini ambako nako kuna sheria ndogondogo za kijiji ambazo zinapitishwa na kamati ya utendaji wa kijiji husika.

Nina utamaduni wa kufanya ziara za kushitukiza kila baada ya kuuza mazao yangu, lengo langu hasa ni kujua dunia inakwenda kwa kasi gani bila kuachwa, zipo kasi ambazo nakubali kupitwa na zipo ambazo lazima niende nazo kasi vilevile. Kuna kasi ya kuvaa nguo chini ya makalio, hiyo nilijificha ndani na sikutaka niingie katika mtego huo, kuna kasi ya kujiunga na mifuko ya bima ya afya, hiyo nilikula nayo sahani moja kuhakikisha kuwa ninajiunga ili niweze kupata matibabu kwa wakati na dawa.

Suala la bima ni muhimu sana na ninakubaliana nalo kwa asilimia zote pamoja na upungufu wake mkubwa ambao sisi kama wateja tunaupata pale tunapopata matibabu. Yale masuala ya kunyanyapaliwa yamekwisha ila masuala ya kukosa dawa katika kituo husika ni changamoto ambayo kimsingi lazima iangaliwe upya.

Suala jingine ni kuunganishwa katika matibabu ambayo ni gharama ili hao wenye hizo hospitali waweze kupata fedha na ndipo suala la mgonjwa kuitwa mteja lilipofikia, ukifika hospitalini jiandae vipimo vya ajabu na kuondoka na kiroba cha dawa, hii ni kwa hospitali ambazo kimsingi zimekosa maadili ya kazi na weledi katika kutoa huduma.

Naomba siku moja mifuko hii iendeshe kura za maoni ili wazijue hizo hospitali, zahanati na vituo vya afya.

Hapa sikupitwa na wakati hata kidogo, sasa hivi nikijisikia mgongo unauma, nawahi hospitalini kupata matibabu, tofauti na yule aliyechanga karata zake kununua suruali fupi ya kuvalia chini ya makalio au wigi la kuendea katika shughuli fulani ya kusutana, ndiyo dunia inakwenda kasi na sisi lazima tuchague mambo ya kwenda nayo kasi, vinginevyo itabaki aibu na kuomba michango kila siku kwa marafiki.

Sasa leo nimeamka katika mji wa watu, nimeamkia maeneo ya jiji la wasafi, sitaki kulitaja lakini jambo kubwa nililokutana nalo na kuamsha akili yangu kwenda kasi ya ajabu ni hili la matangazo ya waganga wa kienyeji, tena wakielezea magonjwa wanayotibu na mengi ya hayo magonjwa ni yale ambayo matibabu yake huwezi kuyapata hospitalini.

Nimeona tangazo lenye namba ya simu kabisa katikati ya mji huo likielezea matibabu ya kuwa freemason na kwamba unaweza ukawa tajiri katika kipindi cha mwezi mmoja, nikaduwaa na kujiuliza, hivi huyu mtaalamu serikali imeshindwa kumuona akaitibu serikali yetu iwe freemason ili tuweze kujikomboa na hii hali ya uchumi? Au ndiyo kusema yeye anaweza kutoa huduma hiyo kwa mtu mmojammoja tu na si taasisi? Je, mahitaji yake ni yapi?  Malipo yake anapokeaje?  Kodi yake analipaje?

Nikajiuliza wenye mamlaka ya kutoa leseni kwa hawa watu ni nani? Sikupata jibu, nikaona bora niwaulize waliotangulia na kasi ya nchi yetu labda wanajua, nikajisemea moyoni, hawa waganga mbona hawana bima ya afya? Kwanini wawe na uwezo wa kutibu magonjwa ambayo hospitali zimeshindwa na wasiwe na bima ya afya? Wanatibu nguvu za kiume, akili za darasani, kumrudisha mtalaka, kufaulu bila kusoma, kupata kazi, kisukari, ukimwi na kuokota fedha.

Nikaona niwaulize walio na mamlaka ni nani yuko juu yao? Je, tunayajua madhara ya utapeli wa namna hii unavyoendelea kuachiliwa bila kuchukua hatua?

Na kama si utapeli, kwanini watu hawa wasitumike kwa manufaa ya taifa? Basi naomba niseme kama kuna mtu anamjua mganga wa hivyo anisaidie namba yake nataka nipate ubunge katika uchaguzi ujao.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.