Nianze kuwapongeza Watanzania wote kuingia katika awamu nyingine ya tano ya uongozi wa nchi hii, tukiwa salama salimini na amani yetu ikiwa ipo pasi na maombi mabaya ya watu wa nje na ndani ya nchi yetu, katika kutuombea tupatwe na mabaya katika mabadilishano haya
Nawapongeza Watanzania kwa kuamua kutaka amani, nawapongeza Watanzania kwa kutokubali kununuliwa na watu wachache wenye tamaa ya madaraka, nawapongeza Watanzania kwa uelewa wa umuhimu wa amani na mwisho nawapongeza Watanzania kwa kuendeleza utamaduni wetu wa amani.
Sasa ni wiki ya tatu imeanza baada ya bendera ya utawala wa awamu ya nne kushushwa na kupandishwa kwa bendera ya awamu ya tano. Mengi tumeyashuhudia katika kipindi hiki kifupi cha uongozi wa awamu ya tano, nawapongeza sana wale wachezaji wachache ambao wameweza kuhimili kuiendesha Serikali bila kuwa na wasaidizi kwa kipindi kirefu, kumbe kila kitu kinawezekana kama tukiamua.
Katika kipindi hiki kifupi tumeona mabadiliko mengi, tumeona wafanyakazi wa Serikali wakiwahi maofisini, wakifanya kazi kwa bidii na uwepo wao mahala pa kazi ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana kwa wiki chache tu.
Katika kipindi hiki tumeona majipu kadhaa yakikamuliwa na wenye kusikia uchungu ni watu wakubwa wakubwa waliokuwa wakiamini kuwa Serikali ni wao na wakasahau kuwa waajiri wao ni Watanzania wapigakura, hilo lilianza kuoneshwa na mkuu wa nchi siku chache tu baada ya kutinga Ikulu.
Alianza kwa kupiga marufuku safari za nje ya nchi, safari ambazo ziliigharimu Serikali mabilioni ya shilingi ambayo yangeweza kuingizwa katika mpango wa maendeleo ya nchi yetu, alipunguza gharama za vikao na sherehe, alipunguza baadhi ya kazi ambazo alijua fika kuwa zingeongeza gharama kwa Taifa letu, haya ndiyo mabadiliko ambayo nilikuwa najua nayahitaji kwa muda mrefu, na yapo mengi ambayo natabiri yatakamilika baada ya safu ya Serikali ya Awamu ya Tano kukamilika.
Nianze kwa kumpongeza Rais kwa uamuzi wa kuonesha mfano kwa viongozi wengine, kiongozi ndiye anayekuwa kioo kwa viongozi wenzake, ameanza kwa kufanya uamuzi mzito katika sekta mbalimbali na baadhi ya viongozi wengine nao wakaamua kuchukua hatua kabla Rais hajawashukia na kuchukua hatua dhidi yao. Kumbe kila kitu kinawezekana kama tukiamua.
Rais alijinasibu bayana katika kampeni zake, matumaini ya Watanzania yakaangukia kwake na Watanzania wameridhika na utawala wake katika siku za awali tu kuelekea katika kipindi cha miaka mitano. Simjui vizuri Rais lakini kwa mujibu wa maelezo ya watu wa karibu yake hana nguvu ya soda na nguvu yake ni mwanzo hadi mwisho. Katika hili naomba tumuombee afya njema aweze kukidhi mahitaji ya Watanzania katika kipindi chake.
Rais amekuwa msiri ili aweze kutekeleza kile anachokiamini, alifanya siri hata katika uteuzi wa waziri mkuu ambaye pamoja na kwamba alitajwatajwa lakini haikuwa kwa nguvu zile ambazo wengine walihusishwa nazo. Kwa bahati nzuri hata yeye waziri mkuu mteule hakujua kwamba anachaguliwa, naamini kwa kitendo cha kuaminiwa na kiongozi wake hatafanya ajizi katika kuitetea ilani ya chama chake na hatathubutu kumwangusha aliyemteua.
Nakumbuka wakati wa Julius kulikuwa na aina fulani ya kufanana na matukio kadhaa ya kiuongozi ambayo nimeyaona, mojawapo ni lile la Julius kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Lwanzali mkoani Njombe kwenda kutoa zawadi kwa kijiji hicho bora, alitumia Land Rover chache na viongozi wachache kwenda kuhimiza maendeleo.
Wakati rais wa awamu ya tano alipokuwa akitakiwa kwenda kuhutubia Bunge na kufanya uteuzi wa waziri mkuu wiki jana, tumeshuhudia udogo wa msafara na namna ya usafiri alioutumia, tumeshuhudia hafla fupi isiyo na mbwembwe nyingi wala gharama, tumeshuhudia usiri mkubwa ambao ulimliza waziri mkuu mteule. Inasemekana alikuwa akifunga vitu vyake ahame katika nyumba ya Serikali.
Sasa kuna baraza la mawaziri, nataka kuamini kuwa hakuna aliyezaliwa akiwa waziri au kusomea uwaziri. Mheshimiwa rais, nakuomba chagua viongozi unaoamini wewe kwa moyo wako kuwa wataenda na kaulimbiu yako ya ‘hapa kazi tu’. Usikubali kuletewa jina na wathibitishie Watanzania kuwa wewe ndiye John Pombe Magufuli, mzee wa misimamo na tingatinga.
Naamini Mungu atakuongoza katika kutatua kero za Watanzania kama ulivyoahidi, na najua humtamki Mungu kwa kuwapendeza Watanzania bali unamaanisha, hata siku uliyokula kiapo ulilitaja jina la Mungu mara kumi na tano katika hotuba yako fupi ya dakika kumi. Mungu awe kimbilio lako na watendee Watanzania ulichokiamini, utakumbukwa daima.
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.