Nakumbuka zamani wakati wa machifu, waliokuwa viongozi wetu wa kijadi, walikuwa wanamiliki mashamba kidogo, wake kidogo, na mali ya jamii inayowazunguka. Mali iliyomilikiwa na chifu na ambayo kimsingi ilikuwa ya jamii ni pamoja na mashamba, chakula, busara, na uamuzi mzito wa jamii husika.
Nchi hii wakati tunautafuta uhuru, tuliheshimu utawala wa kijadi, yaani machifu waliokuwapo na waliotangulia mbele ya haki. Mtanzania yeyote aliye na akili timamu ukimuuliza majina ya machifu anaweza kukutajia pamoja na sifa zao. Hakuna hata chifu mmoja aliyekuwa na dhuluma kwa jamii yake au aliyetenda maovu juu ya jamii aliyokuwa anaitawala.


Hawa ndiyo machifu wa Tanzania ambao wengi wao hawakuchaguliwa na wananchi. Ilikuwa inatokea tu kutokana na kauli zao thabiti na misimamo yao juu ya wananchi wao, na utawala ule ulikuwa wa kurithishwa wakiamini kuwa hata watoto wao watakuwa na chembechembe za busara kutoka kwa wazazi wao.
Hili halina mjadala katika kuthibitisha utawala wa kichifu, ninaloweza kuthibitisha ni jinsi machifu hawa walivyoshindwa kujilimbikizia mali au kuwa wafanyabiashara pamoja na kumiliki ardhi na watu wao. Ipo dhana ya shanga na utumwa na ipo dhana ya madini na zawadi mbalimbali kwa machifu.
Wakati wa utawala wa machifu kulikuwa na matajiri ambao wengi wao walikuwa wakiheshimu uamuzi wa machifu. Hawa walikuwa wafanyabiashara na wengi wao walipata ridhaa ya machifu katika biashara zao. Wapo waliomiliki maduka, magari, majumba na vito vya thamani.


Pamoja na utajiri wao bado waliweza kuheshimu utawala wa chifu, na walishirikiana na utawala wa chifu walipohitaji msaada au chifu alipohitaji msaada wao kwa ajili ya jamii anayoitawala. Kimsingi hapa ndipo utakapojua kuwa utawala ni kipaji na siyo pesa au nguvu ya wapambe.
Nimeamua kuwaandikia barua hii leo baada ya kufanya marejeo katika kijitabu changu cha zamani sana cha Azimio la Arusha, kijitabu ambacho kimsingi kilitambua nguvu ya fedha katika utawala na uamuzi unavyoweza kuathiri jamii inayotawaliwa.
Kitabu hiki kinasema wazi kuwa wafanyabiashara siyo viongozi, wanaomiliki mali siyo viongozi, wanaomiliki vito vya thamani siyo viongozi. Kiongozi ni mfano wa jamii anayoitawala, kiongozi anatakiwa kufanya kazi ya uongozi na siyo kufanya kazi ya biashara.


Leo tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi, nikaona ni vyema nikalikumbusha hili, kwamba kiongozi huzaliwa na karama ya uongozi kama ilivyo kwa wafanyabiashara kuzaliwa kutoka katika familia za biashara, uongozi unaweza kuwa wa kubembelezwa kutokana na hekima ya mtu lakini mtu hawezi kuuza hekima kwa wananchi kwa kutumia fedha.
Kuna malalamiko mengi ambayo yanatolewa na watu wengi wakiwamo wagombea nafasi mbalimbali hapa nchini. Wapo wanaowatuhumu wengine wakisema wanatumia fedha kutafuta uhalali wa hekima, wapo wanaosema kwamba wengine wana nafasi kwa sababu ya fedha walizonazo. Kimsingi mimi hili sikubaliani nalo, ninachoweza kukubaliana ni suala la hekima na si vinginevyo.


Iwapo mtu hana hekima hawezi kuinunua, labda wanaodhani hana hekima ndiyo wanaoweza kununulika. Chama ni kilekile na kinafuata taratibu zilezile za uteuzi wa kiongozi, hakiangalii sura au kusikiliza majungu ya watu, kiongozi hunadi sera na siyo kunanga mtu. Ya Kaizari mwachieni Kaizari na yetu tupeni siye.
Chama kimetangaza sifa za rais, anayejiona hatoshi anaweza kutafuta kazi au biashara nyingine tofauti na uongozi, kwa kuwa uongozi ni karama na kipaji, uongozi ni suala la ukoo kama ilivyo biashara, uongozi mtu huzaliwa nao, kiongozi hata awe na umri mdogo hekima humtenga na kumfanya kuwa kiongozi wa jamii.
Kiongozi lazima awe na uwezo wa kuongoza taifa na siyo familia, lazima awe mwadilifu, awe na elimu ya kutosha au ufahamu mkubwa, kiongozi ni lazima awe anaweza kutuunganisha na siyo kututenganisha katika muungano wetu, awe mwepesi wa kusoma alama za nyakati sasa na baadaye, asiyumbishwe hata na familia yake – awe mume au mke.


Kiongozi wetu si wa kwetu peke yetu, sisi siyo kijiji, ni miongoni mwa mataifa mengine, kwa hiyo lazima awe na uwezo wa kutufanya kuwa miongoni mwa wenzetu duniani, asiwe katili. Kiongozi lazima uwe na subira katika kutoa uamuzi mzito.
Kiongozi ni lazima awe anawajua anaowatawala, aheshimu unyonge wao na kuufanyia kazi, asipende kujikweza, akipende chama chake na atetee maslahi ya taifa, asijilimbikizie mali ikiwezekana afe maskini kwa ajili ya taifa lake, akubalike na wanaotawaliwa na awe muwajibikaji wa dhati. Hili ni ombi langu kwenu wapiga kura. Ya Kaizari hebu mwachieni na yetu tupeni.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.